Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 imesomwa wiki iliyopita bungeni jijini Dodoma na kwa sasa inajadiliwa kabla ya kupitishwa tayari kwa utekelezaji wake kuanzia Julai Mosi mwaka huu.
Kwa kawaida, pamoja na ukweli kwamba kabla ya kusomwa kwake tayari wizara zote zinakuwa zimekwisha kusoma bajeti zao, bado Bajeti Kuu husubiriwa kwa hamu na wananchi wengi.
Hii ni kwa sababu kusomwa kwake, kisha kupitishwa na Bunge, ndio muhuri wa moto katika mipango na mikakati ya maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja wa Tanzania na taifa zima.
Swali linaloumiza vichwa vya watu wengi kila baada ya kusomwa bajeti ni, je, utekelezwaji wake utafikiwa kwa asilimia ngapi? Je, bajeti iliyopita imetekelezwa kwa kiasi gani?
Ni bahati mbaya kwamba hakuna mtu anayejishughulisha na mambo yaliyotangazwa mwaka mmoja uliopita. Wengi hutazama mbele na kusubiri ‘mazuri’ yajayo, wakijitahidi kusahau yaliyopita.
Lakini kwa namna ambavyo bajeti ya mwaka ujao wa fedha ilivyochambuliwa, ni wazi kuwa wasomi kadhaa hawakufurahishwi na wingi wa vipaumbele vilivyowekwa.
Wingi huu wa vipaumbele unasababisha watu kushindwa kufuatilia kikamilifu utekelezaji wake na ndiyo maana wasomi na wataalamu kadhaa wanatamani kuwe na vipaumbele vichache tu kwa mwaka.
Mathalani, kama mwaka huu tumeamua kumaliza kabisa miradi ya kimkakati, basi wananchi wafahamu hivyo, na kwamba ndani ya mwaka mmoja mradi fulani utakuwa umekamilika ili mwaka mwingine juhudi zielekezwe sehemu nyingine.
Lakini pia tunafahamu kuwa ili Bajeti Kuu ya Serikali 2022/23 itekelezeke kikamilifu, kila Mtanzania sehemu alipo anapaswa kutoa mchango wake na kusaidia utekelezaji.
Maana yake anayetakiwa kulipa kodi, alipe mara moja; anayetakiwa kutoa huduma aitoe bila kulazimishwa, anayetakiwa kusimamia eneo fulani afanye hivyo.
Haya yote yanawezekana iwapo tu kutakuwa na watu wenye moyo wa kizalendo na wenye uchu wa kuiona Tanzania ikipiga hatua kubwa kiuchumi na kushindana na mataifa mengine Afrika.
Tunaipongeza serikali kwa walau kuwakumbuka watu wenye maisha duni kwa kutoa elimu bure hadi kidato cha sita; kuongeza bajeti ya TASAF na kutenga fedha kwa ajili ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu.