DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Wakati mjadala kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na bidhaa mbalimbali ukitamalaki nchini, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kinatarajia kushuhudia kujengwa kwa vituo 12 vya kubadilisha mifumo ya matumizi ya nishati katika magari.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dk. Maduhu Kazi, amesema vituo hivyo vitajengwa na Kampuni ya Taqa Arabia Tanzania Ltd.

“Vituo 12 ni vya ubadilishaji magari kutoka kutumia petroli na dizeli kwenda kwenye mfumo wa gesi. Utekelezaji wa vituo viwili vikubwa kati ya hivyo 12 utakamilika mwaka huu,” amesema Dk. Kazi.

Mpaka sasa kituo pekee kinachobadili mifumo ya magari ili yatumie nishati ya gesi ni DIT pekee, ambapo ni magari ya petroli tu ndiyo huwekewa mfumo wa gesi huku mipango ikiendelea ili magari ya dizeli nayo yaanze kubadilishwa.

Bei ya nishati ya mafuta imesababisha wadau mbalimbali wa maendeleo kuipigia kelele serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuongeza kasi ya matumizi ya gesi asilia; malighafi inayopatikana nchini.

Taarifa ya Dk. Kazi inasema miradi 85 imesajiliwa kati ya Januari na Machi mwaka huu, ambayo itasaidia kuzalisha ajira na kukuza pato la taifa.

Dk. Kazi amesema kiwango hicho ni kikubwa kulinganisha na miradi 51 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka jana, ambapo ajira 12,191 zinatarajiwa kuzalishwa.

“Miradi hiyo ina thamani ya dola za Marekani milioni 787.40 ikilinganishwa na kipindi hicho mwaka 2021 ambapo thamani ya miradi ilikuwa dola milioni 450.56. Hii ni sawa na ongezeko la asilimia 74.76,” amesema Dk. Kazi.

Amesema miradi hiyo imelenga katika uwekezaji kwenye sekta ya usafirishaji, viwanda, miundombinu, kilimo ujenzi/majengo ya biashara, taasisi za fedha, rasilimali watu, utalii na huduma mbalimbali.

Mbali na Taqa Arabia Tanzania Ltd, Dk. Kazi amesema:

“Mradi wa ujenzi wa viwanda vya saruji utatekelezwa na Kampuni ya Alotaib Nad Blak Bib na Prime Cement wenye thamani ya dola milioni 113, ambapo ajira 1,097 zinatarajiwa kuzalishwa.”

Pia upo mradi wa kuunganisha magari aina ya Howo utakaotekelezwa na Kampuni ya Saturn Corporation kwa ushirikiano wa Tanzania na Canada.

“Katika kupambana na upungufu wa mafuta ya kula, tumesajili Kampuni ya Organo Africa itakayozalishaji tani 182,000 za mafuta kwa mwaka na kugharimu dola za Marekani milioni 42.68,” amesema Dk. Maduhu.

Amesema kiwanda hicho kitazalisha ajira za moja kwa moja 1,097 na kutengeneza soko kwa mazao mbalimbali ya wakulima yatakayotumika kama malighafi.

“Hizi ni juhudi za TIC kuhakikisha tunaibua fursa mbalimbali zilizopo na kuzitangaza kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi waje kufanya uwekezaji utakaotatua changamoto zilizopo hasa ajira kwa vijana,” amesema.

Katika kipindi hicho TIC imetiliana saini miradi sita inayotarajiwa kuwekeza dola za Marekani bilioni 1.1 zitakazotumika kukuza miradi iliyopo na kuanzisha mipya, ukiwamo ujenzi wa kiwanda cha mbolea cha Intracom kinachojengwa jijini Dodoma.