DAR ES SALAAM
Na Mwalimu Samson Sombi
Nchi za Afrika zilianza kuvamiwa na kutawaliwa na mataifa makubwa ya Ulaya baada ya kumalizika kwa mkutano wa Berlin maarufu kwa jina la Kiingereza kama ‘Berlin Conference 1884/85’, uliokuwa na ajenda ya kugawana Bara la Afrika miongoni mwa mataifa kwa njia ya amani.
Aidha, kabla ya kufanyika kwa mkutano huo chini ya uenyekiti wa Kansela Bismark, kiongozi wa Ujerumani, yalitumwa makundi matatu kutoka Ulaya kuja Afrika.
Makundi hayo ambayo ni wapelelezi, wafanyabiashara na wamisionari pamoja na sababu mbalimbali zilizowaleta ajenda yao kuu ilikuwa kufanya utafiti na uchunguzi juu ya upatikanaji wa malighafi, masoko na vitega uchumi kwa ajili ya maendeleo ya viwanda huko Ulaya.
Sababu kubwa ya kuvamiwa kwa Afrika ni mapinduzi makubwa ya viwanda yaliyotokea huko Ulaya yakiongozwa na Uingereza. Mapinduzi hayo yalisababisha uhaba mkubwa wa malighafi kwa ajili ya viwanda.
Mipaka baina ya nchi za Afrika ilianza kuwekwa mwaka 1886, mataifa saba yaliyohudhuria mkutano wa Berlin yalianza rasmi kutawala makoloni yao kwa kuzingatia masharti ya mkutano huo maalumu wa kibeberu.
Tanganyika, Rwanda na Burundi zilikuwa chini ya utawala wa Wajerumani, huku Kenya, Uganda na sehemu ya Zanzibar zikitawaliwa na Waingereza.
Kuvamiwa na kutawaliwa kwa Waafrika ndiko kulikuwa mwanzo wa harakati za Waafrika hao kujikomboa kutoka katika makucha ya mabeberu waliokuwa na uchu mkubwa wa kuinyonya Afrika iliyojaliwa utajiri wa kila aina.
Nchi mbalimbali za Afrika zilianzisha vyama vya siasa kuunganisha wananchi, kupigania uhuru wa nchi hizo chini ya viongozi wazalendo na shupavu wa Afrika.
Tanganyika chini ya uongozi wa Chama cha TANU na Mwenyekiti Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilipata uhuru Desemba 9, 1961 kutoka kwa Waingereza.
Miaka miwili baada ya Tanganyika kujipatia uhuru wake Januari 12, 1964 Zanzibar ilipata uhuru wake kutoka kwa Sultani.
Kupata uhuru kwa pande hizo mbili haukuwa mwisho wa mapambano ya kuendelea kuwaunganisha Waafrika, kudumisha amani katika harakati za kujitegemea kiuchumi zaidi badala ya kuwa na uhuru wa kisiasa na uchumi tegemezi.
Katika hatua nyingine, Mwalimu Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume walikutana na kujadili kwa kina juu ya kuziunganisha pande mbili, yaani Tanganyika na Zanzibar ili kuwa nchi moja.
Kumbukumbu zinaonyesha Tanganyika na Zanzibar ziliingia mkataba Aprili 22, 1964 huko Zanzibar kwa lengo la kuunganisha nchi hizo mbili baada ya kutiwa saini na viongozi wa pande mbili – Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa upande wa Tanganyika na Sheikh Abeid Aman Karume kwa upande wa Zanzibar.
Baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo ambao ulijulikana kama hati ya Muungano, mkataba huo ulipelekwa kwenye mabunge yote mawili na Aprili, 26 mwaka 1964 uliridhiwa rasmi kuwa sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kufuatiwa na sheria kubwa ya kuchanganya udongo wa pande zote mbili.
Hata hivyo nchi hiyo mpya iliendelea kujulikana kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hadi Oktoba 28,1964 ilipobadilishwa rasmi kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , jina ambalo linatumika hadi hivi leo kupitia sheria ya Jamhuri ya Muungano Namba 61 ya mwaka 1964.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao mwaka huu umefikisha miaka 58 tangu kuanzishwa kwake ni wa mfano katika Bara la Afrika na dunia kwa ujumla kutokana na umadhubutu wake, tofauti kabisa na baadhi ya nchi za Afrika ambazo zilijaribu kuungana bila mafanikio.
Aliyekuwa Rais wa Libya, Muammar Gaddafi, alifanya juhudi za kuunganisha taifa lake na nchi za Misri na Syria kuunda umoja wa nchi za Kiarabu Septemba Mosi, mwaka 1972, matokeo yake umoja huo ulidumu hadi Novemba 19, mwaka 1977. Mataifa ya Afrika Magharibi – Senegali na Gambia yaliungana Februari, mosi 1982. Muungano huo ulidumu hadi Septemba 1989.
Pamoja na mambo mengine, muungano wetu umeendelea kudumu kutokana na muundo wake ambao unatoa haki sawa kwa pande zote mbili.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina muundo wa vyombo viwili vyenye mamlaka ya kiutendaji, ambayo ni Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pia kuna vyombo vyenye mamlaka ya utekelezaji wa utoaji wa haki ambayo ni Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mbali na hivyo, kuna vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma, ambavyo ni Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza la Wawakilishi kwa upande wa Zanzibar.
Katika utekelezaji wa shughuli zake, Serikali ya Muungano yenyewe imepewa mamlaka ya kushughulikia mambo yote ya muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri na mambo yote yasiyo ya muungano kwa upande wa Tanzania Bara.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenyewe imepewa mamlaka ya kushughulikia mambo yote yasiyo ya muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar.
Na katika upande wa Serikali Kuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano akitoka Bara, Makamu wa Rais ni lazima atoke Tanzania Zanzibar, na kama Rais wa Jamhuri ya Muungano atatoka Zanzibar, makamu wake atatoka Tanzania Bara.
Aidha, katika muundo huo kumekuwa na jamii yenye umoja, ushirikiano na isiyokuwa na ubaguzi wa aina yoyote katika harakati za kujiletea maendeleo kwa pande zote mbili.
Uchumi wa pande zote mbili umeendelea kukua kwa kasi, kuimarika kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya jamii, ulinzi wa mipaka, raia na mali zao unaendelea kuimarika siku hadi siku.
Uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine umeendelea kuimarishwa huku demokrasia na utawala wa kuzingatia na kufuata sheria ukipewa kipaumbele.
Jumatano ya Machi 31, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuapishwa kwa Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, alisema Dk. Mpango pamoja na majukumu mengine atakuwa na jukumu la kushughulikia kero za muungano, mojawapo ikiwa ni suala la fedha kwa pande zote mbili.
Katika hatua nyingine, hoja 11 kati ya 18 za muungano zimepatiwa ufumbuzi na kusainiwa hati ya makubaliano ya kuziondoa ndani ya kipindi cha uongozi wa Rais Samia.
Agosti 24, 2021 hati hizo zilisainiwa kati ya mawaziri na makatibu wakuu wa wizara husika na kushuhudiwa na Makamu wa Rais, Dk. Mpango huko Zanzibar.
Hoja hizo ni pamoja na ya uvuvi kwenye ukanda wa bahari kuu, uingizwaji wa maziwa kutoka Zanzibar na watumishi wa Zanzibar katika taasisi za muungano.
Nyingine ni mgawanyo wa mapato yatokanayo na fedha za misaada na Waziri wa Fedha Zanzibar kuwa na mamlaka ya kupokea fedha za misaada kutoka nje.
Hoja ya tano ni mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, hoja ya sita ikiwa ni mkataba wa mkopo wa ujenzi wa barabara ya Chakechake hadi Wete – Pemba.
Aidha, hoja ya saba iliyotatuliwa ni mkataba wa mkopo wa ujenzi wa Bandari ya Mpigaduli na usimamizi wa ukokotoaji na ukusanyaji wa kodi unaofanywa na Bodi ya Mapato Zanzibar.
Nyingine ni mapato yanayopatikana Idara ya Uhamiaji Zanzibar kuwekwa kwenye mfuko mkuu wa serikali kwa ajili ya matumizi, lakini kwa sasa yatabaki Zanzibar.
Hoja mbili ambazo zimeondolewa lakini hazikusainiwa hati ni uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Amana na uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa Usuluhishi wa Migogoro ya Kikodi.
Akizungumza baada ya kusaini hati hizo, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alisema hatua ya kumaliza hoja hizo itakuwa na faida kubwa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
Jumanne ya Oktoba 5, 2021 Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi alisema ameridhishwa na kasi ya utatuzi wa kero na changamoto za Muungano na kusisitiza kuwa serikali yake itatoa ushirikiano mkubwa katika kutatua kero zilizobaki na zile zinazojitokeza.
0755-985966