DAR ES SALAAM 

Na Jackson Kulinga

Siku moja kabla ya kufanyika mkutano wa 13 wa Baraza la Biashara la Taifa (TNBC), Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Paul Makanza, alizungumzia kuridhishwa kwake na umakini wa serikali katika kutekeleza maazimio ya TBNC.  

Mkutano huo ulifanyika Juni 8, mwaka huu jijini Dodoma na Makanza anasema sasa serikali imeungana na sekta binafsi katika kujenga uchumi wa taifa.

Kilichomfurahisha Makanza ni mrejesho wa serikali katika uamuzi uliofanywa na Mkutano Mkuu wa 12 wa Baraza uliofanyika Juni 26, 2021, wa kwanza kufanyika chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Hii inatupa imani kwamba serikali imedhamiria kweli kuondoa vikwazo vyote vinavyoelezwa. Ipo dhamira ya dhati ya kujenga uchumi wa taifa letu,” anasema.

Si kila Mtanzania anaelewa uzito wa kauli hii, lakini ukweli ni kwamba katika ufunguzi wa mkutano wa 12, Mwenyekiti wa TPSF, Angelina Ngalula, aliipongeza serikali kwa kazi nzuri zilizotekelezwa kukuza uchumi na kuinua maendeleo ya taifa, hasa juhudi binafsi za Rais Samia. 

Angelina pia ni mjumbe wa TNBC na Mwenyekiti wa Kongani ya Usafirishaji na siku hiyo alisema:

“Tunaipongeza serikali kwa kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji na ushirikishwaji wa sekta binafsi ambayo imekutana na kufanya majadiliano na Rais, Waziri Muu, mawaziri, wabunge na watendaji wa Serikali.

“Pamoja na mikakati ya kuendeleza sekta binafsi, majadiliano yetu yalielekezwa katika kukemea na kudhibiti rushwa katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), hasa eneo la kukadiria kodi na kufunguliwa akaunti za benki za wafanyabiashara zilizofungiwa na TRA, jambo ambalo limerudisha imani.”

Taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa 12 inatoa ushahidi wa kutosha kwa nini sekta binafsi sasa ina imani na kauli, ahadi na vitendo vya serikali. 

Kwa mfano, iliazimiwa kwamba mfumo wa majadiliano wa TNBC uwe sawa na wa majadiliano wa masuala ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar, ili maazimio ya sekta binafsi na ya umma yatokane na maridhiano ya pande zote mbili. 

Uboreshaji wa mfumo umefanywa na kugusa ngazi ya taifa, wizara, mikoa na wilaya. Sasa TNBC inaridhika kuhusu mfumo wa majadiliano (ulioibuka), ufanisi wa utekelezaji wa maazimio na mrejesho kati ya sekta ya umma na binafsi utaimarika.

Iliazimiwa pia kuwa mfumo wa TNBC uwe jumuishi kwa kuongeza wadau zaidi; suala ambalo limetekelezwa kwa kuongeza idadi ya washiriki, hasa wafanyabiashara na wawekezaji. 

Taarifa ya utekelezaji wake inasema: “Lengo ni kuhakikisha mabaraza ya biashara mikoani na wilayani yanafanya vikao kila robo ya mwaka. Wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na watumishi wengine wa umma wakutane mara kwa mara na sekta binafsi katika maeneo yao.”

Kadhalika iliazimiwa kwamba Ofisi ya Rais, Tamisemi, isimamie mikutano ya mikoa na wilaya ambapo Tamisemi kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji ya TNBC imetekeleza.

Mikutano imefanyika Tabora, Songwe, Simiyu, Shinyanga, Ruvuma, Pwani, Njombe, Mwanza, Mtwara, Morogoro, Mbeya, Mara, Manyara, Kigoma, Geita na Dar es Salaam.

“Mikoa ya Singida, Simiyu, Ruvuma, Rukwa, Njombe, Manyara na Iringa imepatiwa mafunzo kuhusu namna bora ya uendeshaji wa majadiliano yenye tija na ufanisi pamoja na kutoa mrejesho kuhusu utekelezaji wa maazimio,” inasomeka taarifa ya mrejesho.

Mengine yaliyoazimiwa na kutekelezwa ni kuwapo kwa mapitio ya sera, sheria, kanuni na taratibu ili kuainisha upungufu; ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu imeelekeza wizara zote za kisekta kufanya mapitio, kuonyesha upungufu na kupendekeza uboreshaji wa sera na sheria mbalimbali.  

Mambo yaliyofanyiwa mapitio na uboreshaji ni Sheria ya Fedha ya 2021/22, Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya 1996, Sera ya Biashara ya 2003, Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya 2003, Sheria ya Uvuvi ya 2003 na Mpango Mkakati wa miaka 15 wa kuendeleza uvuvi kuanzia mwaka 2021/2022.

Iliazimiwa kwamba taasisi zote za umma zitekeleze majukumu na kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara na wawekezaji kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.  Ofisi ya Waziri Mkuu imezielekeza taasisi zote kufanya hivyo. 

Ofisi hiyo pia inafanya mikutano na taasisi zote za urekebu (regulatory entities) kuzielekeza namna bora ya kufanya kazi kwa weledi bila kuathiri biashara na uwekezaji wa sekta binafsi, ikihimizwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika taratibu na malipo.

Iliazimiwa yakamilishwe majadiliano kuhusu mikataba ya kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na unganishi ya Mchuchuma, Liganga na Bandari ya Bagamoyo. Timu ya kitaifa ya majadiliano ya serikali tayari imeundwa na inajadiliana na wawekezaji.  

Iliazimiwa kuwa Wizara ya Fedha na Mipango idhibiti ongezeko la kodi/tozo mpya. Wizara imetoa maelekezo kwa wizara nyingine na taasisi zote za umma, ikizitaka kutofanya marekebisho ya tozo bila kushauriana na wizara husika.

Iliazimiwa kuboreshwa mazingira ya biashara baina ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kwa kuondoa vikwazo au sheria, kanuni na taratibu zisizokuwa na tija katika kudumisha biashara na Muungano.  Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeboresha mazingira ya biashara kati ya Bara na Zanzibar.

Iliazimiwa Wizara ya Malilasili na Utalii, Wizara ya Mifugo na sekta binafsi wajadiliane na kutoa mapendekezo kuhusu sheria, kanuni na taratibu ili kuondoa changamoto za mwingiliano kati ya maeneo tengefu ya utalii na ufugaji.   

Wataalamu kutoka wizara hizo mbili walikutana Desemba 21, 2021 kwa ajili ya kupata uelewa na kutoa mapendekezo ya kutatua changamoto za kisheria, kanuni na taratibu zilizopo kuhusu maeneo yaliyohifadhiwa au tengefu kwa ajili ya utalii na ufugaji.

Iliazimiwa kwamba ijengwe na kuimarisha miundombinu wezeshi inayounganisha Tanzania na majirani wake.  Wizara ya Ujenzi na Uchukuazi inaratibu tafiti kuhusu ujenzi wa miundombinu wezeshi ya kuunganisha Tanzania na Kongo DRC.  Miundombinu wezeshi itachochea biashara kati ya nchi mbili hizi.

Iliazimiwa ifanywe tathmini  au mapitio kuhusu mifumo ya pre-shipment inspection (PSI) na destination inspection (DI)  na kutoa taarifa yenye ushauri mahususi kwa serikali ili iweze kufanya uamuzi sahihi kuhusu suala husika.  

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na TNBC wamefanya tathmini ya mifumo ya ukaguzi wa mizigo, hususan magari, kabla na baada ya kusafirishwa. Tathmini hiyo ilithibitishwa na mkutano wa wadau Novemba 19, 2021.

 Iliazimiwa kwamba sekta binafsi iunde mfumo wa kujitathmini na kufanya biashara na uwekezaji kwa weledi, uaminifu na nidhamu kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na taratibu za nchi sawa na serikali inavyowajibika.  

Taarifa ya mrejesho inaonyesha kuwa sekta binafsi haijatekeleza azimio hilo. Doa hilo kwa sekta binafsi linathibitisha busara ndani ya methali kwamba ‘nyani haoni kundule’.  

Kwa mifano michache hii, kuna sababu ya mtu kujiridhisha kwamba Mtanzania anayefuatilia jitihada za TNBC katika kuimarisha uchumi wa taifa, ataelewa pia msingi wa kauli nzito ya Makanza kabla ya mkutano wa 13 wa TNBC ambao umemalizika jana jijini Dodoma.   

Mkutano huu pia umetoa maazimio mengine ya kuyasukuma mbele maendeleo ya taifa letu.

TNBC ilianzishwa Septemba 2001. Ni taasisi ya majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta ya biashara.