DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Waliokuwa wafanyakazi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati na kuwasaidia ili uongozi uwape haki zao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake zaidi ya 1,000, mmoja wa wastaafu hao, Charles Masanduku, amesema uongozi wa TRL umewazungusha kwa muda mrefu sana kuwapatia mafao yao.
“Kitendo cha Mkurugenzi Masanja Kadogosa kutotulipa kwa wakati kimetuchosha na kutuondolea uvumilivu tuliokuwa nao. Huu si ubinadamu hata kidogo,” amesema Masanduku.
Masanduku amesema uongozi wa TRL unafanya mambo tofauti na maelekezo ya Rais anayeyataka mashirika yote kuwalipa wastaafu ndani ya muda mfupi.
“Mimi nilikuwa mfanyakazi wa TRL tangu mwaka 1977 hadi nilipostaafu mwaka 2015. Lakini tangu nilipostaafu sijapata malipo kama tuzo ya kustaafu. Pamoja na wenzangu tumekwenda mahakamani kudai haki zetu na mara zote tunashinda kesi. Lakini mkurugenzi hatupi haki zetu,” amesema Masanduku.
Amesema kikwazo kikubwa ni mkataba na Kadogosa kukosa utashi wa kuwasaidia.
“Ni Kadogosa ndiye anatufanya tuishi maisha magumu. Sijui anapata wapi mamlaka ya kufanya hivi? Ndiyo maana tunaomba Rais atusaidie,” amesema.
Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli (TRAWU), Elias Chizigwi, amesema mgogoro huo ni wa muda mrefu na umekuwa ukipitia hatua mbalimbali.
“Mwishowe tulifikia makubaliano ya malipo, lakini mkurugenzi amekuwa akikataaa bila sababu za msingi. Madai tuliyonayo kwa sasa ni tuzo za kustaafu na mishahara,” amesema.
Chizigwi amesema jitihada za TRAWU zimefanikisha malipo kwa wastaafu 60 huku maelfu wakizungushwa na menejimenti ya TRL.
“Mashirika mengi ya umma yameitikia wito wa Rais kwa kuwalipa wastaafu tofauti na ilivyo kwa TRL ambako kumekuwa na danadana nyingi kutoka mwaka 2012,” amesema.
Mwenyekiti wa TRAWU, Sudi Waziri, amesema shauri la wastaafu na TRL lipo Tume ya Usuluhishi (CMA).
Amesema kilichowashangaza TRAWU ni uamuzi wa TRL badala ya kufuata makubaliano yaliyowekwa mahakamani, wakamwomba Mwanasheria Mkuu (wa Serikali) aingilie kati ili shauri lipelekwe Mahakama ya Kazi.
“Mahakama ya Kazi ikadai kwamba mkataba uliotumika CMA uliisha muda na haukusainiwa na Mwenyekiti wa Bodi. Hayo yote yapo na yalikuwa chini ya mamlaka ya mkurugenzi.
“Baada ya hapo hakujafanyika utekelezaji wowote ndipo wastaafu wakarudi mahakamani kukazia hukumu ya kesi namba 31/2021. Tayari hukumu imetoka Aprili 1, 2022 ikielekeza TRAWU kutengeneza mkataba upya ili wastaafu walipwe ndani ya siku 60,” amesema.
Waziri ameiomba TRL kufanya malipo hayo haraka kabla ya Mei 30, 2022 kwa kuwa wengi kati ya wastaafu hao wanaishi maisha magumu huku wengine tayari wamekwisha kufariki dunia.
JAMHURI limezungumza na Kadogosa anayesema hayupo tayari kulizungumzia suala hilo kwa kuwa lipo mahakamani.