Dar es Salaam
Na Andrew Peter
Rekodi ya Simba katika mechi za ugenini ni kikwazo pekee kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara katika kutimiza ndoto ya kucheza nusu fainali na hatimaye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kwa mujibu wa ratiba ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba inacheza dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini; TP Mazembe ya DR Congo na Pyramids FC (Misri); ndugu wa Libya, Ahli Tripoli dhidi ya Al Ittihad; wakati Al Masry SC (Misri) wanapambana na RS Berkane (Morocco).
Simba imefuzu hatua ya robo fainali baada ya kuichapa USGN mabao 4-0 na kufikisha pointi 10 sawa na vinara wa Kundi D, RS Berkane.
Tayari wameanza harakati hizo juzi, Jumapili, wakiwa nyumbani dhidi ya Orlando Pirates na watamalizia ugenini Aprili 24, mwaka huu.
Ratiba hii inaonekana kuwa ngumu kwa Simba ambayo rekodi yake kwa mechi za ugenini inaonyesha kwamba si tu hufungwa; ila timu nzima hucheza chini ya kiwango kwa kiasi cha kushangaza.
Kocha Pablo Franco na benchi lake wanapaswa kufanya kazi ya ziada kujenga saikolojia ya wachezaji wajiamini kwamba hata ugenini wanaweza kushinda pia.
Pablo anakiri kwamba Orlando Pirates ni timu kubwa na ngumu na kwamba hakutakuwa na nafasi ya kufanya makosa. Nina uhakika hata wao wana wasiwasi, kwa sababu wanakutana na timu nzuri.
“Tunachotakiwa kufanya ni kujiandaa vizuri kwa kuhakikisha tunatumia vema mchezo wa nyumbani. Tunahitaji kuongeza umakini ugenini ili kupata matokeo mazuri,” anasema raia huyo wa Hispania na kungeza:
“Ninahitaji kutengeneza rekodi yangu na ya klabu kwa kuhakikisha tunaingia hatua inayofuata.”
Ni wazi kibarua cha Pablo kitakuwa salama zaidi iwapo Simba watafanikiwa kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.
Simba ni timu pekee ya Tanzania iliyofanikiwa kucheza robo fainali tatu; mbili za Ligi ya Mabingwa na moja ya Kombe la Shirikisho (sambamba na fainali ya mashindano haya mwaka 1993), lakini miamba hawa huwa wanyonge wanapomalizia mechi zao ugenini.
Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2010 hadi sasa, Simba imecheza mechi 17 za hatua mbalimbali za mtoano katika michuano mikubwa kwa klabu Afrika.
Katika michezo minane iliyoanzia nyumbani hatua ya mtoano; imeshindwa kusonga mbele mara saba na ni mara moja tu, mwaka 2012, ndipo ilisonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini.
Ilikuwa ni baada ya ushindi wa nyumbani wa mabao 2-0 dhidi ya ES Setifi kabla ya kufungwa ugenini mabao 3-1 hivyo matokeo ya jumla kuwa 3–3!
Katika mechi tisa ambazo Simba ilianzia ugenini na kumalizia nyumbani kwenye hatua ya mtoano; wameshinda na kusonga mbele mara sita huku wakiondolewa mashindanoni mara tatu nyumbani.
Rekodi zinaonyesha mwaka 2010 katika Kombe la Shirikisho, Simba ilitolewa katika raundi ya pili ya mashindano na Haras El Hodood kwa jumla ya mabao 3-6.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam, Simba ilishinda 2-1 kabla ya kuchapwa 5-1 jijini Cairo.
Jinamizi hili liliendelea mwaka 2011, wakitupwa nje ya mashindano na Motema Pembe kwa kufungwa jumla ya mabao 2-1.
Simba ilianza kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0 nyumbani kabla ya kupoteza 0-2 jijini.
Unyonge wa Simba ugenini uliendelea mwaka 2012, ikiwa na rekodi nzuri ya ushindi wa mabao 3-0 nyumbani, walishindwa kuulinda katika mchezo wa marudiano kwa kuruhusu kipigo cha mabao 3-0 nchini Sudan; na Al-Ahly Shendi kusonga mbele kwa ushindi wa penalti 8-9, baada ya mechi kumalizika kwa sare 3-3.
Mwaka 2018, ndoto za Simba kusonga mbele hatua ya makundi zilizimika kutokana na sheria ya bao la ugenini baada ya kulazimishwa sare 2-2 kwenye Uwanja wa Mkapa na Al-Masry; huku mchezo wa marudiano uliochezwa Misri ukimalizika bila kufungana.
Mwaka 2011 katika Ligi ya Mabingwa, Simba ilishinda rufaa dhidi ya TP Mazembe kwa kumchezesha Janvier Besala Bokungu, CAF ikaitoa mashindanoni Mazembe, lakini ikitaka Simba na Wydad AC ya Morocco kucheza mechi moja ya mtoano kwenye uwanja huru ili kupata timu ya kufuzu robo fainali.
Mechi ikapigwa Misri, Simba wakachapwa mabao 3-0.
Waliporudi tena Ligi ya Mabingwa mwaka 2013, Simba waliaga mashindano katika hatua ya awali baada ya kukubali kichapo cha jumla ya mabao 5-0 kutoka kwa Recreativo do Libolo ya Angola.
Wakifungwa bao 1-0 jijini Dar es Salaam kisha wakanyukwa 4-0 huko mjini Luanda.
Msimu wa 2018/19 ulikuwa wa mafanikio kwa Simba kabla ya ndoto zao kuzimwa na TP Mazembe kwa kufungwa 4-1 jijini Lubumbashi, DRC kufuatia sare ya kutofungana waliyoipata Dar es Salaam.
Nayo UD Songo ya Msumbiji iliwaduwaza Simba msimu wa 2019/20, baada ya kulazimisha suluhu nyumbani kabla ya sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Mkapa; wageni wakasonga mbele kwa sheria ya bao la ugenini.
Msimu wa 2020/21, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini walitumia vema uwanja wao wa nyumbani kwa kuwafunga Simba 4-0 kabla ya vijana wa Msimbazi kulipa kisasi kwa ushindi wa 3-0 lakini wakaondolewa mashindanoni katika hatua ya robo fainali kwa matokeo ya jumla wa mabao 4–3.
Pamoja na ushindi wa ugenini wa mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, msimu huu Simba waliwaduwaza mashabiki wao walipokubali kichapo cha mabao 3-1 nyumbani, hivyo kutupwa nje ya mashindano katika hatua ya awali kwa sheria ya bao la ugenini baada ya matokeo kuwa sare ya 3–3.
Kwenye makundi Kombe la Shirikisho msimu huu, katika michezo mitatu waliyocheza ugenini, Simba wamefungwa mabao sita; USGN 1-1, 2-0 na Berkane kabla ya kunyukwa 3-0 na ASEC Mimosas.
Bernard Morrison ndiye mchezaji pekee aliyeifungia bao Simba ugenini katika sare ya 1-1 dhidi ya US Gendamarine.
TAKWIMU ZA SIMBA LIGI YA MABINGWA
2011: Élan Club (Comoro) 2–4 Simba
Wydad AC (Morocco) 3–0 Simba
2013: Simba 0–5 Recreativo do Libolo (Angola)
2018/19: Simba 8–1 Mbabane Swallows (Eswatini)
Nkana (Zambia) 3-4 Simba
Simba 1–4 TP Mazembe (RD Congo)
2019/20: UD Songo (Msumbiji) 1–1 Simba
2020/21: Plateau United (Nigeria) 0–1 Simba
FC Platinum (Zimbabwe) 1–4 Simba
Kaizer Chiefs (Afrika Kusini) 4–3 Simba
2021/22: Jwaneng Galaxy (Botswana) 3–3 Simba
KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA
2010: Lengthens (Zimbabwe) 1–5 Simba
Simba 3–6 Haras El Hodood (Misri)
2011: Simba 1-2 Motema Pembe (DR Congo)
2012: Kiyovu Sports (Rwanda) 2–3 Simba
Simba 3–3 ES Setif (Algeria)
Simba 3–3 (8–9p) Al-Ahly Shendi (Sudan)
2018: Simba 5–0 Gendarmerie Nationale (Djibouti)
Simba 2–2 Al-Masry (Misri)
2021/22: Simba vs Orlando Pirates (Afrika Kusini)