Dar es Salaam
Na Mwalimu Samson Sombi
Maendeleo makubwa ya nchi pamoja na mambo mengine hutokana na maono na msimamo wa kiongozi mkuu wa nchi.
Aidha, maendeleo ya nchi huwa na hatua kuu nne ambazo ni mipango, mikakati ya utekelezaji wa mipango, usimamizi na upimaji wa utekelezaji wa mipango hiyo.
Kiongozi ni lazima awe na maono mapana yanayoakisi malengo na dira ya nchi anayoiongoza, awe na ujasiri wa kuthubutu kufanya uamuzi wenye masilahi mapana ya taifa.
Mshahiri na mwandishi wa riwaya wa Marekani, Marge Piercy, aliwahi kusema: “Mwanamke shupavu ni yule anayetaka kufanya yale ambayo wengine wanadhani hayawezekani.”
Rais Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani Machi 19, 2021 amekuwa na msisitizo mkubwa sana juu ya nchi kujitegemea kiuchumi huku akiweka bayana nia yake ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kama hatua pekee ya kukuza uchumi wa nchi.
Aprili, 2021, Rais Samia alihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani na kueleza mikakati na dira ya serikali yake.
Pamoja na mikakati mingine alieleza mwelekeo kwamba utakuwa ni kurudisha imani na kutoa vivutio kwa wawekezaji na wafanyabiashara, ikiwamo kuwezesha uwekezaji kufanyika kwa haraka na kwa mazingira tulivu na salama.
“Nchi yetu imekuwa na changamoto ya kutokuwapo kwa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, ikiwamo kutokuwa na sera zinazotabirika, urasimu unaokwamisha ustawi wa biashara na uwekezaji. Serikali ya Awamu ya Sita inakusudia kufanya marekebisho makubwa,” anasema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Aprili 6, mwaka 2021 Rais Samia alieleza umuhimu wa uwazi na mazingira bora kwa uwekezaji na biashara hapa nchini, huku akiwataka viongozi wahusika kufanya kazi kwa weledi na uzalendo mkubwa.
“Anakuja mwekezaji anawekeza pesa zake, anafungua Insurance Company (Kampuni ya Bima) kubwa, anakuja na wataalamu wake pengine wawili.
“Wataalamu wamefika, miaka mitatu anaomba tena kibali cha kazi. Ahaa! Weka Watanzania! Huu ni mradi wake mwenyewe, anatia Sh 1 akijua itazaa 1.5. Kwa nini umlazimishe aweke mtu ambaye hamtaki?”anahoji Rais.
Rais anawataka wanaosimamia uwekezaji wajenge mazingira bora ya uwekezaji.
“Makampuni yanafungwa ndugu zangu si uongo, yanafungwa na wanaondoka, yakiondoka uchumi wetu unapungua, ajira zinapungua, na hicho ndicho kilio chetu Watanzania, mifuko inabaki mitupu,” anasema Rais.
Akikumbushia hotuba yake bungeni, Rais anasema: “Juzi tu nilitoa kauli ya kodi, wawekezaji wengi wanampigia katibu wangu na wasaidizi wangu – mwambie Rais tunataka kumwona aje atuhakikishie, tunataka kuja Tanzania. Kwa hiyo watu wanataka kuja Tanzania. Naomba tuvute wawekezaji, tupate ajira, fedha izunguke, uchumi ukue.”
Akiwa katika ziara ya kikazi nchini Kenya Mei, 2021, Rais Samia alimweleza Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta kwamba Kenya ni mdau mkubwa wa biashara na uwekezaji Tanzania, na kwamba wanapaswa kuboresha mazingira kwa ufanisi zaidi.
“Kwa mfano wakati wa mazungumzo yetu nimemwarifu Rais Kenyatta kuwa Kenya inashika nafasi ya tano kwa uwekezaji nchini Tanzania kiulimwengu lakini kwa nchi za Afrika Mashariki inashika nafasi ya kwanza,” anaeleza Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Rais Samia anasema kwa lengo la kukuza biashara na uwekezaji “tumekubaliana kuendelea kufanyia kazi changamoto hususan vikwazo visivyo vya kodi, hivyo sasa viondoke na tumekubaliana kuwa tume yetu ya ushirikiano iwe inakaa kutoa suluhu ya vikwazo vinavyojitokeza.”
Moja ya maeneo ambayo ni lango kuu la biashara na uchumi wa nchi ni bandari. Nchi yetu ni miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki zenye bandari nyingi, kubwa na bora ambazo ni mtaji mkubwa sana katika kukuza uchumi na kuongeza pato la taifa.
Akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Biashara (TENC) jijini Dar es Salaam Juni 26, 2021,
Rais Samia Suluhu Hassan anasema wameanza mazungumzo ya kufufua mradi wa Bandari ya Bagamoyo pamoja na ule wa chuma na makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga.
Akizungumzia mradi huo wa Bandari ya Bagamoyo, Balozi wa China hapa nchini, Chen Mingjian, anaipongeza serikali ya Tanzania kwa kuboresha mazingira ya uwekezaji.
“Nimejifunza kuwa Serkali ya Tanzania imefanya marekebisho ya sheria ya uwekezaji na kukuza uwekezaji, mamlaka hizo zinawezesha kupunguzwa kwa gharama za kufanya biashara ikiwamo kupunguza kodi na mchakato wa kufanya kazi,” anasema Mingjian.
Katika hatua za kuimarisha diplomasia ya uchumi, Aprili 22, mwaka huu Tanzania imesaini mikataba saba ya biashara na kampuni za marekani yenye thamani ya Sh trilioni 11.7 inayotarajiwa kuzalisha ajira 301,110 katika sekta ya kilimo, utalii na biashara.
Mbali na mikataba hiyo, Rais Samia alishuhudia utiaji saini wa hati za makubaliano kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya uwekezaji na biashara kati ya kampuni za Marekani na Tanzania.
Katika hatua nyingine, Rais Samia aliyaomba mashirika ya kimataifa kuzisaidia nchi zinazoendelea kutumia nishati ya kijani.
Aliomba hayo alipozungumza na Rais wa Benki ya Dunia, David Malpass, kwamba hilo litasaidia kuepuka uharibifu wa mazingira.
“Mashirika ya kimataifa yanakuja na teknolojia mpya kila siku yanatuambia tutumie nishati ya kijani, yanapaswa kuangalia hali tulizonazo. Afrika tunaweza katika gesi, umemejua na upepo, lakini tunahitaji msaada kukusanya nishati kutoka vyanzo hivyo,” anasema Rais Samia.
Rais Samia ameendelea kuimarisha uhusiano mwema na nchi wanachama wa Afrika Mashariki na kukaribisha wawekezaji wa nchi hizo kuja kuwekeza Tanzania kwa masilahi mapana ya Tanzania na nchi hizo.
Mei 10, mwaka huu Rais Samia alifanya ziara ya siku mbili ya kitaifa nchini Uganda, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipoingia madarakani.
Katika ziara hiyo Tanzania na Uganda zimesaini mikataba miwili ya makubaliano kuhusu ulinzi wa nishati, huku Rais Samia akiwakaribisha wawekezaji kutoka Uganda kuwekeza nchini.
Rais Samia alisema wamefanya majadiliano na mwenyeji wake Rais Museveni katika masuala mbalimbali ikiwamo nishati, biashara, usafiri, maendeleo ya miundombinu, afya, utulivu wa kisiasa na usalama, lengo likiwa ni kuimarisha uchumi wa nchi hizo.
Rais amewaalika pia wafanyabiashara wa Oman kuja kuwekeza nchini Tanzania huku akiwahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji na uwepo wa nguvukazi ya kutosha.
Katika ziara yake ya siku tatu nchini Oman Juni 12, mwaka huu Rais Samia alisema hayo wakati akishiriki kongamano la wafanyabiashara nchini Oman na kwamba endapo Oman itatumia fursa ya kuwekeza nchini itanufaika na soko kubwa ambalo Tanzania inaweza kulifikia.
“Sisi ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pia ni wanachama wa SADC ambao kwa pamoja tunatengeneza idadi ya watu karibu milioni 500, ambalo ni soko kubwa.
“Pia wanachama wa soko huru la Afrika (ACFTA). Hili linaongeza idadi ya watu na kufanya soko la watu kuwa bilioni 1.3,” anasema Rais Samia.
Rais Samia alieleza kuhusu fursa za uwekezaji Tanzania ikiwamo kilimo, mifugo, uvuvi, madini, utalii, uzalishaji, teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) na maendeleo ya miundombinu.
Kwa upande wake Waziri wa Biashara, Viwanda na Uwekezaji wa Oman, Qais bin Mohammed Al-Yousef, anasema wako tayari kujadili ni kwa namna gani wanaweza kushirikiana na kuendeleza fursa hizo ambazo Tanzania imezitaja.
“Pia tuko tayari kuangalia namna tunavyoweza kuimarisha biashara, uwekezaj na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya watu wa nchi zote mbili, hususan katika maeneo ya kilimo, uvuvi, viwanda, madini na utalii kama yalivyotajwa na Rais Samia,” anasema Al-Yousef.
Ofisa Uvuvi Mwandamizi Mkoa wa Geita, Tito Mlelwa, anasema Rais Samia amefanikiwa kujenga diplomasia ya kiuchumi na kuvuta wawekezaji wengi kuja kuwekeza Tanzania kwa kipindi kifupi.
“Ziara za Rais Samia kimataifa zinajenga diplomasia ya kiuchumi na kuwahakikishia wawekezaji hali ya usalama na amani iliyopo Tanzania. Wawekezaji wanahitaji mazingira mazuri, usalama wao pamoja na fedha zao,” anabainisha Mlelwa.
Kwa upande wake mfuatiliaji wa masuala ya siasa na kijamii, Hashini Yahya wa Masika, Manispaa ya Morogoro, anasema vijana wanapaswa kuchangamkia fursa zinazopatikana katika uwekezaji na kumpongeza Rais Samia kwa jitihada za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Na Mwalimu Samson Sombi.
0755-985966