Mombasa
Na Dukule Injeni
Eneo ambalo wagombea wawili wakuu miongoni mwa wanne waliopitishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu nchini Kenya utakaofanyika Agosti 9, mwaka huu wanahitaji zaidi kura ni Mlima Kenya.
Wapiga kura wengi wanatoka eneo hili lenye jamii ya Wakikuyu, Waembu na Wameru na katika uchaguzi wa mwaka huu, Mlima Kenya, halina mgombea urais mwenye ushawishi anayeweza kuvaa viatu vya Rais Uhuru Kenyatta.
Hivyo, katika kuvutia wapiga kura kutoka Mlima Kenya, Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, walichagua wagombea wenza kutoka jamii ya Wakikuyu na kufanya mchuano kuwa mkali.
Hata kabla ya wagombea hao kuchagua wagombea wenza, Ruto ndiye alikuwa na nafasi kubwa ya kuzoa kura nyingi kwa kufanya ziara za mara kwa mara Mlima Kenya huku akijadiliana na wanasiasa wa eneo hilo.
Lakini ujio wa Martha Karua, waziri wa zamani wa Katiba na Sheria, akiwa mgombea mwenza wa Odinga, kumebadilisha upepo na kauli za hivi karibuni kutoka kwa wanasiasa wa Mlima Kenya wanaomuunga mkono Ruto kumeibua fukuto ndani ya muungano wa Kenya Kwanza ya Naibu Rais Ruto.
Anayenyoshewa kidole zaidi ni mgombea mwenza wake, Rigathi Gachagua, kutokana na kile kinachodaiwa ni mbabe na dikteta asiyeshaurika, na kwamba tabia pamoja na kauli zake zinaudhoofisha muungano wa Kenya Kwanza.
Ruto na Rigathi wote wanatoka katika Chama cha UDA na waliingia kwenye makubaliano na vyama vidogo kutoka Mlima Kenya, ndoa ambayo imekuwa ya furaha hadi siku za hivi karibuni, huku zikiwa zimebaki wiki chache Kenya kwenda debeni.
UDA ya Ruto imesimamisha wagombea wa nafasi mbalimbali kutoka Mlima Kenya kama ilivyo kwa vyama vidogo ndani ya muungano wa Kenya Kwanza, lakini kumekuwa na mvutano nani atapata wabunge wengi wa Bunge la Taifa, Bunge la Seneti na Bunge la Baraza la Kaunti.
Mvutano huo ulisababisha kiongozi wa Chama Cha Kazi, Moses Kuria, na Mwenyekiti wa Tujibebe Wakenya, William Kabogo, kuamua kususia mikutano ya kisiasa ya UDA huku kiongozi wa The Service Party of Kenya, Mwangi Kiunjuri, na mwenzake wa Farmers Party of Kenya, Irungu Nyakera, wakiomba kuitishwa kikao kujadili mgogoro huo wakiwashutumu UDA kuwadharau viongozi kutoka Mlima Kenya.
Katika moja ya mikutano na wafuasi wake, Kabogo aliwaambia tatizo kubwa ndani ya UDA ni Gachagua, akimtaja mgombea mwenza huyo wa Ruto kuwa ni dikteta na mtu asiyeaminika.
“Nilipinga chaguo la Gachagua kama mgombea mwenza wa Ruto kwa sababu yeye ni dikteta. Mara kadhaa nilimwambia Ruto kwamba atapoteza kura kwa sababu ya Gachagua,” amesema Kabogo ambaye anawania ugavana wa Kiambu kupitia Chama chake cha Tujibebe Wakenya, ambacho kiliingia makubaliano na Kenya Kwanza.
Gachagua aliandaa mkutano wa kisiasa mjini Thika lakini vijana wakaanza kupiga kelele kwa kulitaja jina la Kabogo, jambo ambalo mgombea mwenza huyo wa Ruto akishirikiana na vijana wa UDA alilikemea na kuwataka wanaosababisha vurugu kuandaa mikutano yao na kusukuma ajenda zao.
Anayeungwa mkono kushinda ugavana katika Kaunti ya Kiambu ni Kimani Wamatangi wa Chama cha UDA, kiti ambacho kinamezewa mate na Kabogo na Kuria, ambao Wamatangi anawataja kwamba ni wasababisha vurugu wasio na nia njema ndani ya Kenya Kwanza.
Kama ilivyo kwa Kabogo na Kiunjuri, ndivyo ilivyo kwa kiongozi wa TSP, Mwangi Kiunjuri, aliyemshutumu mgombea mwenza wa Naibu Rais kuchochea mtafaruku miongoni mwa vyama shiriki katika muungano wa Kenya Kwanza.
Kiunjuri alimtaka Gachagua kuwaheshimu, kwani viongozi wa vyama vidogo wana haki sawa kama ilivyo kwa wao UDA kwenye meza ya mazungumzo na kumuonya kuwa safari iliyoonekana kuwa njema kwa Ruto kuelekea Ikulu inaweza ikaingia shubiri.
“Viongozi wa Chama Cha Kazi, Moses Kuria, Chama cha Tujibebe, William Kabogo, Chama cha Amani National Congress, Musalia Mudavadi, Ford Kenya ya Moses Wetang’ula na mimi ni vinara ndani ya Kenya Kwanza,” amesema Kiunjuri.
“Makubaliano yetu ni kuwa tutapata haki sawa ndani ya Kenya Kwanza na hiyo ikimjumuisha Naibu Rais Ruto ambaye ni kiongozi wa UDA, hivyo Gachagua lazima aheshimu haki sawa ya vinara,” amesema.
Vita ya kushinda viti eneo la Mlima Kenya inayodaiwa kuchochewa na Gachaghua inatokana na makubaliano ya Kenya Kwanza inayoainisha nafasi serikalini itagawanwa kulingana na namba ya viti ambavyo kila chama kinashinda.
Hii ndiyo imetajwa kama sababu kubwa ya Gachagua kuhakikisha UDA inapata viti vyote eneo la Mlima Kenya na kuzima ndoto ya vyama vidogo ndani ya Kenya Kwanza kuwamo kwenye serikali endapo Ruto atashinda urais.