DAR ES SALAAM

NA THEONESTINA KAIZA-BOSHE

Katika mpango wa kuwahamisha wafugaji na mifugo yao kwa hiari kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA) kwenda Kijiji cha wafugaji Msomera, Handeni mkoani Tanga, serikali imefanya tukio kubwa la kipekee na la kihistoria. 

Japokuwa hatua hiyo ilibeba gharama kubwa mno, ni hatua ya kipekee na ya serikali kujivunia. Hata hivyo, katika sakata zima la migongano ya wafugaji wa NCA na pia katika Pori Tengefu la Loliondo dhidi ya uhifadhi wa wanyamapori kwenye maeneo hayo, serikali inayo ya kujifunza kama kweli inataka kukomesha migogoro ya namna hiyo nchini.

Kwanza, tuangalie mazuri na ya fahari yanayotokana na sakata hilo. Kubwa ni kwamba, kwa wafugaji kuhama kwa hiari NCA ni kama ilivyo kwenye usemi wa “kulala maskini na kuamka tajiri”.

Hii ni kwa maana wametoka kwenye eneo lisilojitosheleza kwa mahitaji ya malisho, maji na huduma za kijamii kwenda kwenye kijiji chenye mahitaji yote ya mifugo na makazi ya binadamu; tena ya hali ya juu. Ni mahali ambako hawahitaji kwenda mbali kutafuta maji na malisho kama ilivyokuwa walikotoka.

Ni kijiji kilichoandaliwa kwa ukamilifu wa kipekee; ikiwa ni pamoja na nyumba za kisasa na huduma zote za kijamii. Na kwa wale wanaopenda kuendelea kuishi kwenye nyumba za kiasili wamehakikishiwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kujengewa, wakitaka.

Hapo nimezungumzia uzuri wa uamuzi huu kwa wafugaji; kuna pia mazuri ya serikali ya kujivunia na kupongezwa. Serikali kuweza kufanya yaliyotakiwa kufanya katika kuhifadhi ikolojia ya Serengeti, na kuwatimizia wafugaji madai yao sawia, si jambo dogo kwa nchi yotote kufanya katika kipindi kifupi kama tunavyoona.

Hii ni kwa maana ya kuweza kufanya mipango thabiti na kuitekeleza kwa gharama kubwa katika muda mfupi pasipo kutetereka. Jingine ni kuweza kuzima kelele za wachochezi kwa namna isiyoacha shaka, kuanzia wanasiasa wa jamii husika hadi asasi zisizo za kiserikali (AZAKI) zilizokwisha kujijengea ushawishi mkubwa.

Licha ya mazuri ya kuhamisha wafugaji kutoka Ngorongoro kwenda Handeni, kuna walioilaumu na hata kuishutumu serikali kufanya mambo kisiasa. Hili sioni kama ni kosa, bali naliona kama kutimiza wajibu kwa upande wa Serikali Kuu. 

Hii ni kwa sababu migogoro ya NCA na Loliondo ilihusu malalamiko ya wananchi kuhusu masilahi yao kijamii, hivyo ilibidi serikali iingilie kati kwa namna ambayo ingetoa jawabu au suluhu ya mgogoro, kuwafariji waathirika, na hapo hapo kuzuia uvunjifu wa amani.

Isitoshe, kulishakuwa na dalili za kuvunjika kwa amani kulikokuwa kunachochewa na wachochezi, wengine wakiwa na ushawishi mkubwa na nguvu ya fedha; ikiwa ni pamoja na wa kutoka nchi ya jirani na mashirika ya kimataifa; mambo yaliyofanya utatuzi wa migogoro hiyo uwe nje ya uwezo wa wahifadhi.

Ni muhimu ieleweke kuwa migongano ya wafugaji na uhifadhi wa wanyamapori Loliondo, na hata NCA imekuzwa na wachochezi kwa kutumia uongo. Nafasi hairuhusu kuongea kwa kina na upana kuhusu uchochezi na wachochezi katika migogoro ya wafugaji na uhifadhi wa wanyamapori katika Wilaya ya Ngorongoro; ikibidi iwe mada ya wakati mwingine.  

Hivyo, kwa makala hii itoshe tu kugusia mambo mawili ya uongo yaliyotumiwa kuteka akili za wasiojua uhalisia wa masuala husika.

Uongo wa kwanza ni unaosemwa kuwa eneo la Pori Tengefu la Loliondo linalowekewa mipaka – kilometa za mraba 1,500 ni makazi ya Wamasai tangu enzi za mababu zao, na kwamba kwa kuwaondoa humo serikali inawapoka haki ya binadamu. 

Hii si kweli. Kwanza, kisheria eneo likiwa na hadhi ya Pori Tengefu hairuhusiwi kufanya makazi humo, isipokuwa kwenye Hifadhi ya Ngorongoro (NCA), ambamo Wamasai walianza kuishi mwaka 1959.

Kabla ya hapo eneo la Ngorongoro Crater lilikuwa Closed Reserve, hadhi iliyokuwa nayo tangu mwaka 1921, na ambayo haikuruhusu makazi, mifugo, wala kilimo. 

Wamasai walipohamishiwa humo waliruhusiwa kuishi humo na mifugo yao kama ilivyokuwa asili yao; pamoja na kufanya kilimo kidogo kinachodhibitika. Hii iliifanya NCA kuwa hifadhi ya matumizi mseto ya ardhi ya kipekee nchini. Hata hivyo, dhana hii haikufanikiwa na ikaibidi serikali kuondoa kilimo katika marekebisho ya sheria ya mwaka 1975.

Uongo mwingine ni maelezo kuwa eneo linalohifadhiwa ni la vijiji vya wafugaji. Eneo hilo ni sehemu ya pori tengefu, hivyo haliwezi kuwa sehemu ya makazi. 

Kisheria hairuhusiwi kufanya makazi, na hata kulisha mifugo, kwenye pori tengefu, pasipo kupata kibali maalumu kutoka kwa mamlaka husika. Aidha, kupandisha hadhi pori tengefu kuwa pori la akiba, kisheria ni utaratibu sahihi.

Baada ya kusema hayo, napenda kueleza ninachokiona kikiwa upungufu kwa upande wa serikali, na kuhimiza isiache kujifunza kutokana na somo lililojitokeza Ngorongoro na kwingineko kunakojitokeza migogoro baina ya binadamu na uhifadhi wa wanyamapori.

Somo lenyewe ni kwamba katika migogoro ya aina hii chanzo kinakuwa ni wahifadhi kutotimiza wajibu wao ipasavyo na serikali kuchelewa mno kuchukua hatua.

Serikali, mathalani, kwa ngazi ya wizara, ikichelewa kuchukua hatua kutatua matatizo ya kiutendaji ngazi ya hifadhi, inasababisha matatizo kukua hadi kuzua uhasama baina ya wananchi na wahifadhi; na hata kuwa na mtazamo na matendo hasi dhidi ya uhifadhi wa wanyamapori hadi hali inakuwa tete.

Hali hii ndiyo inasababisha kuibuka kwa wadau mbalimbali wenye nia tofauti tofauti, jambo linalozua migongano ya kimasilahi, kuibuka kwa wachochezi, na hatimaye taharuki na uvunjifu wa amani. 

Hivi ndivyo ilivyokuwa katika migogoro ya Ngorongoro. Na inavyokuwa imefikia hapo, utatuzi wa mgogoro unakuwa wa ngazi ya kitaifa, na unakuwa na taswira ya zimamoto, na wenye gharama kubwa kupita kiasi.

Mgongano kuhusu matakwa ya wafugaji dhidi ya uhifadhi wa wanyamapori NCA umekuwapo muda mrefu; kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 1970. Mwaka 1975 Sheria ya NCA ilirekebishwa kuondoa kilimo hifadhini. Tangu wakati huo hali haijawahi kuwa shwari.

Katika kutafuta suluhu kumefanyika tafiti kadhaa na Tume ya Siwale ya 1984 na kupendekeza mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mipango ya usimamizi (management plans). Ni mambo machache yametekelezwa; na migogoro imeendelea kufukuta na kuchochewa hadi kulipuka mwaka huu. Kama serikali ingechukua hatua mapema ingeepuka sakata hili.

Mwandishi wa makala hii, Theonestina Kaiza-Boshe ni mwana taaluma wa wanyamapori, mazingira na maendeleo endelevu. Anapatikana kwa simu: 0762-889342, barua pepe: [email protected]