Ndugu Mhariri, tunaomba nafasi japo ndogo katika gazeti lako tukufu ili Rais Samia Suluhu Hassan na watendaji wake wafahamu yanayotusibu.
Malalamiko yetu ni ya kukaa gerezani kwa muda mrefu katika kesi za mauaji zilizopo Mahakama Kuu upande wa Kisutu Extended bila kusikilizwa.
Zifuatazo ni baadhi ya kesi za mauaji zilizopo Mahakama Kuu upande wa Kisutu Extended ambazo zimechukua muda mrefu bila kusikilizwa tangu mwaka 2008.
- 1. Adam Charles Mkude – PI 14/2008
- 2. Jumanne Adiad Omary – PI 24/2010 iliyosajiliwa Kisutu Extended kama CCS No 7/2017
- 3. Hassan Bulanga – PI 06/2010 iliyosajiliwa Kisutu Extended kama CCS No. 31/2014
- 4. Mark Libila Kwalanda – PI 18/2013 iliyosajiliwa Kisutu Extended kama CCS 78/2017
- 5. Frank Pius Rwanda – PI 34/2013 iliyosajiliwa Kisutu Extended kama CCS 37/2019
- 6. Leonard Mathias – PI 19/2013 iliyosajiliwa Kisutu Extended kama 52/2019
- 7. Mashaka Adam – P1 19/2013 iliyosajiliwa Kisutu Extended
- 8. Laurent Hendrick – PI 14/2014 (Kisutu Extended CCS 68/2020)
- 9. Idd Mussa na wenzake wawili – PI 24/2015 (Kisutu Extended CCS 93/2020)
- 10. Nickson Gervas – PI 25/2015 (Kisutu Extended CCS 32/2019)
- 11. Nassoro Shaban – PI 30/2016 (Kisutu Extended CCS 103/20190)
- 12. Issa Kassim Swadaka PI 29/2016 (Kisutu Extended CCS 69/2019)
Mheshimiwa Rais, hiyo hapo ni mifano michache ya kesi zilizopo katika mahakama hiyo ya Kisutu Extended.
Uwepo wetu huku gerezani kwa muda mrefu tumekuwa tukifuatilia mara nyingi katika vyombo vya habari tukisikia ukiziagiza mamlaka husika kuangalia au kufuatilia mashauri yaliyokaa muda mrefu mahakamani yamalizwe au kama hayana mashiko yaondolewe mahakamani, lakini hali imekuwa ni tofauti kwa upande wa Mahakama ya Kisutu Extended ambayo imekuwa kama kichaka cha kuficha watu magerezani kwa muda mrefu.
Mhe. Rais Samia, tumekuwa tukimwandikia barua Msajii wa Mahakama Kuu, mafaili ya kesi zote za mauaji yapo kwake na yeye ndiye mwenye mamlaka, lakini akijibu katika barua tofauti tofauti kwamba hakuna fungu la kuendesha kesi.
Jambo la kushangaza Mahakama Kuu upande wa Posta kesi zinakwenda, mahabusu wanamaliza mashauri yao kwa wakati, hivyo tunabaki kujiuliza, hawa wengine fedha za kuendesha kesi zinapatikana wapi? Mbona kesi zinakwenda?
Sisi wa huku Kisutu Extended mbona mambo hayaendi? Kwani sisi ni Watanzania wa wapi tofauti na wenzetu? Haki iko wapi? Usawa uko wapi?
Mhe. Rais, tangu umeanza kuziagiza mamlaka kumaliza mashauri kwa wakati, ni kwamba mashauri mengi yamefutwa hata katika mahakama za wilaya.
Mashauri mengine hata mwaka mmoja hayajachukua, tumeona yameondolewa mahakamani. Hivyo kesi nyingi zilizoondolewa ni mpya, lakini nyingi zilizobaki ni za zamani na ndizo nyingi zilizopo katika mahakama tunayoilalamikia, Kisutu Extended.
Mhe. Rais, ni kwamba mahabusu wote wa kesi za zamani bado tupo gerezani na hadi sasa bado hatujui hatima yetu.
Mhe. Rais, lengo kuu la barua hii ya wazi kwako ni kukuomba ututatulie changamoto hii inayotusumbua kwa muda mrefu.
Tuna imani kubwa sana na wewe. Vilevile tuna imani utakapoiona barua hii utatusaidia ili nasi tukaungane na familia zetu ambazo tumetengana nazo kwa muda mrefu sana.
Tunakutakia afya njema, tunakutakia ujenzi mwema wa taifa letu pendwa la Tanzania; tunakuombea sana Mwenyezi Mungu akuongoze na kukulinda.
Wako watiifu,
Mahabusu wa kesi za mauaji Gereza la Mahabusu Segerea.