Wiki hii serikali imetangaza kukubali maombi ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ya kupandisha kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa umma nchini.
Haya ni maombi ya muda mrefu na mara kwa mara serikali imekuwa ikishindwa kuyatekeleza kwa sababu moja au nyingine; lakini sasa imeamua kupandisha mshahara kwa asilimia 23.3.
Katika sherehe za Mei Mosi za mwisho kwa Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, ombi hili lilitolewa katika muktadha wa utani, ambapo walimu walimuuliza; ‘shemeji unatuachaje?’
Maombi haya yalirejeshwa tena kwa Rais wa Tano, Dk. John Magufuli, aliyewaahidi wafanyakazi kuwapa nyongeza baada ya kumaliza uhakiki wa vyeti na wafanyakazi feki.
Yakaja tena wakati wa sherehe za kwanza za Mei Mosi kwa Rais wa Sita, Samia Suluhu Hassan, jijini Mwanza mwaka jana, naye akaomba muda ili ajipange na kuangalia mwenendo wa uchumi.
Hatimaye sasa nyongeza hiyo imetangazwa na walau Julai ya mwaka huu kwa wafanyakazi wa umma itakuwa tofauti kidogo na nyingine nyingi zilizopita.
Tunaamini kwamba nyongeza iliyotolewa na serikali, hata kama haikufika kile kiwango kilichopendekezwa na TUCTA, bado itasaidia kwa namna moja katika mapambano ya maisha.
Nyongeza hii sasa itumike kama hamasa na motisha kwa watumishi wa umma kuongeza tija na ufanisi kazini ili kuipa serikali sababu ya kuendelea kufanya hivyo kila mwaka.
Kauli zilizotolewa na viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT); Kaimu Rais Mwalimu Dinah Mathamani na Katibu Mkuu Mwalimu Deus Seif kabla hata ya nyongeza kutangazwa, zitumike kama dira ya watumishi wote wa umma.
Viongozi hawa walikaririwa na Gazeti la JAMHURI wakisema kwa nyakati tofauti kwamba upandishwaji wa vyeo na madaraja kwa watumishi wa umma, walimu wakiwamo, uliofanywa na serikali ndani ya mwaka mmoja umewafariji sana.
Wakatoa wito kwa walimu kuchapa kazi kwa bidii. Na sasa, kwa kuwa mishahara imeongezwa sambamba na kupandishwa kwa madaraja kwa watumishi wa umma, basi wito wa kufanya kazi kwa bidii uliotolewa na CWT unapaswa kuchukuliwa na kada zote.
Kaulimbiu ya ‘Haki na Wajibu’ itumiwe na kada zote za watumishi wa umma, kwamba wakati wanapodai nyongeza na kupewa, ndio wakati muafaka wa kuchapa kazi kwelikweli.