Ikifika Oktoba mwaka huu wakati wa uchaguzi wa rais wa awamu ya tano, tutakuwa tumepiga hatua nzuri na ya kujivunia kuwa na utawala bora na siyo bora utawala.
Watanzania tutakuwa tumetumia demokrasia yetu ya kuchagua Serikali mpya bila kuwa na vurugu za kubadilishana madaraka.


Hili ni jambo la kujivunia, hii ni safari ndefu ilikotokea tangu wakati wa ndiyo na hapana, tangu wakati wa jembe na nyumba, tangu wakati wa kupigiwa kura na kuwa kura ya siri, tangu wakati wa kushangilia kiongozi aliyepita katika uchaguzi na kuweka kando tofauti zetu. Hii ndiyo Tanzania ninayoijua mimi vizuri.
Tanzania ya leo inakutana na changamoto nyingi, kimsingi changamoto hizi ni mwanzo mzuri wa maendeleo ya Taifa, moja ya changamoto ambazo tunapaswa kukabiliana nazo ni katika ngazi ya uongozi wa Taifa, ni vigumu na siyo rahisi kila mtu akaitaka nafasi hiyo akapewa kwa ridhaa ya wananchi bila kujua misingi ya nchi yetu inasemaje, inawezekana wapiga kura wakawa wamejazwa ujinga na kumpa nafasi hiyo nyeti rafiki yao.


Hivi sasa Tanzania tunahitaji rais, lakini ni rais wa namna gani ndilo swali ambalo tunapaswa kujiuliza kila siku, na hasa kipindi hiki tunachoelekea katika kufanya mchakato wa mgombea wa urais. Katika waraka uliopita nilisema juu ya haki ya msingi ya mtu kuchagua na kuchaguliwa.
Hadi hapa ilipofika nchi yetu, tumetoka mbali kidemokrasia na kiuongozi. Laiti tungekuwa si watu makini kuheshimu uamuzi wa wahenga wetu, Taifa leo lingekuwa limeingia katika machafuko makubwa, kwa maana hiyo basi hatuna budi kuheshimu maneno ya viongozi wetu waliotangulia ili tubaki katika hali ileile ya tangu zamani.


Tanzania ninayoifahamu mimi yenye mabadiliko kila siku, tunahitaji rais ambaye ataweza kwenda na wakati ili kuweza kukabiliana na hizo changamoto. Moja ya changamoto kubwa ambazo zinalitikisa Taifa hili ni rushwa, haya ni matokeo ya kukataa Azimio la Arusha ambalo lilikuwa na misingi thabiti kabisa ya kukabiliana na hali hiyo.


Rushwa ni adui wa haki, tunaona jinsi haki yetu inavyopotea kila siku kutokana na kuenea kwa rushwa katika kila sekta, leo hakuna sekta ambayo rushwa haijatawala, ni vita ngumu kwa kuwa imeota mizizi hadi kwa watoa rushwa wakiamini ni haki yao ya kimsingi kutoa ili wapate huduma.
Kuna vigezo vingi vya mtu kuwa rais, kimojawapo ni kutotaka hiyo nafasi kutokana na ugumu wake, siyo kazi ya kuomba kienyeji kutokana na matakwa yako, ngazi hii mtu hubembelezwa na akiona anatosha basi huchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo lakini baada ya kujiridhisha ndani ya chama anachotoka mgombea huyo.


Tunahitaji mtu mwadilifu wa kweli siyo kuigiza kama wengine, tutatumia kila njia ya kujua uadilifu wa mgombea hata kama chama kitampendekeza mgombea huyo kienyeji kwa kununua uadilifu bila kuzingatia uadilifu wa dhati ya moyo wake na malezi.
Tunahitaji rais msomi, si msomi tu wa vitabu lakini na elimu gunduzi ya maisha ya kawaida ya Mtanzania anayemuhusu, asiwe amewahi kuhusishwa na sakata lolote la ufisadi au kujihusisha na biashara yoyote haramu, na hapa tunahitaji kiongozi wa uwajibikaji hata kwa sakata ambalo halimhusu yeye moja kwa moja. Hii ndiyo sifa ya kiongozi safi.


Tunamhitaji kiongozi mzalendo, kiongozi anayeweza kusimamia rasilimali na mali ya Watanzania na nchi yao, kiongozi atakayeweka maslahi ya Taifa mbele na kukataa maslahi ya wachache, kiongozi atakayefanya urais kuwa taasisi na wala siyo mali yake, kiongozi atakayepokea kijiti na kwenda nacho mbele na siyo kurudi nyuma kimaendeleo.


Hapa tunatakiwa kurejea maandiko na maagano ya viongozi waliopita katika awamu nyingine.
Sifa za kuwa kiongozi na hasa katika ngazi hii ya urais ni nyingi na kila moja inajitegemea na wenye kuwa na sifa hizo wapo japokuwa huwa hawaonekani katika ulimwengu wa mchakato wa nafasi hiyo nyeti.
Tunamhitaji rais mwenye kuheshimu maadili, mwenye kuweza kuwajibika kwa nguvu zake zote na ambaye pia ataapa kuilinda Katiba ya nchi yetu ikiishapitishwa.

Wasaalamu
Mzee Zuzu
Kipatimo.