MOMBASA

Na Dukule Injeni

Hatimaye wagombea urais, hususan wa muungano wa Azimio la Umoja One, Kenya Alliance na Kenya Kwanza

wameteua wagombea wenza siku chache tu kabla ya Mei 16, mwaka huu, iliyotengwa na Tume Huru ya Uchaguzi

na Mipaka (IEBC) kuwa siku ya mwisho.

Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga, mgombea urais wa Azimio la Umoja, amemteua Martha Karua kuwa

mgombea mwenza kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Agosti 9, mwaka huu.

Naibu Rais William Ruto, anayewania urais kupitia United Democratic Alliance (UDA); moja ya vyama ndani ya

Kenya Kwanza, amemteua Rigathi Gachagua kuwa mgombea mwenza.

Wote Gachagua na Martha wanatoka eneo la Mlima Kenya, ambalo kwa mara ya kwanza halina mgombea urais mwenye ushawishi mkubwa kumrithi Rais Uhuru Kenyatta, hivyo kuwataka vinara wanaowania urais kuchagua wagombea wenza kutoka eneo hilo lenye idadi kubwa ya wapiga kura.

Ni wazi Ruto na Odinga walihitaji mwanasiasa kutoka Mlima Kenya atakayewahakikishia kura nyingi za eneo

hilo na bila shaka hadi sasa tayari wapiga kura kutoka Mlima Kenya wameshagawanyika.

Uteuzi wa Martha uliamsha shangwe kwa kina mama wengi, wakimuona kama ni mmoja wao huku Odinga

akimmiminia sifa kuwa ni mpambanaji na si mtu anayekata tamaa mapema, akisisitiza nchi itakuwa kwenye mikono salama.

“Huyu mwanamke ana roho nzuri kama inavyoonyesha

kwenye mapenzi kwa watoto na wajukuu wake… Ni mbunifu, msaidizi mzuri na atakuwa mwanamke wa

kwanza kuwa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya,” amesema Odinga.

Mbali na kumteua Martha kuwa mgombea mwenza wake, Odinga pia amesema endapo watashinda, atamuongezea majukumu mengine ambapo atakuwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba.

Lengo hilo linatokana na nia ya Odinga kufanya maboresho kwenye Katiba iliyopitishwa mwaka 2010, jaribio ambalo kwa kushirikiana na Rais Kenyatta walishindwa kulifanikisha kupitia ‘Building Bridges Initiative (BBI)’.

Martha ambaye ni kiongozi wa Chama cha NARC Kenya, aliwapiku wawaniaji wengine 11 waliofika mbele ya jopo maalumu kupigwa msasa.

Hao ni kiongozi wa Chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Murang’a, Sabina

Chege, aliyekuwa Mbunge wa Gatanga, Peter Kenneth, Gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho kutoka Chama cha

ODM na kiongozi wa National Liberal Party, Stephen Tarus.

Wengine ni Waziri wa Kilimo, Peter Munya, Gavana wa Kakamega kutoka Chama cha ODM, Wycliffe Oparanya,

Gavana wa Kitui ambaye pia ni kiongozi wa NARC, Charity Ngilu na Gavana wa Nakuru, Lee Kinyanjui.

Naibu Rais Ruto naye akamchagua Gachagua badala ya Seneta wa Tharaka Nithi, Profesa Kithure Kindiki, licha ya kupata kura nyingi kutokana na ushawishi wake kwa wapiga kura na kwamba kwa muda mrefu amekuwa

akimtetea Ruto.

Aidha, Gachagua ni chaguo la Ruto akiamini yeye ni kiungo muhimu katika kutekeleza mabadiliko ya kiuchumi endapo Kenya Kwanza itashinda uchaguzi.

“Nataka niwahakikishie kuwa Rigathi ana moyo wa kuipambania nchi na nilihitaji mtu mkakamavu. Kenya inahitaji mtu mkakamavu ambaye anaweza kukabili changamoto za nchi yetu. Naye ni Rigathi,” amesema.

Ruto aliongeza kuwa amemchagua Gachagua kwa sababu ni mchapakazi na anamjali mwananchi wa kawaida.

Wawili hawa hawakukutana barabarani, kwani wamesoma darasa moja katikati ya miaka 1980 wakiwa Chuo Kikuu cha Nairobi, baadaye wakatumikia utawala wa hayati Rais Daniel arap Moi kudhibiti vuguvugu la wanafunzi waliokuwa na misimamo mikali dhidi ya serikali.

Vivyo hivyo, kwa Odinga na mgombea mwenza wake, Martha, wamekuwa pamoja wakipambana dhidi ya utawala wa chama kimoja chini ya Rais Moi wakitetea demokrasia na haki za binadamu mwanzoni mwa miaka ya 1990.

Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa siasa na amewahi kufanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya Kenya, ikiwamo Tanzania.