DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Juni 27, 2004 nilifanikiwa kukutana na Peter Greenberg, mtayarishaji wa kipindi cha televisheni cha ‘The Royal Tour’ na kuzungumza naye mambo mengi kuhusu kipindi hicho na uzoefu wake kama mwanahabari, ‘producer’ wa utalii duniani kwa miaka mingi kwenye Shirika kubwa la CBS, Marekani.
Nimshukuru Balozi wa Marekani aliyenialika kwa mapokezi mazuri na ukarimu wake pamoja na wafanyakazi wa ubalozi.
Nimepata nafasi ya kuzungumza na maofisa kadhaa kwenye dawati la utamaduni ubalozini hapo.
Amani yetu, mtaji wetu
Greenberg alitangulia kwa kusema kuwa anaiona Tanzania kama nchi nzuri yenye Amani, na la msingi amesema ni nchi inayoruhusu mazungumzo.
Watu kuzungumza amesema ni jambo la msingi na la kistaarabu. Jana (wiki iliyopita) tuliona vipande vilivyochaguliwa na si sinema yote, kwa sababu ya muda. Lakini pia kupisha mazungumzo baina ya waalikwa na mtayarishaji.
Kwa msingi huo siwezi kufanya uchambuzi wa maudhui ya filamu hiyo kitaalamu.
Kikwete, Magufuli waliombwa
Peter amesema alijaribu kutengeneza filamu hii nchini kwa miaka mingi kuanzia kipindi cha Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikubali kushiriki ingawa wasaidizi wake hawakupenda.
Amesema alimjaribu Rais Dk. John Magufuli, lakini hakuvutiwa kushiriki. Ametuhabarisha kuwa kipindi hiki cha televisheni kilianza mwaka 2000 wakati Mfalme Abdullah wa Jordan alipokubali kushiriki.
Hadhira
Kipindi cha ‘The Royal Tour’ kitaonyeshwa katika chaneli 350 duniani. Filamu hii imepata onyesho maalumu la kwanza (premiered) huko Marekani kisha kufuatiwa na ‘streaming’, halafu itaonyeshwa Tanzania kwa kuanzia Arusha, Zanzibar halafu Dar es Salaam.
Mfululizo wa vipindi hivi utakuwepo kwenye mtandao kwa miaka mingi ijayo na kuangaliwa na watu wengi zaidi.
Peter amesema amewapa rekodi zote zikiwamo ambazo hazikuingizwa kwenye vipindi (yaani ‘raw footage’) Wizara ya Maliasili na Utalii waweze kuzitumia.
Fedha za kutengenezea zimetoka wapi?
Aprili 28, jijini Arusha, Rais Samia amefafanua kuwa fedha zote zilizotumika katika utengenezaji na utayarishaji wa filamu hii zimetokana na wafanyabiashara mbalimbali ndani na nje ya sekta, tofauti na tulivyofikiri mwanzoni kuwa mashirika kama TANAPA, NCAA, TTB, TAWA na TFS yalichangia gharama.
Hii ilichangiwa na barua ya Aprili 18, mwaka huu iliyoandikwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu iliyoyatambua mashirika haya yaliyopeleka wawakilishi kwenye uzinduzi Marekani kama ‘wafadhili’.
Kwa upande mwingine, nchi yetu imewekeza na ni mzalishaji hivyo asilimia fulani ya mapato yatokanayo na uuzwaji, fedha za leseni ya filamu hii tunapaswa kufaidika nayo.
Swali nisiloweza kulijibu ni kuwa, je, jambo hilo liko kimkataba?
Utalii wa utamaduni
Alipoulizwa swali kuhusu utalii wa utamaduni (cultural tourism), Peter alisema hakuna utalii bila utalii wa utamaduni, akasema wageni wengi wanaokuja kutalii ni wenye akili na wakisha kuangalia vivutio, hutaka kujua maisha ya watu na tamaduni zao.
Kwa nini hatuzalishi filamu kutumia vivutio tulivyonavyo?
Nilipomuuliza juu ya nini kifanyike ili Watanzania waanze kutengeneza filamu kwa kutumia vivutio vyetu ambavyo kwa sasa vinatumiwa na wageni na kuhusu soko la filamu hizo duniani, alisema kitu cha msingi ni kueleza hadithi na mambo yenu (tell your own story).
Akaongeza kuwa soko lipo tena kubwa sana na kwamba ni muhimu kulidhibiti soko, yaani kudhibiti idadi ya watalii ili kusiwe na uharibifu na utalii uwe wa kudumu (sustainable).
Miundombinu ya uzalishaji
Nilipomuuliza Peter kuhusu suala la uzalishaji wa kazi bora za filamu, alisema kwa kurudia: “Jengeni studio za uzalishaji zenye ubora.”
Aliposema hivi, niliikumbuka miundombinu ya filamu nchini, moyoni nilijisemea tu: “Hajui nchi nzima hii tuna majumba 11 tu ya filamu yanayofanya kazi.”
Kubakiza ujuzi
Kwenye eneo la ujuzi, amesema kuwa ‘ The Royal Tour’ imeshirikisha Watanzania (local crew) katika uzalishaji wake kwani watu tisa katika ‘crew’ ya watu 43 walikuwa Watanzania.
Si haba, kwani hii ni karibu asilimia 30! Siku za usoni ni muhimu jambo hili liwe la kisheria kuhakikisha ipo ‘kwota’ ya watu wetu katika kila uzalishaji wa filamu utakaofanyika nchini ili kupata ujuzi.
Wapi Bodi ya Filamu?
Kwa mtazamo wangu tangu shughuli hii ya kutengeneza filamu ianze, inaonekana wazi kuwa Bodi ya Filamu haikushirikishwa kikamilifu na kama walishirikishwa ni kwa uhafifu sana.
Inasikitisha kuona hawaonekani kwenye hatua nyingi ikiwamo kwenye uzinduzi wa Marekani.
Kama tuliwapeleka TANAPA, NCCA, TTB, TAWA na TFS, tungewapeleka pia ‘Tanzania Film Board’! Hii naisema kwa kuwa tulipeleka watu wengi Marekani. Ni muhimu siku za usoni washirikishwe ili kuwajengea uwezo.
Wakati vijana wetu hapa ndani wanabanwa na masharti haya, filamu hii ilipewa ‘njia ya mwendokasi’ kwani haikuwasilisha andiko la muswada (script) wala ‘raw footage’ kabla ya umaliziaji wake kama sheria inavyotaka.
Binafsi sizipendi sheria hizi kwani si rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje. Basi tuzirekebishe.
Ninafahamu wizara na Bodi ya Filamu wamo katika harakati ya kuandika kanuni upya.
BASATA
Basata pia hawakushirikishwa. Utengenezaji wa filamu una asilimia 80 ya wataalamu wa sanaa za uoni (visual arts).
Kama tunakubali kuwa utalii wa utamaduni ni sehemu nyeti ya utalii, basi Baraza lina nafasi ya kipekee ya kushiriki, hivyo nafasi ya Basata ni ya msingi, hasa katika kujifunza na kuweka kumbukumbu, lakini pia kuingiza katika mipango yao.
Tukumbuke Basata ndiye msajili wa wasanii wote na hata mama ajitayarishe kwenda kusajiliwa huko.
Kushirikisha vyombo hivi kikamilifu pia kunasaidia kuandikwa kwa ripoti mbalimbali ambazo zingesaidia kuongoza utafutaji masoko, utungaji sera, kanuni na sheria.
Biashara kwanza, siasa baadaye
Kwa nchi ya siasa mbele kama Tanzania, changamoto kubwa ni kuifanya Royal Tour kuwa jambo lenye lengo la kibiashara na kiutalii badala ya jambo la kisiasa.
Tunaona kuwa kwa sasa baadhi ya vyombo vyetu ‘vinaliuza’ jambo hili kama la kisiasa zaidi, vyombo hivi huchukua muda mwingi kumsifia Rais Samia.
‘Royal tour isn’t about Samia, but advertising what Tanzania has to offer to the world!’
Nimeona viongozi wengi wakipita kwenye vyombo vya habari wakidai: “Tukae mkao wa kula kwani baada ya ‘Royal Tour’ Tanzania itapata watalii wengi sana.”
Dhana hii si sahihi, kwani bidii kubwa inahitajika kwenye maeneo mengi kuwavuta watalii.
Rais Samia amefanya kazi yake, sasa unapoongea na hadhira ya ndani kwa lengo la kukuza utalii wa ndani husemi; “mama kaupiga mwingi” bali unaoanisha bidhaa (products) mbalimbali kama wanyama, uzuri wa maeneo, ngoma na maajabu yaliyomo katika nchi yetu kimkakati ili kuvutia Watanzania kwenda kuyaona maajabu hayo.
Peter ametamka jana kuwa serikali nyingi duniani hazifanyi vizuri katika kuvutia watalii, kwa hiyo watu wa nchi wana nafasi nzuri ya kufanya kazi hiyo.
Chapa
Kwa mtazamo wangu, nafikiri hatutakiwi kulipa chapa (branding) jina ‘The Royal Tour’ kwani hizi ziko nyingi, bali ‘Tanzania Royal Tour’.
Tukumbuke kuwa kwa dizaini, ‘The Royal Tour’ imetengenezwa kuvutia watalii wa nje na si wa ndani, hivyo nguvu ielekezwe huko. Balozi zetu na taasisi za utalii zinaweza kushiriki vema.
Kunani kusini?
Peter amekubali kuwa hakwenda kabisa kwenye eneo la kusini mwa nchi yetu bali ameishia kaskazini (northern circuit).
Kwa maoni yangu huku kusini si tu kuna vivutio vizuri bali maeneo aliyokwenda ya kaskazini si mageni kwa watalii duniani, haya yameishatangazwa sana siku za nyuma.
Ingependeza kama angekwenda pia kufukua tamaduni na maisha, mbuga na makabila ya kusini kama Wamakua, Wangoni, Wamakonde, Wanyakyusa na wengineo na hili lingechangia kuleta jambo jipya katika sinema hii.
Mkakati wa kitaifa
Muhimu sasa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikishirikiana na Wizara ya Utalii na wadau wakakaa kuona jinsi gani watatengeneza mpango wa kitaifa wa utalii wa kiutamaduni (cultural tourism).
Hatuna sera, mikakati ya filamu
Muhimu pia kupitisha sera ya filamu, sera ya miliki bunifu na kuandika sheria mpya ya filamu kwani iliyopo ni ya mwaka 1976!
Baadhi ya wanaoshangilia mama ‘kuupiga mwingi’ ndio hao wamekuwa kikwazo katika kuboresha sekta ya filamu iliyojaa wizi (piracy) mkubwa tena wa waziwazi kabisa nchini.
Hitimisho
Mwisho, ‘Tanzania Royal Tour’ inaelekea kufanikiwa katika hatua hii ya pili baada ya uzalishaji, lakini siku za usoni tusifanikiwe kwa kubahatisha.
Kwa nini? Kwa sababu mpaka sasa vyombo vyetu hasa vya sanaa havina mpango mkakati. Bodi ya Filamu, wizara na Basata hawana mipango ya kimkakati.
Mbele ya safari tusisubiri ‘Peter’ mwingine aje na mradi kisha nasi turuke naye tukishangilia kwa vigelegele.
Tutengeneze mpango mkakati wetu wa miaka mitano na kuwepo mahala panapozungumzia uwekezaji kutoka nje katika filamu.
Tunajua serikali imo mbioni kuandika sera ya uwekezaji, ni vema ikumbuke kuandika yahusuyo katika filamu na sanaa kwa ujumla.
Mwandishi wa uchambuzi huu, Robert Mwampembwa, ni msanii, mwandishi na mkurugenzi wa Taasisi ya Mtandao wa Sekta Bunifu Tanzania (CINT).