TANGA

Na Mwandishi Wetu 

Bandari ya Tanga ni miongoni mwa bandari kongwe hapa nchini. Bandari ya Tanga ilianza kujengwa mwaka 1888 na kukamilika mwaka 1891 ikijulikana kwa jina la Marine Jetty.

Bandari ya Tanga ni ya kwanza kutoa huduma Afrika Mashariki huku ujenzi wake ukichagiza maendeleo ya njia nyingine za usafirishaji, hasa ujenzi wa mtandao wa reli katika eneo hilo.

Pia gati la kwanza katika Bandari ya Tanga lilijengwa mwaka 1914, na la pili lilijengwa mwaka 1954. Kwa sasa ina gati mbili zenye urefu wa mita 450 zinazofanyiwa maboresho makubwa kupitia miradi inayoendelea.

Kwa mujibu wa Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha, bandari hiyo ina ukubwa wa hekta 17 na inajumuisha eneo la Mwambani lenye hekta 176 na Chongoleani lenye hekta 207.

Mrisha anasema bandari hiyo inafanya kazi nangani, kwa maana ya kupakua na kupakia mzigo melini (Stream Operations) kwa umbali wa mita 200 na kabla ya maboresho ilikuwa inafanya kazi umbali wa kilomita 1.7 kutoka gatini hadi meli inapotia nanga, hali ambayo bado inaongeza gharama za uendeshaji kwa kuhudumia shehena mara mbili (double handling), ingawa imepunguza kidogo gharama za mafuta.

Aidha, anasema bandari hiyo inasimamia bandari nyingine nne ndogondogo ambazo ni Pangani, Kipumbwi, Sahare na Mkwaja.

Anasema Mkoa wa Tanga una bandari zisizo rasmi (bubu) takriban 50 zilzobainishwa katika maeneo mbalimbali.

Anazitaja baadhi ya bandari hizo kuwa ni Buyuni Kuu, Chingwe, Kiwavu, Kwale Moa, Mundura, Sadani, Tongoni, BomaNdani, Kasera, Chongoleani, Gawani, Kichalikani, Kwa Makofia, Mwera na Monga.

“Kabla ya maboresho, kina cha maji gatini kilikuwa ni mita tatu (kina cha asili), wakati lango la kuingilia meli lilikuwa na kina cha kati ya mita tatu hadi tano.

“Huduma za meli za kimataifa (Deep Sea) zilikuwa zinafanyika nangani umbali wa kilomita 1.7 kutoka gatini na bandari hiyo ilikuwa na uhaba mkubwa wa mitambo na vifaa vya kuhudumia meli na shehena,” anasema.

Kwa masoko ya ndani, anasema bandari hiyo inahudumia mikoa ya Kanda ya Kaskazini ambayo ni Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

Aidha, kwa masoko ya nje, anasema kutokana na nafsi yake kijiografia ina fursa ya kuhudumia nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Malawi zinazopakana na Tanzania kupitia mpaka mmoja (Single Boarder Point).

Kuhusu utendaji kazi wa bandari hiyo, anasema shehena kuu zinazosafirishwa kwenda nje ya nchi ni katani, mbao, kahawa, macadamia, saruji pamoja na bidhaa za chakula zinazosafirishwa kwenda visiwani Pemba na Unguja.

Pia anasema shehena kuu zinazopokewa ni clinker, makaa ya mawe, malighafi za viwandani, vipuri, vifaa vya ujenzi, mafuta na gesi na kuanzia mwaka 2000 inakua kwa wastani wa asilimia 8.7.

Uboreshaji Bandari ya Tanga

Mrisha anasema serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari ya Tanzania (TPA) imefanya maboresho makubwa katika Bandari ya Tanga ili iweze kuchangia kikamilifu kukuza pato la taifa kwa kuhudumia wateja wa ndani na nchi jirani zinazotegemea bandari za Tanzania kusafirisha bidhaa kutoka na kwenda nje ya nchi.

Katika uboreshaji wa bandari hiyo, anasema TPA ilianza kwa kutekeleza miradi miwili ya kimkakati yenye thamani ya Sh bilioni 429.1 na imetekelezwa na Kampuni ya China Harbor Engineering Company katika awamu kuu mbili.

“Awamu ya kwanza imehusisha kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia na sehemu ya kugeuzia meli kutoka kina cha maji cha mita tatu hadi mita 13, pamoja na ununuzi wa mitambo na vifaa vya kuhudumia meli na shehena. 

“Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 172.3 ulianza kutekelezwa Oktoba, 2019 na unatarajiwa kukamilika Aprili, 2022 baada ya kuongezewa muda kutokana na changamoto ya Uviko-19, hasa katika uzalishaji na usafirishaji wa mitambo iliyoagizwa,” anasema.

Katika hatua nyingine, anasema kazi za kuongeza kina na upana wa lango la kuingilia na sehemu ya kugeuzia meli pamoja na kuweka vifaa vya kuongozea meli zimekamilika kwa asilimia 100 na kutumia jumla ya Sh bilioni 111.42.

“Kwa ujumla, awamu ya kwanza imekamilika kwa asilimia 95 na asilimia tano iliyobaki ni ununuzi wa mitambo ya kupakia na kupakua shehena na kati ya mitambo 16 iliyopangwa katika mradi, 10 imewasili na inatumika,” anasema.

Kuhusu awamu ya pili, anasema inahusisha uboreshaji wa gati mbili zenye urefu wa mita 450 kwa gharama ya Sh bilioni 256.8.

Anasema mradi huo ulianza kutekelezwa Desemba, 2020 na unatarajiwa kukamilika Oktoba, 2022 na hadi sasa utekelezaji wa jumla wa mradi umefikia asilimia 29.

Miradi ya Bandari ya Tanga

Mbali na maboresho yaliyoelezewa awali, anasema serikali kupitia TPA imetekeleza miradi mingine ambayo ni uwekaji wa miundombinu wezeshi kwa ajili ya Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda.

Miradi mingine ni ukarabati mkubwa wa maghala na sehemu ya kuhudumia shehena na usimikaji wa mita za kupima mafuta (flow meters).

Pia anaitaja miradi mingine inayotekelezwa kuwa ni maandalizi ya miundombinu wezeshi kwa ajili ya Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda na tayari serikali kupitia TPA imetwaa ardhi (hekta 200) itakayotumika kujenga miundombinu ya gati la mafuta hayo.

Vilevile anasema ununuzi wa mitambo ya kuhudumia meli kubwa zitakazotumika kusafirisha mafuta ghafi unaendelea na TPA inashiriki kikamilifu katika hatua za utekelezaji wa mradi huu kupitia Kamati ya Kitaifa.

Si hivyo tu, pia anasema bandari hiyo imefanya maboresho makubwa hasa katika maeneo ya kuhifadhi mizigo (sheds) na maghala matatu yenye ukubwa wa mita za mraba 34,686 yamekarabatiwa.

Anasema ukarabati wa maghala hayo uliokwenda sambamba na ukarabati wa jengo la abiria, kantini, uzio, mnara wa kuongozea meli na ujenzi wa sakafu ngumu vyote vimegharimu Sh bilioni 4.85.

Kuhusu usimikaji wa mita za kupima mafuta, anasema serikali imezinunua na kuzisimika za kisasa katika bandari hiyo na mradi huo umefanywa na Ofisi ya Rais na zina uwezo wa kupima tani 520 za mafuta yanayopakuliwa kwa saa.

Huku gati ya kuhudumia shehena ya mafuta, anasema ina mabomba makubwa matatu yenye kipenyo cha inchi 12 yanayosafirisha aina tatu za mafuta ambayo ni petroli, dizeli na mafuta ya ndege. 

Kuhusu matarajio ya bandari hiyo anasema iwe na uwezo wa kuhudumia meli zenye kina kirefu gatini tofauti na sasa meli hizo zinahudumiwa nangani (stream operation). 

Anasema kwa sasa bandari hiyo inahudumia shehena kiasi cha tani 750,000 za uzito na matarajio yao baada ya maboresho hayo ni kuongeza uwezo wa kuhudumia hadi tani milioni tatu za uzito.

Pia anasema matarajio yao ni kupunguza gharama za uendeshaji pamoja na kuvutia wamiliki wa meli na wateja wanaotaka kufanya biashara kupitia bandari hiyo na kwa ujumla ushindani wao katika soko la Afrika Mashariki na Kati utaboreshwa.

Anasema serikali kupitia TPA inakusudia kuiboresha bandari hiyo ili kuondokana na changamoto ya kina kifupi, kuhudumia meli nangani na kuwezesha kupatikana kwa meli za moja kwa moja bandarini hapo (direct calls).

Anasema TPA inakusudia kuifanya bandari hiyo iweze kuhudumia kwa asilimia 100 soko la mikoa ya kaskazini ikiwamo Kilimanjaro, Arusha, Manyara na za Rwanda, Burundi, DRC na  Uganda hasa baada ya kukamilika kwa maboresho yanayoendelea na watahudumia tani milioni tatu.

Bodi ya TPA yaridhishwa

Katika hatua nyingine, Bodi ya Wakurugenzi ya TPA imeridhishwa na kazi inayoendelea ya ujenzi wa bandari hiyo na kutaka ikamilike kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu.

Akizungumza wakati wakikagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo hivi karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TPA, Balozi Ernest Mangu, anasema kukamilika kwa ujenzi huo kutakuwa ni kutekeleza dhamira ya serikali ya kufungua mikoa ya kaskazini na nchi jirani kupitia bandari hiyo.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Masoko wa TPA, Nicodemus Mushi, anasema awamu ya kwanza ya miradi miwili inayofanyiwa kazi katika bandari hiyo umefikia asilimia 98 na ukikamilika itahudumia makasha 20,000 na abiria 99,000.