*Ni Sh bilioni 1.1 za zabuni ya kutengeneza sare za Mei Mosi

*Mzabuni adai amehujumiwa kwani mchakato wa zabuni uligubikwa na rushwa 

*Talgwu yasema itafuata taratibu za kisheria kufidiwa gharama 

*Wanachama wang’aka sare zao kutengenezwa chini ya kiwango 

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Fedha za Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) kwa ajili ya kuchapishia sare ambazo ni fulana na kofia za sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) ya mwaka 2022 zimechezewa.

Wakati fedha hizo zikichezewa, Talgwu ndiye alikuwa mratibu wa sherehe hizo kitaifa chini ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) na kufanyika Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi.

Gazeti la JAMHURI limetaarifiwa kwamba fedha hizo ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 1.1 zimechezewa baada ya mzabuni ambaye ni Kampuni ya Savana General Merchandise kupewa zabuni ya kuchapa sare 80,000 lakini zilizobainika kuchapwa kwa ubora uliotakiwa ni 900 na zilizobaki 79,100 zimebainika ni mbovu.

Pia limetaarifiwa kwamba mzabuni huyo alitafutwa na mjumbe mmoja wa bodi ya ununuzi (jina linahifadhiwa) huku akidaiwa alikuwa na uwezo mdogo wa mtaji wake kifedha wa kufanya kazi ya kuzichapa na alilipwa kabla sare hizo hazijafanyiwa uhakiki, jambo ambalo ni kinyume cha makubaliano ya mkataba wao wa zabuni.

Mbali na hayo, limetaarifiwa kwamba hiyo si zabuni ya kwanza kuwa na utata kwa sababu mara kadhaa kumeibuka ubadhirifu, udanganyifu na rushwa katika chama hicho pindi kinapofanya ununuzi.

Mathalani limetaarifiwa kwamba ununuzi wa sare za Mei Mosi, 2020 zilitumika zaidi ya Sh bilioni 1.2 lakini mzabuni (jina linahifadhiwa) alitengeneza fulana na kofia chache na kusababisha baadhi ya wanachama kukosa kutokana na mkataba wa zabuni kuwa na utata.

Pia limetaarifiwa kuwa kulikuwa na udanganyifu katika zabuni ya Mei Mosi, 2019 baada ya mzabuni (jina linahifadhiwa) kutengeneza sare 60,000 huku akilipwa malipo ya kutengeneza sare 80,000 na kofia hazikupelekwa.

Kutokana na kitendo cha mzabuni huyo inadaiwa kuwa ofisi za mikoa za chama hicho zikalazimika kununua kofia za wanachama wao.

Baadhi ya wanachama waliozungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti wiki iliyopita kwa masharti ya kutotajwa majina yao gazetini wamekasirika sare zao za mwaka huu kuwa chini ya kiwango.

“Haiwezekani chama tumemlipa mzabuni fedha za kutengenezea sare za Mei Mosi halafu anatuletea ‘maronyaronya’. Wewe hushangai, hata Rais Samia hajavaa sare ya Mei Mosi, mwaka huu.

“Sijui viongozi wetu wanatuchukuliaje na hii kila mwaka ikifika sare za Mei Mosi lazima utasikia jambo la hovyo linatokea, tumechoka kwa kweli,” amesema.

Mwanachama mwingine amesema makato wanayokatwa wanachama wa Talgwu kila mwezi ambayo ni asilimia mbili ya mishahara yao hayawasaidii wao bali yanawasaidia viongozi tu.

Amesema makato ya mishahara yao inawanufaisha viongozi wao kwa sababu wanayatumia kulipana posho za vikao, safari za nje na wanazifuja kadiri wanavojisikia kwa kuandaa makongomano na mafunzo yasiyokuwa na tija.

“Chama chetu hakitusaidii sisi wanachama bali kinawasaidia viongozi peke yao, kwa kuwa ni wababaishaji, si waaminifu, pia ni wabadhirifu na wala rushwa,” amesema.

Mwingine amesema wanachama wa Talgwu wamekuwa wakirubuniwa kwa fulana na kofia ambazo wakati mwingine hazina viwango bora.

Amesema wao hawahitaji fulana na kofia za Mei Mosi bali wanachohitaji ni kuongezewa elimu, mafunzo na maarifa katika maeneo yao ya kazi kutokana na michango yao wanayokatwa kila mwezi.      

Wenyeviti Talgwu mikoa wabaini sare mbovu

Kuanzia Aprili 22 hadi 24, 2022, baadhi ya wenyeviti kupitia kundi lao la WhatsApp la Talgwu Wenyeviti wa Mikoa wakatoa taarifa za kupokea sare mbovu kutoka kwa mzabuni huyo.

“Mimi nilikosa neno la kusema baada ya kupokea sare za Kanda ya Ziwa na kukuta kuna uozo uliokuwa katika vifurushi kama viazi vya Mbeya. Niligoma kuzipokea wala kusaini ‘delivery note’ ya mzabuni na hata kumrudishia mzigo wake.

“Hata huko mikoani sikuzituma. Kesho kama mkoa nitatoa tamko, maana uongozi wameshindwa na kutuona sisi kama watoto wadogo na tujisimamie kwa wanachama wetu, maana wao wanatutambua sisi na si mwingine,” amesema mwenyekiti mmoja.

Mwenyekiti mwingine wa Mkoa wa Mbeya akasema wanawaamini viongozi wao wa juu na akawataka wafanye utafiti wa kina kujua kwa nini mzabuni huyo afanye hivyo na nani yuko nyuma yake?

“Katika suala hili naomba tusitumie jazba, badala yake tutatue changamoto kwa pamoja, maana kati yetu hakuna ambaye anapenda litokee.

“Wenyeviti tumepata aibu ya mwaka, nashauri katibu mkuu azungumze na wanachama kisha aombe radhi kwa yaliyotokea na sisi tutabeba msalaba usio wetu, kwa Mbeya sare zote ni feki,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Kagera, Frank Kalembo, amesema waliwaamini viongozi wao na akawaomba watoe tamko kuhusu sare kama zipo au hazipo katika Mei Mosi.

“Nasi tupate cha kusema ili maisha yaendelee, maana hadi sasa katika mikoa hakuna cha kusema na niwaambie huduma ya Talgwu si sare tu bali zipo huduma nyingi. Tunaomba tamko na sisi tuendelee na maandalizi ya Mei Mosi,” amesema.       

Mwenyekiti wa Iringa amesema mwaka huu wameaibishwa na mzabuni, kwa sababu wamekuta hadi sare zilizochanika.

“Naomba kusema Mkoa wetu wa Iringa ni miongozi mwa iliyopokea mzigo wa fulana na niseme tu baada ya kufanya uchambuzi hakuna hata moja inayofanana na ‘sample’ kamili.

“Tumemwandikia katibu mkuu kama alivyotoa malekezo nini kifanyike kwa katibu wa mkoa, yaani ‘package’ ya mwaka huu kwa kweli mzabuni ametuumiza maana si sawa na alichokiweka ndani,” amesema. 

Mwenyekiti wa Tanga amesema hakuna shaka na suala la kuelimisha wanachama wao kutokana na changamoto iliyojitokeza kwa sababu wameshapata mwongozo.

“Utaratibu ni kila wilaya inaadhimisha sherehe za Mei Mosi kivyake, yaani hatufanyi maadhimisho kimkoa kwa hiyo mkoa wetu ungepewa mgawo wa zaidi ya hizo 500 angalau kila wilaya wakati wa maandamano waweze kushiriki sababu zikiwa chache italeta shida,” amesema.

Mwenyekiti Talgwu Taifa amlaumu mzabuni

Mwenyekiti wa Talgwu Taifa ambaye pia ni Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya, amenukuliwa na chombo kimoja cha habari akimtupia lawama mzabuni aliyepewa kazi ya kuchapisha sare zilizotakiwa kuvaliwa na wanachama wake katika Mei Mosi iliyofanyika Tanzania Bara.

Nyamhokya amenukuliwa akikiri chama chake kupokea fulana mbovu. “Sisi ndio wenye Talgwu na ndio tuliofanyiwa uhuni na huyo mzabuni, kwa hiyo tunazo hizo taarifa,” amesema na kuongeza:

“Sisi tumempa mzabuni na ndiye mwenye kazi, sasa alikwenda kuchapishia wapi, huo ni wajibu wake yeye. Of course chama kina ‘mechanism’ zake, kuna bodi ya zabuni na inatolewa kwa mtu mhusika na taratibu zote za zabuni. 

“Kwa hiyo makosa yakifanywa na mzabuni, zipo taratibu za kufuatwa, ikiwa pamoja na kumbana ili afidie hizo hasara. Huyo mtu anafanya zabuni za serikali na alivyokuja huku na CV zake zikaonekana, kwa hiyo akatunukiwa zabuni. 

“Baada ya kugundua tumesitisha kugawa, tunajaribu kuangalia namna nyingine ya kufanya watu wetu wanaoandamana kuvaa fulana. Kwa hiyo zile taratibu nyingine zinaendelea baada ya kumaliza Mei Mosi hizo zitafuata.” 

Mzabuni alia kuhujumiwa, atoa madai ya rushwa

Akizungumza na Gazeti la JAMHURI kwanza kwa njia ya simu kisha ofisini kwake wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Savana General Merchandise, Crispin Sanga, amesema walipokwenda India kuchapisha hizo sare kuna mshindani (Mhindi) wao mmoja alikwenda nchini humo kuwafanyia hujuma.

“Kumbe tuna taarifa kwamba huyo Mhindi ambaye tuliomba wote hiyo zabuni ndiye aliyetufanyia hujuma ya kwenda kule India baada ya kupeleka watu wao na akatuletea mzigo mwingine wetu ambao ni feki.

“Kwa sasa naenda Chamber of Commerce, nikitoka hapo naenda Ubalozi wa India kisha kwa Mkurugenzi wa Takukuru kwa jambo hili hili la sisi kuhujumiwa,” amesema.

Pia amesema wenyewe kwa wenyewe huko ndani ya Talgwu wana ugomvi wao na ndio walisababisha mambo yote haya.

Amesema wao wenyewe Talgwu wana vita yao humo ndani kwa ndani kuhusu zabuni hiyo na watajua baadaye ni nini kimetokea.

“Lakini ukweli kwa ujumla hali halisi ndiyo hiyo hapo, maana mikoani kote hizo fulana zilipokewa na baada ya kukagua belo la kwanza hadi la tatu lilikuwa safi, kumbe zinazofuata zilikuwa mbovu,” amesema na kuongeza:

“Baada ya kugunduliwa huko mikoani kwamba kuna fulana mbovu wakakubaliana hizo zisigawiwe kwa sababu zina dosari, hatuwezi kusubiri mgogoro wao.

“Ndiyo maana tunapambana kule India katika kile kiwanda kilichofanya hiyo dosari, kwanza kwa njia ya diplomasia na Ubalozi wa India tuone utatusaidiaje na Chamber of Commerce nao tuone itatusaidiaje”

Vilevile amesema si kweli kwamba sare hizo walizichapisha Dar es Salaam bali zilichapwa katika kiwanda kilichopo mji wa Canary, India.

“Januari, mwaka huu tulipewa zabuni na Talgwu baada ya ushindani mkubwa, sisi ni wageni kuingia katika hiyo zabuni, bahati nzuri nyaraka wakati tunahamisha fedha kwenda India hadi tunaleta mzigo Swissport wanatusafirishia.

“Hadi TBS wanatupitishia mzigo hadi nyaraka za watu wa forodha tunazo. Si kweli kwamba tumezitengeneza Dar es Salaam, tuna uhakika tumezichapa India mji unaitwa Canary. Tulifanya hivyo makusudi tu,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema watu wa Talgwu wamegubikwa na rushwa wenyewe kwa wenyewe ndani na walikuwa wanamtaka mzabuni wao Mhindi mmoja wampe hiyo kazi.

Amesema dakika za mwisho wakaona wamepata wao hiyo zabuni na kilichowabeba ni kitu kidogo ambacho ni ubora wa fulana na kofia.

“Sasa hao ngazi za juu huko wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Talgwu inasemekana waligombana wakitaka kumchukua huyo Mhindi na inasemekana huyo ni mtu wao wa zamani na inaonekana wananufaika naye kwa namna moja ama nyingine,” amesema na kuongeza:

“Sasa hao ngazi za juu huko naona ‘interest’ zao zikavuruga kwa sababu huyo Mhindi wao hakupata na ilivyo ni kwamba muda waliotupatia hiyo zabuni ulikuwa umekwisha na tulipata habari kwamba walikuwa Arusha huko wakatupitisha kabla ya Januari, mapema tu Desemba.

“Lakini baadaye tukaja kusikia kwamba tumeshindwa, tukasema kama ni hivyo basi haina shida, tuache na watu wa bodi ya zabuni ndio waliokuwa na ugomvi wao na dakika za mwisho Januari ndiyo tumepewa mkataba na tulitaka kuchapisha hizo fulana hapa Tanzania tukaona viwanda vingi viko, bize vina kazi nyingine.”

Kutokana na hali hiyo, amesema ndipo wakaamua kwenda kuzichapisha nje ya nchi kwa sababu wasingewahi kwa kuwa muda ulikuwa umwekwenda na wakaanza kukilipa fedha hicho kiwanda kilichopo India kama walivyosema katika nyaraka za zabuni hiyo.

Kuhusu kampuni hiyo kuwa na uwezo mdogo wa mtaji wa fedha wa kuweza kufanya kazi hiyo, amesema walipopewa zabuni hiyo waliambiwa wathibitishe uwezo wao wa kifedha na wakaziomba benki za DTB na CRDB ziwaandikie barua Talgwu kuthibitisha kwamba wanazo.

“Benki hizo ziliwaandikia barua kuthibitisha kwamba sisi tuna fedha na tukaendelea na kazi hata wakati wao wanabishana wenyewe ndani wakasema watuite kisha tuwathibitishie uwezo wetu wa mtaji wa fedha na tukafanya hivyo, wanazo barua kutoka hizo benki,” amesema.

Katika hatua nyingine, amemshangaa Nyamhokya kuwatupia lawama wao wakati mawasiliano bado yanaendelea kwa kuwa hata madai ya kuzikataa hizo fulana ni kutokana na ufito wake kukosewa, kwa kuwa uko vibaya lakini swali wanalojiuliza kwa nini zilipokewa walipozipeleka mikoani kwa wenyeviti wa Talgwu.

“Sisi kazi yetu tumemaliza na tunachofanya kwa sasa hivi ni kuandika invoice ili tulipwe fedha zetu zilizobaki,” amesema.         

Katibu Mkuu Talgwu Taifa afunguka

Awali baada ya wenyeviti wa Talgwu wa mikoa kubaini dosari, Katibu Mkuu wa Talgwu Taifa, Rashid Mtima, ameandika barua Aprili 28, 2022 kwenda kwa makatibu wake wa mikoa kuhusu ubovu wa sare uliofanywa na mzabuni.

“Kwa masikitiko makubwa napenda kuwapa taarifa kuwa mzabuni wa sare za Mei Mosi (T-shirt) kwa mwaka 2022, ameleta sare tofauti kabisa na aina (sample) aliyoagizwa na chama. 

“Chama kimesitisha kuzitumia sare hizo kwa ajili ya sherehe za Mei Mosi kwa mwaka 2022. Hili limezingatia mikataba ambayo mzabuni na chama ameingia kwa kuzingatia kifungu namba 14 cha mkataba uliosainiwa Februari 4, 2022,” amesema kupitia barua hiyo. 

Pia kupitia barua hiyo amesema baada ya kujitokeza tatizo hilo na katika kipindi kifupi kuelekea Mei Mosi, 2022 viongozi wakuu wameamua kupata sare chache 20,000 ili kusambaza mkoa unaoadhimisha kitaifa na mikoa mingine yote ipate sare katika wilaya kwa ajili ya maandamano na wafanyakazi hodari. 

“Hii inalenga kufanikisha upatikanaji wa sare katika maeneo ambayo sherehe hizi zitafanyika kwa sababu chama chetu kinaratibu sherehe hizi kwa mwaka huu kitaifa,” amesema na kuongeza: 

“Suala hili litaleta manung’uniko kwa wanachama ambao hawatapata sare, nawaagiza kuwaelekeza wanachama kuwa watulivu kwa sababu viongozi wanatambua haja ya kila mwanachama kupata sare kwa mwaka 2022. 

“Katika kipindi hiki kuelekea sherehe hizi za Mei Mosi, 2022 tuhakikishe tunasimamia ugawaji wa sare ipasavyo kwa uadilifu ili kutimiza dhamira ya kufanikisha sherehe hizi zinazotarajiwa kuwasilishwa kwenu ndani ya siku mbili tangu tarehe ya barua hii.” 

Amesema Talgwu itaendelea kumsimamia mzabuni ili haki zao kimkataba zipatikane na masilahi mapana yasipotee kutokana na changamoto iliyojitokeza.

“Maeneo yote ya uwajibikaji wa kimajukumu kwa mzabuni yatazingatiwa kwa kiwango kikubwa na kwa kuzingatia taratibu tulizojiwekea tunatarajia kufuatilia suala hili katika mchakato wote ili kuweza kubaini chanzo cha tatizo hili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa na kuhakikisha suala hili halijitokezi tena katika chama chetu,” amesema. 

Katika hatua nyingine, Gazeti la JAMHURI lilizungumza na Mtima wiki iliyopita kwa njia ya simu, pamoja na mambo mengine amesema taarifa ya mzabuni huyo kudai amehujumiwa ni mambo ya uswahili na si utendaji kazi.

“Huoni kama hizo taarifa ni uswahili? Hivi hizo taarifa ni za kiutendaji kweli? Wewe unakubali vipi kuhujumiwa? Kama hizo fulana zinatengenezwa huwezi kuona kama si unazozihitaji, hayo maneno anaweza kuzungumza mtu yeyote.

“Sisi ndio tuliozikataa hizo fulana kwa sababu zilikuwa na dosari na leo (Ijumaa) nimekaa na mawakili wangu na tunaanza kuangalia taratibu za kufanya. Unajua hujuma unaweza kumhujumu mtu ambaye hajitambui,” amesema. 

Kuhusu mzabuni huyo kutokuwa na uwezo, amesema mbona amegharamia hayo mabalo ya fulana kutoka India na yamepanda ndege?

“Wakati mwingine si uwezo wa mtaji wake kwa sababu ni mzabuni ambaye anafanya kazi nyingi hadi serikalini na inawezekana alikuwa na mtu akamuamini asiye sahihi na ndiye aliyemwingiza mkenge, ila sasa kama anaanza kusingizia amehujumiwa kwanini aruhusu hujuma?” amehoji na kuongeza:

“Biashara ni ushindani na wewe unajua na mimi wala siamini hicho kitu. Mtu gani aliyekosa zabuni halafu anakwenda kumhujumu mtu kwa maana ipi? Kwa maana siku nyingine apate yeye tena? 

“Hiyo inakuwa ni zabuni mpya, ni afadhali ujiandae na zabuni ijayo ikitangazwa kuliko kumhujumu mtu kwa sababu aliyepata si kwamba atapata tena miaka mitatu au minne mbele. Mwakani mnaweza kushindana tena katika zabuni, kama mwaka huu umeshindwa au ukishinda leo haina maana mwakani utashinda tena kwamba ili umhujumu leo ili mwakani asizingatiwe tena?” 

Aidha, amesema haamini kama kuna mtu anaweza kumhujumu kwa sababu haiwezekani kuwe na mtu wa kuwekeza nguvu za kufanya hivyo wakati ana haki ya kuomba mwakani na anaweza akapata.

Amesema wao wamezikataa hizo sare kwa kuwa zina dosari na ataanza kuzungumza jinsi gani mzabuni aliidanganya kamati yake ya ukaguzi.

Hata hivyo, amesema kuna kiwango cha mtu kumdanganya na hizo sare alivyozipeleka mikoani ilikuwa ni lazima wenyeviti wazione.

“Yeye alizipeleka fulana mikoani na zikakataliwa na huko si makao makuu na kama ulitudanganya wakati wa kukagua ukatuonyesha nzuri na tulipofika mikoani zikagundulika ni feki na zina kasoro tuna uwezo wa kuzikataa zote au baadhi hata zile 80,000 zote, kama zilikuwa mbovu tuna nafasi ya kuzikataa kwa sababu mkataba unaturuhusu.

“Ila nisingependa tufike huko, kwa sababu kulingana na taratibu zetu za ununuzi tunatakiwa kufuata taratibu zetu, yeye ameshindwa kazi na tutamwambia ameshindwa kazi,” amesema.

Pia amesema anachotakiwa kufanya mzabuni huyo ni kuwafidia fedha zao na wakishindwa katika njia za maelewano ziko taasisi zitakazowasaidia kumaliza suala hilo kwa usalama, iwe mahakamani au kwa mpatanishi.

Kuhusu malipo ya mzabuni yaliyobaki amesema chama hicho ni taasisi na ina taratibu zake na wameingia naye mikataba lakini hawawezi kumlipa mtu ambaye amekiuka taratibu za mkataba. 

Amesema mkataba wao unawaruhusu kufanya hivyo na kwa bahati mbaya zabuni hiyo imepitia katika mazingira magumu.

Amesema kwa sababu ilifika hatua sare hizo zilikuwa haziwezi kuja hapa nchini kwa njia ya meli na wakalazimika kumuwezesha ili azisafirishe kwa njia ya ndege. 

Pia amesema kwa mara ya kwanza mzabuni huyo walimlipa Sh milioni 300 kisha wakamlipa Sh milioni 400 hasa baada ya kuleta kisingizio cha usafiri wa ndege.

“Tulimlipa hizo fedha na wala haina shida na kwa kuwa kitu ulichokitengeneza kina dosari, hiyo fedha itarudi tu hata kama ni shilingi ngapi itarudi, hata kama tutakuwa tumelipa zote kwa sababu amekiuka mkataba na hata amepigwa kapigwa yeye mzabuni, siyo sisi wateja wake,” amesema. 

Aidha, amesema aliyehujumiwa ni mzabuni na wao hawawezi kuingia katika gharama za kuhujumiwa kwake na hiyo haitakuwa haki.

Kuhusu mchakato wa zabuni kugubikwa na vitendo vya rushwa, amesema kwa mujibu wa muhtasari wa vikao vyao hakuna jambo kama hilo. 

“Hakuna kwa sababu factor za zabuni ni moja na wanasema tumpe fulani kwa unafuu wa jambo fulani na bahati mbaya zabuni tuliitoa muda ulishapita lakini mwisho yeye ndiye aliyepewa.

“Hayo maneno anayosema kwamba tuna mambo ya rushwa nilitarajia niyapate kutoka kwa mtu aliyekosa zabuni, yeye amepata anasemaje hivyo au yeye alitoa ndiyo maana akapewa?” amehoji. 

Kuhusu kwa nini zabuni za sare za Mei Mosi zinakuwa na migogoro kila wakati, amesema ni kwa sababu katika chama hicho wanatumia gharama kubwa zaidi kuliko kitu chochote.

“Tunatumia fedha nyingi kununua sare za Mei Mosi na unavyotuona tuko imara ni kwamba tumezingatia taratibu na kuna hatua zilichukuliwa kwa wafanyakazi mwaka juzi na lazima nisimame imara kusimamia taratibu kama kiongozi,” amesema na kuongeza: 

“Huwezi kujua kwa sababu hao wanaokuwapo katika zabuni na mimi kama kiongozi lazima nisimamie taratibu ziende, kelele za watu ni lazima kwa sababu hii ni zabuni kubwa kuliko zote ndani ya chama. Hata wazabuni kuwatipu ni kitu cha kawaida lakini baada ya hapo tunatokaje? Taratibu zinafuatwa na mwisho mnatoka na kitu kizuri?

“Na si mtu amekwenda huko amefeli halafu anasema mambo ya rushwa, kwa hiyo asiichafue taasisi yangu na huu ni mwaka wa sita nasimamia ununuzi wa fulana na yeye ndiye aliyekuja kutuangusha mwaka huu.”

Katika hatua nyingine amesema sare hizo zinapokewa mikoani lakini wanaunda kamati ya ukaguzi japo haizikagui sare moja baada ya nyingine katika mabalo zaidi ya 100 ila zilizokaguliwa ni zile zilizoonekana ni nzuri.

“Huwezi kuzikagua zote, unaweza kuzikagua mbili tatu tu na utajiridhisha kisha utaandika ripoti na ukweli ni kwamba huwezi kumdanganya binadamu, leo utamdanganya mtu ataandika ripoti nzuri na anayekwenda kuzivaa akiziona mbovu? 

“Itakuwa ni akili ya hovyo kusema watu watatu wanaona ziko poa wakati zinakwenda kuvaliwa na watu elfu 70,” amesema.

Kuhusu hatua za kuchukuliwa, amesema ipo miongozo, kuna mkataba, nyaraka za zabuni alizonunua na watakaa na kamati yake wakiwamo wanasheria na maofisa ununuzi, wataanza kuchukua hatua zaidi.

Amesema fedha alizolipwa mzabuni kwa mujibu wa mkataba hazikuwa kwa asilimia bali zilikatwa katika mafungu kuanzia Sh milioni 400 kisha Sh milioni 300 na malipo ya mwisho alikuwa analipwa Julai, 2022 na licha ya kwamba mzigo wa sare alikuwa ameuleta Mei, 2022.

Amesema fedha iliyobaki ni karibu Sh milioni 400 ambayo ni karibu theluthi moja na hata kama angekwenda mzabuni huyo angekwenda vizuri, angewapa sare hizo kisha angewadai.