Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu, ameanza kutekeleza kwa vitendo maagizo ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuikaribisha sekta binafsi kushiriki kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi ili kujenga Tanzania mpya.

Wiki iliyopita Mchechu alizuru Makao Makuu ya Shirika la Nyumba Zanzibar (NHZ) yaliyopo Mji Mkongwe. Lengo la ziara yake lilikuwa kuimarisha ushirikiano wa mashirika hayo mawili.

Mchechu anasema miongoni mwa vipaumbele vya NHC kuanzia Julai, 2022 ni kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha na kuendeleza sekta ya nyumba nchini.

Anasema NHC inakusudia kupata wawekezaji muhimu 200 wenye mitaji isiyopungua Sh bilioni 2 kila mmoja.

Vipaumbele vingine anasema ni kuangalia rasilimali za shirika ili zitumike kujiendesha kibiashara na kuongeza idadi ya nyumba kupitia sera ya ubia.

Rasilimali nyumba zitatumika vema kupangisha na kuuza ili kuongeza kipato na kuongeza kasi ya ujenzi wa nyumba mpya ili kuendelea kutimiza lengo la NHC la kuwa kiongozi katika usimamizi na endelezaji wa miliki nchini.

Mkurugenzi Mkuu huyo anasema ili kufikia malengo hayo na kutekeleza vipaumbele vilivyopo sasa kwa ufanisi, NHC itafanya mabadiliko ya watendaji wake kwa kupanga watu sahihi katika nafasi sahihi ili kuliwezesha shirika kufikia matarajio ya Watanzania, serikali na wadau wa sekta ya nyumba.

“Tutafanya mabadiliko ya ndani kwa kupanga watu sahihi kwenye nafasi sahihi ili shirika lifanye vizuri katika nyanja mbalimbali na kufanya mabadiliko ili mambo yaendelee kwa kasi, tuweze kukimbia kwa kasi inayotakiwa na Serikali ya Awamu ya Sita,” anasema Mchechu ambaye yuko kwenye mageuzi makubwa ya kuliboresha shirika.

Rasilimali watu ni nyenzo muhimu ili kubadili au kuleta matokeo chanya ndani ya shirika, ni kwa sababu hiyo anasisitiza kuwa inaundwa timu yenye weledi itakayokidhi malengo ya shirika kadiri ya maelekezo yaliyotolewa na serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Anasema ili kuungwa mkono na wadau mbalimbali muhimu, shirika limekuwa likikutana na wadau wa sekta binafsi kuwaeleza mpango mkakati wa shirika na mipango mingine ya kuendeleza sekta ya nyumba.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa ZHC, Mwanaisha Ali Said, anaishukuru NHC kwa kutoa mafunzo mbalimbali kwa watendaji wa ZHC na kuahidi kutembelea tena NHC akiwa na watendaji wake ili kupata mafunzo kutoka kwa wakuu wa vitengo na kujua jinsi ya kuendesha shirika.

“Tunafurahi umerudi tena NHC kwani utatusaidia na tutakuja kuwatembelea huko Bara ili kuweza kupeana ushauri wa namna ya kwenda mbele na kujifunza kupitia mambo makubwa ambayo NHC imeyafanya, hasa jambo letu tunalofanya sasa la kuendeleza eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar ili kukuza utalii,” anasema Mwanaisha.

Kwa upande wake, Mchechu, ameahidi kuwa NHC itaendelea kushirikiana na ZHC kuwaletea wananchi maendeleo na kusaidia kuleta wawekezaji.

Sanjari na hilo, ameshauri ZHC kujenga nyumba za gharama nafuu na kati na kuruhusu wasiokuwa raia kumiliki nyumba ili kuongeza mtaji nchini, pia kuongeza masoko.

“Juhudi za Rais za kufungua nchi mwelekeo mkubwa utakuwa kuhusisha sekta binafsi, hivyo nawashauri Shirika la Nyumba la Zanzibar kukaribisha wawekezaji ili kuendeleza shirika na kuongeza kipato,” ameshauri Mchechu.

Katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Samia, NHC imekusudia kujenga nyumba 5,000 za gharama nafuu na kati.

Mchechu anasema ili kusaidia suala la makazi, hasa baada ya serikali kuhamia Dodoma, shirika litaendelea kujenga nyumba katika Jiji la Dodoma na hivi sasa litauza nyumba 50 eneo la Medeli  ili kupata fedha za kujenga nyumba nyingine 100 katika eneo hilo.

Awali Mchechu alipata fursa ya kutembelea baadhi ya nyumba kongwe za shirika hilo zinazokarabatiwa katika eneo la Mnadani, Mjini Unguja ikiwa ni kazi ya kwanza ya ujenzi kufanywa na shirika hilo tangu lianzishwe mwaka 2014 kwa Sheria ya Baraza la Wawakilishi Na. 6.

Mchechu amefanya ziara hiyo ya kikazi baada ya kuhudhuria uzinduzi wa Taasisi ya Mwanamke (Mwanamke Initiatives Foundation – MIF) uliofanywa juzi na Rais Samia Suluhu Hassan.

Sehemu ya makala hii ya mtangazaji kwa mara ya kwanza ilitoka kwenye Blog ya Tanzania Panorama.