Septemba 1961, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alitoa ilani iliyokuja kujulikana kama Ilani ya Arusha kuhusu uhifadhi.
Alisema: “Kudumisha uhai wa wanyamapori wetu ni suala linalotuhusu sana sisi sote katika Afrika. Viumbe hawa wa porini pamoja na mapori wanamoishi siyo tu kwamba ni muhimu kama mambo ya kustaajabisha na kuvutia, bali pia kwamba ni sehemu muhimu ya maliasili yetu na ustawi wa maisha yetu katika siku za baadaye.
“Kwa kukubali dhamana ya kuhifadhi wanyama wetu tunatoa tamko la dhati kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa wajukuu na watoto wetu wataweza kufaidi utajiri na thamani ya urithi huu.
“Kuhifadhi wanyamapori na mapori waishimo kunahitaji utaalamu maalumu, watumishi waliofunzwa pamoja na fedha. Tunatazamia kupata ushirikiano kutoka kwa mataifa mengine katika kutekeleza jukumu hili muhimu. Kufanikiwa au kushindwa kwa jukumu hilo kutaathiri siyo tu Bara la Afrika pekee, bali ulimwengu mzima.”
Maneno haya ya Mwalimu ndiyo mwongozo wa uhifadhi Tanzania na katika mataifa mengine ya Afrika. Mababu zetu licha ya kukosa elimu ya darasani, walikuwa wahifadhi wazuri kuliko madaktari na maprofesa wa leo. Waliposema msitu fulani hauruhusiwi kukatwa miti, walifanya hivyo ili kulinda misitu. Si kweli kwamba misitu hiyo ilikuwa na nyoka au mizimu, bali waliwajengea hofu watu ili kuilinda hiyo misitu. Elimu ya leo haijasaidia kulinda mazingira yetu.
Kwa miaka mingi nimekuwa mmoja wa washiriki wakuu wa masuala ya uhifadhi. Naupenda uhifadhi. Wale wanaosoma Biblia Takatifu watakubaliana nami kuwa binadamu ni kiumbe wa mwisho kabisa kuumbwa baada ya viumbe wengine kama wanyama na ndege. Mungu aliwaumba wanadamu ili wautawale ulimwengu na vilivyomo – si kuutawala ulimwengu na kuviua vilivyomo.
Kwa namna ya pekee leo najadili kidogo kuhusu Loliondo. Kuna upotoshaji mkubwa mno kuhusu kazi inayoendeshwa na serikali katika Pori Tengefu la Loliondo na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Baadhi ya watu wameamua kupotosha kwa makusudi kabisa ili kuleta taharuki na vurugu. Tujuavyo, Loliondo hawahamishwi watu, bali kunawekwa vigingi ili kulitambua eneo linalopaswa kuendelea kuwa chini ya uangalizi wa serikali kwa kuwashirikisha wananchi. Hapo chini nimeeleza sababu za kuilinda Loliondo. Ngorongoro kunaletwa mabadiliko ya hiari ya watu na mifugo kuhamishwa ili hifadhi isilemewe maana tayari hali ya uhifadhi ni mbaya. Kwenye mipango yote hii hakuna mahali binadamu anaondolewa kwa mabavu.
Pori Tengefu la Loliondo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4,000 lilianzishwa kisheria mwaka 1959 na serikali ya kikoloni ya Waingereza kama Pori la Akiba chini ya agizo la serikali ya wakati huo lililojulikana kama Agizo la Hifadhi ya Wanyamapori, kifungu cha 302 (The Fauna Conservation Ordinance, section 302) kilichowekwa na mamlaka ya kikoloni ya kutenga maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori.
Hadhi ya kisheria baadaye ilibadilishwa na kuwa Pori Tengefu mwaka 1974 kwa Sheria ya Wanyamapori Na. 12 ya mwaka huo ili kuruhusu shughuli za uwindaji; hadhi iliyolifanya Pori Tengefu la Loliondo kuwa na hadhi ya kuwa na msimu wa uwindaji wa wanyamapori katika eneo hilo.
Aidha, Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 1974 iliruhusu shughuli za kinadamu kufanyika sambamba na shughuli za uhifadhi wanyamapori ndani ya Mapori Tengefu (Game Controlled Areas). Eneo kubwa la Pori Tengefu la Loliondo ni kiungo muhimu katika ikolojia ya Serengeti ambayo upande wa kaskazini inaunganisha Pori la Akiba la Maasai-Mara nchini Kenya na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa upande wa kusini.
Kipekee eneo la Pori Tengefu la Loliondo ndiko vyanzo vingi vya maji kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ziwa Natron vinakoanzia, hivyo kufanya makundi makubwa ya wanyamapori kupenda kuishi maeneo haya. Asilimia takriban 50 ya maji yanayoingia Serengeti hutoka Loliondo. Pori Tengefu la Loliondo kwa muda mrefu limekuwa likitumika kama kitalu cha uwindaji wa kitalii kwa ajili ya kuliingizia taifa fedha za kigeni.
Hali ya Pori Tengefu la Loliondo kwa sasa kutokana na Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 1974 kuruhusu shughuli za binadamu na shughuli za uhifadhi kufanyika, kuna mabadiliko makubwa kutokana na shughuli za kimaendeleo, shughuli za binadamu na ongezeko la idadi ya watu na mifugo.
Hivi sasa Pori Tengefu la Loliondo lina maeneo ya aina mbalimbali kama ifuatavyo:
*Mji wa Wasso na Loliondo ambako hivi sasa miji hii inakua kwa kasi kubwa.
*Misitu ya Hifadhi (Loliondo I, II na Sariani).
*Maeneo mengi kutengwa kwa ajili ya shughuli za kilimo; mfano kata za Digodigo, Sale, Oloirien na Samunge.
*Mashamba makubwa binafsi. Mfano Thomson Safari wana shamba lenye ukubwa wa kilometa za mraba 126.17 (hekta 12,617).
*Eneo lote la Pori Tengefu la Loliondo (kilometa za mraba 4,000) ni kitalu (hunting block).
*Ongezeko kubwa la mifugo na hivyo kuhitaji maeneo makubwa ya malisho.
*Maeneo ya uwekezaji- mfano machimbo ya madini eneo la Naan na Mgongo.
*Ongezeko la watu kutoka NCAA ambako wamehamishiwa eneo la Jema, Tarafa ya Sale, ingawa wengi wao wamerejea tena kuishi NCAA.
Kutokana na mwingiliano wa matumizi haya mbalimbali, kumekuwapo migogoro mingi ya matumizi ya rasilimali za maliasili, hasa ardhi na wanyamapori ambayo imeendelea kukua siku hadi siku.
Juhudi mbalimbali zimefanyika kutatua migogoro hiyo, lakini juhudi hizo hazikuleta mafanikio. Kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii, serikali ilitangaza kauli ya kurejesha eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 2,500 (sawa na 62%) kwa wananchi, na eneo linalobaki la ukubwa wa kilometa za mraba 1,500 (38%) kuwa Pori Tengefu la Loliondo ili kuendana na Sheria Na. 5 ya Wanyamapori ya mwaka 2009 ambayo hairuhusu shughuli za binadamu ndani ya Mapori Tengefu. Hapa isisitizwe kuwa serikali imetoa eneo la kilometa 2,500 kwa wananchi, na si kwamba wananchi wananyang’anywa eneo lao.
Eneo la kilometa za mraba 1,500 lililopendekezwa kubaki kuwa Pori Tengefu kwa mujibu wa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi wa mwaka 2010, na pia tamko la aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii (Balozi Hamis Kaghasheki) Machi 2013, eneo linalopendekezwa kuwa Pori Tengefu limo ndani ya kata za Ololosokwan, Soitsambu, Oloipiri, Loirien Magaiduru, Losoito Maaloni, Arash na Kata ya Malambo Kijiji cha Piyaya zinazopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ilipandisha hadhi tena Mapori Tengefu nchini kuwa na hadhi sawa na Mapori ya Akiba. Kwa mantiki hiyo na kwa mujibu wa sheria hiyo, serikali imehitajika kupitia upya Mapori Tengefu yote nchi nzima kwa lengo la kubaini Mapori Tengefu yenye sifa ya kuendelea kuwa maeneo ya Hifadhi (GCA), na yale ambayo hayakuwa na sifa, serikali ikapanga kuyafuta.
Kwa kuwa eneo lote la Tarafa ya Loliondo na Sale lilikuwa ni ardhi ya hifadhi na wakati huo huo likitumiwa na wananchi kwa shughuli za maisha yao, serikali ikaona ni vema kupunguza maeneo ya Pori Tengefu ili eneo lililobaki liwe chini ya umiliki wa wananchi na litumiwe kwa shughuli zao za kila siku na kujiletea maendeleo.
Hivyo basi, katika kupitia upya eneo hilo la Pori Tengefu la Loliondo, ikaonekana kuwa eneo linalofaa kuendelea kubaki kuwa Pori Tengefu (GCA) ni eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 1,500 kwa mujibu wa rasimu ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi ya mwaka 2010.
Eneo hili ni muhimu kwa ikolojia ya Serengeti ikiwa na vyanzo sita vya maji, mapito na mazalia ya wanyamapori. Pia eneo hilo lina umuhimu mkubwa sana kwani linategemewa na wakazi wa kata saba kama maeneo ya makazi, malisho ya mifugo na upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli zao za kila siku. Baadhi ya vyanzo vya maji vilivyopo katika eneo hilo ni kama ifutavyo:
*Mto Pololeti – vijiji vya Oloipiri, Soitsambu, Maaloni, Arash, Ololosokwan.
*Mto Irmolelian – vijiji vya Piyaya, Arash, Malambo, Maaloni.
*Mto Orgumi – Losoito, Arash, Oloipiri, Magaiduru na Piyaya.
*Vyanzo vya maji vya Lima One – vijiji vya Soitsambu, Oloipiri, Oloirien, Ololosokwan.
*Chanzo cha Maji Mlima Loilale – vijiji vya Ololosokwan, Kirtalo, Soitsambu.
*Chanzo cha Maji Mlima Loili – vijiji vya Ololosokwan na Soitsambu.
Kwa maelezo haya mafupi, umuhimu wa Loliondo kwa uhifadhi na usalama wa Ngorongoro, Serengeti na Maasai-Mara si jambo la mjadala. Wala hili si suala la kusababisha mapigano au maumivu kwa wananchi na kwa serikali.
Tunao wajibu wa kukwepa aina zote za uchochezi kwenye suala hili jema linalolenga kulinda rasilimali hii kwa manufaa na masilahi mapana ya umma.
Majirani zetu ambao wana mkono mkubwa kwenye sakata hawana haki ya kuingilia mambo yetu ya ndani kwa sababu jambo linalofanywa lina nia njema ya kulinda uhifadhi. Watanzania hatujawahi kufeli kwenye mazungumzo na kutenda mambo yetu kwa amani na utulivu. NGOs zitambue kuwa kazi yake ni kujenga, si kubomoa. Tanzania ni ya Watanzania wote. Rasilimali za nchi sharti zilindwe kwa shauku na wivu mkubwa.