DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Kwamba amani ni muhimu katika maisha ya kila siku ya binadamu ni suala lisilokuwa na ubishi.

Amani ni nguzo ya maendeleo. Bila amani hakuna shughuli zozote za kijamii zinazoweza kufanyika. Bila amani maisha ni ya shaka kubwa.

Kwa kawaida hata viapo vya viongozi wakubwa katika kila taifa huelekezwa katika kulinda amani na uhuru wa wananchi wa nchi husika, huku wakiomba msaada wa Mwenyezi Mungu. 

Amani ni suala mtambuka duniani. Mataifa hujitahidi kwa kila hali kulinda mipaka yake. Jumuia ya kimataifa nayo husaidia katika kulinda amani kule ambako ‘amani imetoweka na taifa haliwezi kujilinda lenyewe’.

Aghalabu amani ikitoweka wanaoathirika zaidi ni wanawake, watoto na wazee.

Wapo watu nchini ambao wameyatoa maisha yao kusaidia kuwapo kwa amani nje ya Tanzania, mmoja wao akiwa ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Eva Stesheni.

Mama huyu ni mmoja wa askari kutoka mataifa mbalimbali waliowahi kuwa walinzi wa amani Darfur, Sudan.

Darfur, eneo lililokumbwa na adha na machafuko ya kila aina kwa miaka mingi, kwa hakika si eneo la kumvutia mtu kwenda, lakini SSP Eva amekwenda na kufanya kazi ya kulinda amani kwa vipindi viwili tofauti.

“Mimi ni askari polisi kwa miaka 22 sasa, nikianzia kazi Chang’ombe, Dar es Salaam, mwaka 2000,” anaanza kusimulia Afande Eva, mhitimu wa shahada ya sosholojia na mkufunzi wa Chuo cha Taalumu cha Polisi.

Afande Eva alihudumu Kituo cha Polisi Chang’ombe kwa miaka 10, ambapo mwaka 2009 hadi 2011 alishiriki ulinzi wa amani Darfur chini ya Umoja wa Mataifa (UN).

“Katika Jimbo la Darfur nilikuwa Ofisa Mshauri wa Jinsia na Watoto; baadaye nikawa Mratibu wa Kituo cha Polisi Jamii Elisalaam,” anasema. 

Eva alirudi nyumbani mwaka 2012 na kuendelea na kazi yake ya awali, ukufunzi chuo cha taaluma ya polisi hadi mwaka 2014 alipohamishiwa Kituo cha Polisi Wazo Hill kuwa Mkuu wa Kituo.

“Nikarejeshwa tena Darfur mwaka 2016. Kazi niliyopewa safari hii ni Msaidizi Maalumu wa Kamishna wa Polisi wa Sudan upande wa UN katika Makao Makuu ya UN-AMID. 

“Nikadumu huko hadi mwaka 2018 na kuwa Mkuu wa Kituo cha Polisi Salender Bridge. Baadaye nikahamishiwa Kibaha mkoani Pwani. Kwa sasa mimi ni Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kisarawe,” anasema Afande Eva.

Tishio la kifo, kutekwa

Ulinzi wa amani eneo la Darfur si suala la lelemama hata kwa askari, na Afande Eva anasimulia matishio ya kiusalama kwake kama mlinzi wa amani, tena mwanamke.

“Ni hatari. Mwenendo wa kisiasa wa Sudan, taifa lililokumbwa na kadhia ya vita ya muda mrefu, ulisababisha shida kwa walinzi wa amani.

“Askari wa kulinda amani mara kwa mara tulishindwa kufika kwa wakati (eneo wanakotakiwa) na wakati mwingine muda wa kuripoti unakwisha.

“Hata uingizaji wa vifaa mbalimbali na misaada ya kibinadamu inakuwa ni shida kubwa. Hali hii ilituathiri sisi walinzi wa amani na wakimbizi waliokuwa kwenye makambi,” anasema.

Uhaba wa fedha za bajeti unaosababisha kushindikana kwa mipango ya kuongeza idadi ya walinzi wa amani ni suala jingine lililokuwa kikwazo katika kazi hiyo muhimu kwa binadamu. 

“Ukiwa kule unapaswa kujifunza tamaduni za watu asilia ili uendane na maisha yao. Hii nayo ni shida pia,” anasema Eva.

Hali ilivyokuwa

Kati ya mwaka 2009 mpaka 2010 kulikuwa na wimbi kubwa la vifo na mauaji Jimbo la Darfur kutokana na umiliki holela wa silaha.

“Kwa hiyo UN walitusaidia kuwapatia elimu raia kwa njia ya polisi jamii. Tuliwaelimisha na hatimaye wakarudisha silaha walizokuwa wakizimiliki. 

“Katika kipindi hiki tulifanya kazi kubwa kurudisha imani ya jeshi kwa raia wa Darfur. Hawakuwa wakilipenda kabisa jeshi la polisi.

“Baada ya kuwashawishi raia wakarudisha silaha, tukaanza kuwafundisha polisi jinsi ya kuishi vema na jamii. Mauaji yakapungua. Niliporudi mwaka 2016, nikakuta hali shwari.

“Tulifanikiwa kulifanya jeshi hilo kuwa na viwango vya kimataifa na kuhamasisha ushiriki wa polisi wanawake wenye vyeo vya juu kupata nafasi, kwani kipndi hicho alikuwa mmoja tu ambaye alikuwa na cheo cha sajenti,” anasema Afande Eva. 

Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula, anasema serikali itaendelea kuwaenzi walinda amani wote waliojitolea na wanaoendelea kujitolea kuisaidia jamii katika mataifa yenye machafuko.

“Tuna askari wetu kuanzia Lebanon, Sudan Kusini na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

“Tanzania tunaamini katika amani, umoja, kulinda mipaka yetu na tunaamini katika ujirani mwema.

“Lakini kitu muhimu zaidi ni kwamba tunauamini Umoja wa Mataifa na mchango wa jumuiya ya kimataifa katika kuleta amani na usalama duniani,” anasema Balozi Mulamula.

Mwakilishi wa UN nchini Zlatan Milisic, amewapongeza walinda amani akisema: “Hawa wanafanya kazi kubwa duniani kwa kuhakikisha wanalinda amani pamoja na changamoto wanazopitia.”