Kwa zaidi ya wiki tatu sasa tumekuwa tukipokea malalamiko kutoka kwa wananchi wanaoishi pembeni mwa Ziwa Victoria, wakilalamika kuhusu kukithiri kwa uvuvi haramu.
Malalamiko hayo ambayo kwa namna fulani tumeyathibitisha, yanatoka kwa raia wema waliopo mwambao wa ziwa hilo, hasa wanaoishi ndani ya makumi ya visiwa.
Raia mwema wa kwanza kuleta malalamiko hayo anaishi katika Kisiwa cha Bumbile, Muleba mkoani Kagera. Yeye alitaja hata majina ya watu wanaofumbia macho uvuvi haramu wilayani mwake.
Gazeti la JAMHURI likaamua kuzungumza na wakazi wa mikoa ya Geita, Mwanza na Mara wanaojishughulisha na uvuvi, wachuuzi wa kawaida wa samaki na wale wavuvi wa kiwango cha kati wanaouza samaki viwandani.
Tuliyoyasikia na kuyashuhudia huko ni makubwa na yanatisha. Hali ni mbaya na serikali lazima iingilie kati. Idadi ya samaki imepungua kwa kiwango kikubwa na kuwatia hofu wananchi; jambo lililothibitishwa na wataalamu kutoka taasisi ya serikiali ya TAFIRI.
Yapo mengi tunaendelea kuyafanyia kazi na ndani ya wiki mbili hivi tutayaweka hadharani. Si kwa nia mbaya, hapana. Ila kwa nia moja tu; kusaidia kuwasemea wasio na uwezo wa kusema na kusikika ili kuliokoa Ziwa Victoria.
Huenda maeneo pekee salama yaliyosalia kuwa ya amani kwa samaki na viumbe hai wengine ni yale yanayozunguka visiwa vya Saanane na Rubondo, kwa kuwa yapo chini ya TANAPA. Ingawa ukweli ni kwamba nayo yamekuwa yakivamiwa mara kadhaa na wavuvi haramu.
Wananchi wanalalamika kwamba wizara husika imejikita zaidi kwa ufugaji na wafugaji, ikiutelekeza uvuvi na wavuvi, hivyo kuwapa mwanya watu wasio na nia njema kuangamiza mazalia ya samaki ndani ya Ziwa Victoria.
Ifahamike kwamba uvuvi ni shughuli kubwa zaidi ya kiuchumi kwa maelfu ya watu wa kawaida wa Kanda ya Ziwa kama ilivyo kwa kilimo; ingawa wapo wanaodhani na kuamini kwamba uchimbaji madini ndio unaongoza.
Pia ifahamike kwamba maelfu ya watu wanaoishi kwenye visiwa vya Ziwa Victoria shughuli yao kubwa ni moja tu; uvuvi, na kwamba ni uvuvi ndio huwapatia chakula chao cha kila siku, huku maelfu ya tani za minofu ya samaki yakisafirishwa kwenda ughaibuni.
Kwa maana hiyo tunaiomba sana serikali kuingilia kati na hata ikiwezekana izuie aina yoyote ya uvuvi mkubwa kwa miezi kati ya mitatu hadi sita ili kurejesha kizazi cha samaki kilichopo katika hatari ya kutoweka.