*Yatupiwa lawama ikipachikwa majina ya ‘njia panda ya kuzimu’, ‘ukienda hutoki’
*Mgonjwa alazwa siku sita, atibiwa mara mbili tu akitozwa Sh milioni 1.8
*JAMHURI lapiga kambi siku kadhaa kubaini ukweli, hali halisi ya mambo
*Uongozi wazungumza, wasema lawama nyingi si za kweli, zinawaathiri
Dar es Salaam
Na Alex Kazenga
Kwa takriban miaka minne na nusu sasa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili Kampasi ya Mloganzila imejikuta ikigubikwa na lawama nyingi kuliko sifa.
Mloganzila, hospitali kubwa na ya kisasa, ilizinduliwa Novemba 25, 2017 ikitarajiwa kuwa msaada wa kupunguza msongamano wa wagonjwa waliokuwa wakiilemea Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo Upanga, Dar es Salaam.
Badala yake, kumekuwa na taarifa za kukatisha tamaa zinazoihusu na kusababisha watu kuogopa kwenda kutibiwa au kuwapeleka huko wagonjwa wao.
Mmoja wa watu waliowahi kupata huduma hospitalini hapo (jina tunalihifadhi), ameliambia JAMHURI kuwa ukubwa wa gharama za matibabu unaifanya Mloganzila kupoteza sifa ya kuitwa ‘hospitali ya umma’.
“Wanaoshindwa kulipa gharama za matibabu huzuiwa kuondoka hadi watakapolipa senti ya mwisho. Lakini hata mazingira ya wodini ni mabovu na wafanyakazi hawawajali wagonjwa,” anasema.
Mtoa habari wetu ambaye ni mwandishi wa habari mwandamizi anadai kuwa mwishoni mwa mwezi uliopita alikwenda Mloganzila kupata matibabu ya shinikizo la juu la damu na kisukari; magonjwa yanayomsumbua kwa muda sasa, hakupata matibabu ya ‘kueleweka’ hivyo akaamua kwenda kutibiwa hospitali binafsi.
Amesema alianza kuona dalili za kutohudumiwa vizuri tangu akiwa mapokezi ya wagonjwa wa dharura (emergency), alipokaa kwa saa tatu bila kusikilizwa na hata aliposikilizwa alibaini gharama zinazotolewa hapo kuwa ni kubwa sana.
Baada ya kufanyiwa vipimo, akapelekwa wodini alikolala siku tatu bila kupatiwa matibabu ya aina yoyote.
“Siku ya tatu ilibidi nianze fujo wodini ndipo madaktari na manesi wakaja kuniona. Nilichokibaini kwa haraka ni kwamba pale hakuna uratibu wala ushirikiano mzuri miongoni mwa wafanyakazi,” anasema.
Anawalaumu manesi kwa kutokuwa na huruma wala kauli nzuri kwa wagonjwa, akisema wanafanya kazi kwa mazoea, wakidhani kuwa wote wanaokwenda kutibiwa hapo ni watu wa hali ya chini.
“Baada ya kuona mazingira si rafiki, niliomba kuondoka. Huwezi kuamini, kwa siku sita nilizolazwa hapo, nilipewa tiba kwa siku mbili tu lakini nikaletewa bili ya Sh milioni 1.8!” amesema.
Alipouliza sababu ya ukubwa wa gharama anazodaiwa, akajibiwa kuwa alikuwa akipatiwa huduma ya matibabu ya ‘private’, ilhali kwa siku zote hizo alikuwa amelazwa wodi mchanganyiko na wagonjwa wengine.
“Kabla sijafanya uamuzi wa kuondoka Mloganzila, niliomba kuondolewa kwenye orodha ya wagonjwa wa ‘private’, viongozi wakagoma,” anasema.
Hapo ndipo alipoomba kuondoka, lakini akatakiwa kuandika maelezo kwamba ameondoka kwa hiari yake; wakagoma kumuandikia ugonjwa unaomsumbua na dawa alizokuwa akipewa.
Mjamzito naye atema nyongo
Likiwa Mloganzila, Gazeti la JAMHURI limezungumza na mjamzito aliyefika na kujifungua kwa njia ya upasuaji. Mama huyu analalamikia suala la usafi katika wodi ya wazazi.
“Nilipofika nilitumia mashuka ya hospitali kwa siku mbili bila kuondolewa kwenda kufuliwa, kwa hiyo nikalazimika kutandika vitenge juu ya mashuka yale machafu,” anasema.
Kauli hii inaungwa mkono na mtoa taarifa wetu, mwandishi wa habari mwandamizi aliyeikimbia hospitali hiyo, akisema alipofika kwa mara ya kwanza hospitalini hapo alikosa mashuka ya kujifunika usiku kwa maelezo kwamba yote yalikuwa yamechukuliwa.
JAMHURI limepata pia simulizi nyingine ya kusikitisha kuhusu huduma za Mloganzila kutoka kwa mwananchi mmoja ambaye mtoto wake sasa ni mgonjwa wa kudumu wa hospitali hiyo; simulizi ambayo hatuwezi kuiandika kwa sasa kwani itamfichua na kumpa wakati mgumu.
“Uzuri wa hii hospitali ni majengo ya kisasa, ila upande wa huduma si wazuri kabisa. Ukitaka kuwajua vizuri njoo na bima ya afya uone utakavyohangaika kupata matibabu. Hawakujali kabisa! Utashangaa unapitwa kama hawakuoni. Wenyewe wanataka wagonjwa wa ‘cash’,” anasema Mtanzania huyo anayeuguza mtoto kwa muda mrefu.
Ni taarifa hizi kutoka kwa watu mbalimbali na nyingine zilizozagaa mitaani zikiipachika Mloganzila majina kama ‘njia panda ya kuzimu’ na ‘ukienda hurudi’, ndizo zilisababisha Gazeti la JAMHURI kuweka kambi kwa siku kadhaa kufuatilia kwa kina.
Viongozi wanena
Mkuu wa Kitengo cha Ustawi wa Jamii, Agricola Mushi, anapinga kuwapo changamoto katika hospitali hiyo, akidai kuwa Mloganzila kwa sasa ndiyo kinara katika utoaji wa huduma bora ya matibabu kuliko hospitali nyingine za Dar es Salaam.
“Hii ni hospitali ya rufaa. Wagonjwa wanaoletwa hapa hufanyiwa vipimo vikubwa kuona tatizo, hivyo matibabu watakayopewa baada ya vipimo lazima yawe makubwa pia,” anasema Agricola.
Anapinga lawama kuhusu kutothaminiwa kwa wenye bima ya afya akidai kuwa hupewa kipaumbele.
Kuhusu wagonjwa wasio na bima ya afya huku pia wakiwa hawana fedha za kugharamia matibabu, Agricola anasema Kitengo cha Ustawi wa Jamii huwafanyia uchunguzi na wasio na uwezo hupangiwa utaratibu mzuri wa kulipa deni kidogo kidogo baada ya kupata matibabu.
Kwa upande mwingine, Msimamizi wa Dawati la Huduma Bora kwa Wateja, Hadija Thabith, anashangaa wagonjwa na watu wengine kuilalamikia Mloganzila nje, ilhali kuna dawati la kupokea malalamiko na kuyafikisha haraka kwa viongozi.
“Tupo hapa kusikiliza kero zote za wagonjwa, mpaka tumeweka sanduku la maoni kwa ajili ya kupokea maoni na malalamiko kama hayo. Huyo mgonjwa aliyeondoka (mwandishi wa habari mwandamizi), mbona hakufika kwenye dawati letu? Tungemsikiliza,” anasema Hadija.
Uongozi wa juu wafafanua kwa kina
Akizungumza na JAMHURI kuhusu lawama na visa vinavyohusishwa na hospitali hiyo, Kaimu Mkurugenzi Huduma za Tiba Mloganzila, Dk. Mohammed Mohammed, anasema Mloganzila inaathiriwa sana na taarifa nyingi za uongo.
Anakumbuka kisa cha baba aliyempeleka mtoto wake aliyekuwa amefanyiwa vibaya upasuaji wa goti (katika hospitali nyingine, jina tunalihifadhi) na kupata tatizo la kuganda damu.
Anasema pamoja na juhudi zilizofanywa na madaktari wa Mloganzila huku wengine wakijitolea kumpatia damu, mwishowe alifariki dunia.
“Baba alipoona mwanaye amekufa, akapiga simu kwa Waziri wa Afya akidai kwamba amefika Mloganzila lakini hakupata huduma yoyote.
“Taarifa zilipotufikia, yule baba akaitwa. Kikafanyika kikao. Mkuu wa idara akatoa faili la matibabu ya yule mtoto. Baba aliposomewa yote yaliyofanyika kwa mwanae, ilibidi aombe radhi kwa kusema uongo,” anasema Dk. Mohammed.
Dk. Mohammed anasema hata wao pia ni binadamu, tena Watanzania, wala si malaika na kwamba wanapopewa taarifa za upungufu uliopo wanapata nafasi ya kuboresha huduma.
“Umezungumzia suala la mtu kukaa saa tatu mapokezi ya dharura bila kuhudumiwa. Hilo naweza kukubaliana nalo lakini si kwa wagonjwa wa nje (OPD).
“Watanzania tunapenda urahisi, mtu anaweza kuamua kupita mlango wa huduma ya dharura akitegemea kupata huduma haraka. Hiyo si sahihi,” anasema Dk. Mohammed, akiongeza kuwa eneo la dharura limetengwa mahususi kwa ajili ya kuhudumia magonjwa yanayohitaji huduma za haraka kama kuvuja damu, kupoteza fahamu au pumzi.
Anataja tatizo jingine la hospitali hiyo kwamba, kwa kuwa ni hospitali ya rufaa, wagonjwa wengi wanaokwenda hapo huwa tayari wamedhoofika kiafya huku wengine wakitokea kwa waganga wa jadi ambako wameshindwa kupata nafuu.
Akizungumzia Mloganzila kwa ujumla, Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi na Ukunga, Dk. Redemptha Matindi, anasema kuna ongezeko la wagonjwa kutoka wagonjwa 200 kwa siku wakati imeanza kufanya kazi mwaka 2017 hadi wagonjwa 600 kwa siku.
Anasema miongoni mwa wagonjwa hao, asilimia 90 ni wenye bima ya afya; asilimia tano ni wagonjwa wanaolipa fedha taslimu na asilimia tano nyingine ni wanaotibiwa kwa deni.
Dk. Redemptha anasema wafanyakazi wote kwa jumla wanapambana kwa hali na mali kuhakikisha huduma bora zinatolewa lakini kutokana na kufanya kazi kwa viwango ambavyo havijazoeleka nchini, hujikuta wakiishia kupata lawama.
“Hospitali hii ni ya kisasa. Ina lifti tisa, ina mashine za kufua, kukausha na kupiga pasi nguo. Bili ya umeme tunaotumia kwa mwezi ni Sh milioni 170. Tukianza kulalamika na kusikiliza wanavyotaka wananchi, hatuwezi kuiendesha,” anasema.
Anasema kuna watu hutoka kwenye matibabu katika hospitali binafsi wanakotozwa gharama kubwa, lakini wakifika Mloganzila huanza kulalamikia gharama wakitaka watibiwe kwa fedha kidogo.
Kuhusu malalamiko ya mwandishi wa habari mwandamizi aliyezungumza awali na JAMHURI, Dk. Redemptha anasema uwezekano mkubwa ni kwamba hakufika hospitalini kwa utaratibu unaotakiwa wa kuwa na rufaa.
“Ni kweli hospitali nyingi za serikali kwa sasa zina utaratibu wa huduma ya ‘private’. Huyu anayedai kuchanganywa na wagonjwa wengine akiwa wa ‘private’, angezitaka wodi hizo, zipo na gharama zake zinajulikana. Huku unalipia kila siku unayolala,” anasema.
Hata hivyo, anasema si rahisi mtu aliyekwenda mwenyewe hospitalini bila rufaa kubadilishiwa huduma kwenda kwenye matibabu ya umma, kwani kuna hatua za kufuata ambazo huchukua muda mrefu.
“Hapa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) akija kukagua akakuta mtu binafsi tumemhamisha bila utaratibu kufuatwa, lazima atahoji. Itaonyesha wazi kuna rushwa imetumika,” anasema.
Kwa upande mwingine, anasema hospitali hiyo inakumbana na wakati mgumu hasa kutoka kwa watu wanaotibiwa na kushindwa kulipa, matukio yanayotokea mara kwa mara.
Anadai kuna wanaoambiana kwamba ukilazwa Mloganzila na kushindwa kulipa, ukizuiwa kuondoka utalishwa na kulazwa bure na hatimaye utaachiwa.
“Hata hao wanaoeneza sifa mbaya za hospitali huenda ni miongoni mwa tunaowadai, sasa wanatumia mwanya huo kutaka kukwepa madeni,” anasema.
Kuhusu uchafu na upungufu wa mashuka, Dk. Redemptha amekanusha, akisema yapo ya kutosha na usafi hufanyika kila siku.
JAMHURI limefika katika baadhi ya wodi zilizopo ghorofa ya nane na tisa na kushuhudia vyoo na mabafu vikiwa katika hali ya kuridhisha.
Anasema Mloganzila ina idadi ya kutosha ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wanaotoa huduma kwa saa 24, hivyo hakuna uwezekano wa kutolewa huduma duni.
“Hapa tunao wanafunzi wanaojifunza kwa vitendo, tunao madaktari walioajiriwa na tunao madaktari wanaosomea ubobezi, hawa wote wanapita kuona wagonjwa.
“Madaktari wanafunzi hatuwaruhusu kufanya uamuzi juu ya mgonjwa lakini kituo chao cha kazi ni wodini, wao kazi yao ni kuangalia maendeleo ya mgonjwa na kutoa ripoti kwa daktari mhusika,” anasema Dk. Redemptha.