Serikali imeingia doa. Migomo wafanyabiashara na madereva wanaoendesha mabasi ya abiria, imetikisa nchi kiasi cha kufanya wadau kadhaa kueleza kuwa nchi imekosa sifa za uongozi.
Tukio la kwanza, ambalo limekuwa likijirudia linahusu wafanyabiashara ambao mara kwa mara wamekuwa wakigoma kwa kufunga maduka kwa shinikizo la kuachiwa Mwenyekiti wao, Johnson Minja.
Tukio la pili ni la madereva, ambao Ijumaa iliyopita walitekeleza azimio la kugoma kusafirisha abiria wa ndani ya ya mikoa yao na wale wa nje, wakipinga mpango wa Serikali.
Akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalum yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu anasema, “Hizi sasa si dalili tena, ni dhahiri kuwa CCM na Serikali yake wamechoka.”
“Nitashangaa. Nitashangaa sana kuona wananchi ambao wanakosa huduma kwenye maduka, wanakosa huduma hata ya usafiri wakabaki kuendelea kuiamini CCM na Serikali yake.”
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki, anasema kwamba imefika wakati wa kuipeleka “likizo CCM,” kwa sanduku la kura itakapofika Oktoba, mwaka huu.
“Sasa kama mtu unatembea kwa mguu kutoka Ubungo hadi Kariakoo…kama mtu una safari zako muhimu, kama umefiwa au unakwenda kwenye biashara zako, mikoani au nje ya nchi, unashindwa kusafiri unategemea nini?
“Leo sitaki kuzungumza sana, lakini hali imeonekana. Watu wanajionea mambo yalivyo, hivyo nao leo waseme kwa namna mambo yanavyokwenda,” anasema.
Katibu Mwenezi wa NCCR- Mageuzi, David Kafulila, anasema ni kama Serikali haina uongozi, “…na sifa za serikali ya namna hiyo ni kutafuta kuchukua hatua baada ya kutokea tatizo.”
Kafulila ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kusini, anasema, “Serikali hii imekuwa dhaifu mno katika utekelezaji wa sheria na kwamba itaendelea kupokea migomo ya kila namna kwa kuwa imelemewa na viongozi wabovu na mizigo ambao hawajui wapo kwa ajili ya nini?”
Anasema tatizo la migomo ikiwemo ya wafanyabiashara na madereva lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita yamechangiwa na kukosekana kwa uongozi, ambao unasubiri moto uwake ndipo utafutiwe utaratibu wa kuuzima na kuwaumiza wananchi bila sababu za msingi.
“Kila wiki mamia ya watu hupoteza maisha kwa ajali za barabarani ambazo zingeweza kuzuilika, kwa sababu sheria hazina wasimamizi na Askari wa Usalama barabarani wanaendekeza rushwa tu, iko siku wananchi wataandamana kwa kuchoshwa na ajali hizi,” anasema Kafulila.
Anasema Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe ni mzigo na amepoteza sifa za Uwaziri kutokana na kukithiri kwa ajali za barabarani ambazo yeye anaona kuwa ni jambo la kawaida mamia ya wananchi kupoteza maisha kila wiki kwa matukio ya ajali hizo.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama kipya cha Kizalendo ACT-Tanzania, Samson Mwigamba anasema kwamba Serikali imekuwa ikifanya uamuzi wa kukurupuka.
“Kwa bahati nzuri, mimi ni Mhasibu mwenye CPA. Najua umuhimu wa mashine za EFD’s. Mashine hizo ni nzuri, kama zina ubora, ila kuna shaka ya Serikali kupunjwa akafaidika mfanyabiashara au mfanyabiashara akanyonywa na serikali ikafaidika,” anasema.
Akifafanua zaidi, Mwigamba anasema mfumo wa kodi haupaswi kuwa wa gharama ikilinganishwa na kodi inayokusanywa.
“Haiwezekani mfanyabiashara anayevuna Sh. 25,000 akanunua mashine ya Sh. 800,000. Mbaya zaidi hujaita wafanyabiashara ukazungumza nao,” anasema Mwigamba.
Minja ambaye amefunguliwa kesi katika Mahakama ya hakimu Mkazi Dodoma, anadaiwa kuchochea mgomo wa wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakifunga maduka yao mara kwa mara kupinga matumizi ya mashine za kielektroniki (EFD’s) zinazoelekezwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakidai zinawapunja.
Mara ya mwisho alipelekwa rumande Machi 26, mwaka huu kabla ya kuachiwa siku mbili baadaye baada ya wabunge kuishinikiza Serikali iingilie katia sakata la mgomo wa wafanyabiashara wa maduka nchini.
Mgomo huo umekuwa ukifukuta upya katika baadhi ya mikoa baada ya kiongozi huyo kukamatwa tena na kufutiwa dhamana mapema mwezi huu akidaiwa kuhamasisha wenzake kufunga maduka kushinikiza TRA.
Mbali ya mgomo huo, kuna hili la marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani kwa kuingiza kipengele kinachowataka madereva kwenda Chuo cha Usafirishaji (NIT) kwa mafunzo ya muda mfupi mara kila wakati leseni zao zinapoisha ili kupata sifa ya kupata leseni nyingine.
Utaratibu huo uliotangazwa Machi 30, mwaka huu, ulipingwa vikali huku madereva wakidai kuwa hawakushirikishwa katika kuiandaa.
Madai hayo ni pamoja na kuondolewa kwa ulazima wa kusoma kila baada ya miaka mitatu na kujilipia gharama za mafunzo ambazo walidai ni Sh. 560,000 kwa magari ya kawaida na Sh. 200,000 kwa magari ya abiria.
Madereva hao pia wanadai kuwa hawawezi kuhudhuria mafunzo hayo wakati hawana mikataba ya ajira inayoweza kuwahakikishia kazi zao zinalindwa hadi wanapomaliza mafunzo.
Madai mengine ni kuondolewa kwa faini ya Sh. 300,000 kwa kila kosa la barabarani, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kuhakiki uhalisi wa dereva anayeandikishwa na mmiliki wa chombo husika.
Mwigamba anasema, “Madereva hawa hawana uhakika wa ajira watakapomaliza mafunzo hayo kwa sababu uhaba wa ajira unajulikana. Na hawana mkataba wa kudumu. Serikali inakurupuka.”
Hali hiyo ilizua taharuki mwishoni mwa wiki katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo (UBT) madereva walifanya mgomo wa zaidi ya saa nane kuishinikiza Serikali kufuta matumizi ya kanuni mpya za udhibiti wa safari na usalama.
Naibu Waziri wa Wizara ya Chakula, Kilimo na Ushirika, Godfrey Zambi anasema kuwa Serikali imechelewa kuchukua hatua katika suala la migomo ya wafanyabiashara maana yamekuwepo malalamiko muda mrefu, lakini hakuna aliye tayari kutoa ufumbuzi wa kudumu.
“Haya mambo yanaingizwa na masuala ya kisiasa lakini ufike wakati serikali isikubaliane na mashinikizo yanayotolewa bali ishughulike na kero mapema ili kuondokana na mashinikizo na migomo ya aina hii,” anasema Zambi ambaye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya.
Zambi anaeleza kuwa iwapo nchi itakuwa ikikumbwa na mogomo ya mara kwa mara nchi itakuwa kwenye hatari kutokana na Serikali kulazimishwa kufanyakazi kwa mashinikizo hivyo kujikuta ikipoteza dira na malengo yake katika kuihudumia jamii.
Hata hivyo, mzozo huo ulizimwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka aliyekwenda Ubungo akiwa ameongozana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Maoni ya wananchi
Akizungumzia migomo inayoendelea kushika kasi nchini, Ayubu Amani (34), mkazi wa jijini hapa ambaye ni dereva anadai hali hii imechangiwa na udhaifu wa Serikali ambayo imekuwa ikipuuza kila jambo jema lenye maslahi kwa wananchi na nchi.
Anasema leseni zimepanda kutoka Sh. 10,000 hadi kufikia 40,000, madereva hawana ajira na wanachotegemea ni posho ya Sh. 40,000 na wengine Sh. 18,000 huku serikali ikipuuza malalamiko yao ya muda mrefu kwa kuwanyima haki zao za msingi ndio jambo linaloibua migomo ya namna hii.
“Ubovu wa sheria zilizopo ambazo zimeleta ubaguzi kitabaka kati ya madereva nchini, huku wanaotambuliwa ni wale waliajiriwa na serikali na wanaofanya kazi kwa wamiliki binafsi wa vyombo vya usafiri hawana ajira”, anasema Amani.
John Brown Kapesa (60), Mkazi wa Mbezi, anasema matukio haya yanaonyesha wazi Serikali imeanza kushindwa kufanya uamuzi sahihi kwa wananchi kutokana na kupanga uamuzi bila kuangalia wananchi.
“Madereva wa daladala wanapata posho ya Sh. 10,000 kwa siku sasa hiyo Sh. 600,000 atazitoa wapi? Hizi ni njama za serikali kutaka kujiingizia kipato katika chuo chao,” anasema.
Maria Kanza (45) wa katikati ya jiji la Dar es Salaam, anasema kuwa tukio hilo ni fundisho kwa Serikali inapotokea madai ya msingi ya wananchi.
Anasema kuwa Serikali sasa haina budi kuacha kudharau.
Mwanafunzo wa Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Veronica Temba anasema kwamba mgomo wa usafiri Ijumaa iliyopita ulisaabisha kushindwa kufanya mitihani yao.
“Hali hii inaonyesha wazi kuwa serikali imeshindwa kuongoza nchi yetu maana wanashindwa kutatua matatizo kama hayo ambayo yak0 ndani ya uwezo wake,” anasema Veronica.