Na Alex Kazenga
Dar es Salaam
Wadau wa tasnia ya habari wanaiomba serikali kuitazama upya Sheria ya Habari huku wakipendekeza kuwapo kwa chombo kitakachosimamia tasnia hiyo.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amebainisha hayo hivi karibuni katika mkutano maalumu na waandishi wa habari uliokuwa na lengo la kujadili mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Habari nchini.
“Kuna mambo mengi ya kutazamwa upya, mojawapo ni kukiondoa kifungu kinachompa madaraka Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) kuratibu matangazo ya serikali,” anasema Balile.
Aidha, amebainisha kwamba sheria iliyopo sasa inafifisha uhuru wa habari kutokana na kuwapo kifungu kinachotoa utaratibu wa utoaji wa leseni kwa magazeti.
Anautaja ufutaji wa leseni za magazeti ya Mawio, Mwanahalisi, Mseto na Tanzania Daima uliowahi kufanyika kama kikwazo cha uhuru wa vyombo vya habari nchini.
“Mazingira yakiwa mazuri, sheria zikiwa nzuri, matangazo yakatolewa kwa bei stahiki, kinyume cha ilivyo sasa ambapo wanashusha bei watakavyo, mapato ya vyombo vya habari yataongezeka,” anasema Balile.
Anakitaja kifungu cha 5 cha Sheria ya Habari, kipengele cha kwanza kwamba kinaminya ufanisi wa kutoa na kusambaza matangazo nchi nzima, huku pia kikitengeneza mazingira ya rushwa kwa wahusika.
Balile anasema kutokana na mwaka jana Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza vyombo vya habari kupewa matangazo kwa njia ya ushindani na si kwa njia ya upendeleo, anaamini waziri mwenye dhamana atatimiza ahadi hiyo.
“Tunamshuku waziri mwenye dhama ya masuala ya habari; Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye, amesema mara zote kwamba tutaendelea kuzungumza na tutaelewana ni vifungu vipi vifike hatua ipi, kwa ajili ya kuwa na sheria iliyo bora, inayoruhusu uhuru wa vyombo vya habari,” anasema Balile.
Kwa upande mwingine, katika mkutano huo suala la elimu kwa waandishi wa habari lilipewa kipaumbele huku wadau wakitaka taaluma ya uandishi wa habari kuwapo ukomo wa elimu inayotakiwa kwa kila anayefanya kazi ya habari.
Katika mkutano mwingine wa TEF na wadau wa habari ulioendeshwa na Wakili James Marenga, amesema yanahitajika mabadiliko kwenye Sheria ya Makosa ya Mtandaoni ya mwaka 2015 na Sheria ya Kupata Taarifa ya mwaka 2016, ikiwa ni pamoja na kanuni zake za mwaka 2017.
Marenga anasema vipo baadhi ya vifungu na vipengele vyenye upungufu ambavyo vinahitaji kufanyiwa mabadiliko ili sheria hizo ziwe bora na zilete ufanisi.
Anasema umuhimu wa kuwa na sheria rafiki za vyombo vya habari kunachochea ustawi wa maendeleo ya nchi, huku akidai kuwa jambo hilo halipaswi kudaiwa kwa nguvu ilhali watu wanafahamu umuhimu wa kuwa na sheria nzuri za habari.
“Sheria ikiwa rafiki wadau na waandishi wa habari watafanya kazi zao kwa kujiamini bila kukinzana na sheria, na watafanya kazi kwa manufaa ya umma,” anasema Marenga.
Akiizungumzia Sheria ya Huduma ya Habari ya mwaka 2016, anasema iliitambua Sheria ya Habari kama taaluma ya kuheshimika, huku ikiitaja Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 kuwa na upungufu mwingi.
Anasema Kifungu cha 3 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao hakijatoa tafsiri ya neno ‘publish’ (kuchapisha), pia kikitumia neno ‘in other way’ (kwa vyovyote vile), maneno ambayo yanaweza kutumika kufifisha uhuru wa habari.
“Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao, changamoto yake ipo kwenye neno ‘false information’, nalo halijapewa tafsiri, hapa watekelezaji wa sheria wanaweza kulitumia kamkandamiza mhusika,” anasema Marenga.
Aidha, anaitaja changamoto nyingine ya Sheria ya Makosa ya Mtandao kuwa ni kutoa nafasi kwa mamlaka kutoa adhabu isiyo na kikomo.
Katika mkutano huo, wadau wanaitaka sheria hiyo kuwa na ukomo wa adhabu, iseme wazi mhusika atafungwa miaka kadhaa badala ya kutumia neno ‘less than’, huku ikishindwa kutamka ukomo huo.
Vilevile wadau katika mkutano huo wamependekeza kufutwa kwa kipengele cha saba ambacho kinazuia mhusika kufuta taarifa kwenye vifaa vya kielektroniki anavyomiliki, kwani kinaondoa haki ya faragha.
Katika mkutano huo wadau wanataka kurekebishwa kwa kifungu cha 31 kinachoruhusu mamlaka kuchukua vifaa vya kieletroniki vya mhusika na kuvishikilia kwa uchunguzi.