DAR ES SALAAM
Na Andrew Peter
Mtetemo wa Mayele ndio ‘trendi’ ya jiji, mashabiki wa Yanga wanataka kuona, wale wa Simba hawataki. Hiki ndicho kitendawili kinachosubiri jibu Jumamosi hii wakati vinara wa Ligi Kuu watakapowakaribisha watani wao wa jadi, Simba, kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mshambuliaji Fiston Mayele amejijengea umaarufuu kwa aina yake ya ushangiliaji wa kupiga mkono wake mara tatu, anapiga kichwa mbele mara tatu kabla ya kutanua mabega na kutingishika kama mtu anayetetemeka huku akienda mbele.
Mshambuliaji huyo raia wa Kongo alikonga nyoyo za mashabiki wake alipofunga bao katika mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, na hapo ndipo ushangiliaji wake wa kutetema ulipojizolea umaarufu nchini.
Mbali ya sifa hiyo, Mayele ndiye kinara wa ufungaji mabao katika Ligi Kuu akiwa amezifumania nyavu mara 11, jambo linalofanya safu ya ulinzi ya Simba kuwa na kazi ya ziada kumzuia.
Hata hivyo, Mayele anakwenda katika mchezo huo akiwa na kumbukumbu mbaya ya kushindwa kufurukuta mbele ya ngome ya Simba chini ya Henock Inonga na Joash Onyango katika mchezo wa kwanza wa ligi.
Wakati Mayele anatolewa nje dakika ya 86 ya mchezo huo, Inonga alimsindikiza huku akijigamba kwamba amemaliza kazi, hakuna kutetema mbele yake.
Jambo hilo litamfanya Mayele kwenda uwanjani kwa lengo moja tu; kuhakikisha anazifumania nyavu za Simba na kuwapa kile wanachosubiri kuona mashabiki wa Yanga, wakati Inonga atakuwa na jukumu la kuthibisha kwamba yeye ni beki bora na hakubahatisha kumdhibiti.
Vita ya viungo ‘wasioonekana’
Sahau kidogo kuhusu Mayele na Inonga; utamu wa mechi ya watani Jumamosi hii utakuwa katikati ya uwanja wakati viungo ‘wasioonekana’ wa timu hizo watakapokuwa na majukumu ya kutaka kutawala mpira.
Tangu Kocha Nabi aichukue Yanga, imebadili uchezaji wake ikitumia pasi nyingi za chini, aina ya uchezaji unaopendwa zaidi na Simba, jambo linaloonyesha kuwa muda mwingi mpira utachezwa katikati ya uwanja huku ukitawaliwa na ubabe, viatu na ufundi wa kuchezea mpira.
Yanga watakuja na mfumo wa 4-5-1. Safu ya kiungo itaongozwa na ama mkongwe kutoka Uganda, Khalid Aucho, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Zawadi Mauya, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Yannick Bangala, Saido Ntibazonkiza, Farid Musa au Jesus Moloko.
Simba wataingia na mfumo wa 3-4-3 wakiwa na viungo wakabaji watatu; Jonas Mkude, Taddeo Lwanga na Sadio Kanoute. Juu watakuwapo mkongwe Clatous Chama, chipukizi Pape Sakho na Bernard Morrison; mshambuliaji akianza na Meddy Kagere au Chris Mugalu.
Aucho vs Lwanga
Aucho ‘Daktari wa Mpira’. Mganda huyo amepewa sifa hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutumia mguu wa kushoto kuchezesha timu kwa kutoa pasi za uhakika na kuituliza timu.
Kiungo Aucho atakuwa na kazi kubwa ya kutimiza majukumu yake akiwa chini ya ulinzi wa Mganda mwenzake, Injinia Lwanga mwenye sifa kubwa ya kuharibu mipango ya timu pinzani.
Lwanga si kipenzi cha mashabiki kwa aina yake ya uchezaji, lakini amekuwa akifanya kazi kubwa ya kuilinda ngome ya Simba, jambo linalofanya mara kadhaa kupata kadi za njano.
Bangala v Chama
Kiungo mkabaji Bangala ‘Mzee wa Kazi Chafu’ jukumu lake kubwa litakuwa ni kuhakikisha Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ hapati muda wa kukaa na mpira na kutengeneza nafasi kwa washambuliaji wa Simba.
Hakuna ubishi, ushindani wa Mkongo huyo na Mzambia ni jambo litakalovutia zaidi kutazamwa na mashabiki hasa kutokana na aina yao ya uchezaji.
Mauya/Fei Toto v Mkude/Kanoute
Yanga inaweza kuanza na Mauya au Fei Toto. Wote wana uwezo wa kukaba na kuanzisha mashambulizi, lakini moto utawaka watakapokabiliana na akina Mkude au Kanoute wenye sifa zinazofanana nao.
Unataka kuona jinsi wachezaji wanavyocheza kwa majukumu waliyopewa na makocha wao? Basi watazame vijana hao wanne watakavyokuwa wakiwasha moto wa ushindani mkubwa wala usishangae ukiona wanapewa kadi za njano au mwamuzi kuwa mkali zaidi kwao.
Mayele, Kagere wana jambo lao
Yanga wamefunga mabao 33 huku wakiruhusu wavu wao ukitikishwa mara tano tu; wakati Simba wamefunga mabao 23 na kuruhusu mabao saba.
Mayele ni kinara wa ufungaji kwa Yanga akiwa na mabao 11 akifuatiwa na Saido Ntibazonki (6) wakati mkongwe Kagere pamoja na kutokuwa na namba ya kudumu katika kikosi cha Simba, kwa sasa ndiye anayeongoza kwa ufungaji akiwa na mabao saba.
Hakuna ubishi kwamba Mayele ataiongoza Yanga huku Kagere akiwa na jukumu la kuibeba Simba katika mchezo huo muhimu.
Miaka 45 ya rekodi iliyotukuka ya King Kibadeni
Mkongwe Abdallah ‘King’ Kibadeni ‘Mputa’ anapaswa kuingia katika kitabu cha kumbukumbu za dunia, Guinness, akiwa mchezaji pekee hadi sasa aliyefunga mabao matatu katika mechi moja ya watani wa jadi.
Rekodi hii haijavunjwa kwa miaka 45 sasa.
Kibadeni alifunga mabao hayo Julai 19, 1977, wakati Simba wakiichakaza Yanga mabao 6-0. Siku hiyo Kibadeni alifunga katika dakika ya 10, 42 na 89, huku Jumanne Hassan ‘Masimenti’ akifunga mawili dakika ya 60 na 73. Bao la kujifunga ka beki wa Yanga, Selemani Sanga, likafanya idadi hiyo ya mabao sita kwa Simba.
Swali limebaki nani ataivunja rekodi hii kati ya nyota wa sasa wa Yanga na Simba? Tusubiri tuone.
Aprili ya moto kweli
Namba hazidanganyi, rekodi zinaonyesha mwezi huu umetawaliwa na sare kuliko ushindi, hivyo mashabiki wanapokwenda uwanjani wajiandae kwa lolote.
Yanga na Simba tangu mwaka 1982 hadi sasa zimekutana mara 11 Aprili, zikitoka sare mara tano huku kila timu ikishinda mechi tatu tu, hivyo mchezo wa Jumamosi hii utakuwa wa 12 kwa wakongwe hawa.
Ushindi mkubwa kwa Yanga ulikuwa Aprili 16, 1983, iliposhinda 3-1 kwa mabao ya Charles Boniface Mkwasa ‘Master’, Makumbi Juma ‘Homa ya Jiji’ na Omar Hussein, wakati bao la Simba likifungwa na ‘Super’ Kihwelu Mussa.
Simba walijibu mapigo kwa ushindi mnono wa 4-3 mwaka 2010; mabao yaliyofungwa na Uhuru Suleiman, Musa Hassan ‘Mgosi’ na mawili ya Hillary Echesa, wakati ya Yanga yakifungwa na Athumani Idd na mawili ya Jerry Tegete.
Rekodi ya Aprili
APRILI 29, 1982: Yanga 1-0 Simba
APRILI 16, 1983: Yanga 3-1 Simba
APRILI 30, 1988: Yanga 1-1 Simba
APRILI 12, 1992: Yanga 1-0 Simba
APRILI 26, 1997: Yanga 1-1 Simba
APRILI 17, 2005: Simba 2-1 Yanga
APRILI 27, 2008: Simba 0-0 Yanga
APRILI 19, 2009: Simba 2-2 Yanga
APRILI 18, 2010: Simba 4-3 Yanga
APRILI 19, 2014: Simba 1-1 Yanga
APRILI 29, 2018: Simba 1-0 Yanga
APRILI 30, 2022: Yanga V Simba