Wiki hii jicho langu limekutana na kitu kinachoitwa mipango miji. Nimejipa muda wa kufikiri na kulinganisha matamanio yetu kama Watanzania juu ya tunachokiita miji safi na bora iliyopangiliwa. Ulinganisho huu nimeufanya ndani na nje ya nchi. Nimejaribu kuangalia miji ya mikoa kama Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Kagera na Dar es Salaam.

Kwa upande wa nje ya nchi nimejaribu kidogo kulinganisha miji kama Cairo (Misri), London (Uingereza), Montreal (Canada), Washington DC (Marekani), Port Elizabeth (Afrika Kusini) na Lumbumbashi (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo). Kati ya vitu nilivyoviangalia ni mipangilio ya majengo, matumizi ya majengo yaliyopo, utii wa sheria za miji husika na umakini wa viongozi kusimamia uamuzi halali uliofikiwa.

Sitanii, kinachotokea hapa ni kuwa nchi yetu inadhihirisha tofauti kubwa kati ya viongozi wetu na umakini katika kusimamia sheria. Kwa nchi za kigeni nilizozitaja, mara kadhaa nimeshuhudia kwa macho yangu kuwa wanaoheshimu sheria si viongozi tu bali hata wananchi. Nitazungumzia maeneo mawili tu, nayo ni usafi wa miji na matumizi sahihi ya majengo.

Kichwa cha makala haya kinasema tupime ubovu wa viongozi wetu kwa matendo yao. Ninachofahamu hakuna sehemu yoyote duniani ambako wananchi wanaweza kuheshimu sheria pasi uongozi bora. Mwalimu Julius Nyerere alisema ili nchi yetu iendelee inahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Hapa kwetu, naamini watu tunao, ardhi ipo, usiniulize juu ya uongozi bora na siasa safi.

Akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaa, William Lukuvi unaweza kupima alifanya nini, lakini huyu wa sasa hata jina lake silikumbuki vizuri kwani sijui anafanya nini.

Wiki hii nilikuwa namsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu. Ametoa kauli iliyonikuna kwa kiasi kikubwa. Ameeleza anavyokerwa na kauli zinazoonyesha kuwa Tanzania ni taifa la watu masikini. “Kauli hizi zinatupumbaza,” alisema Mchechu. Hakika Mchechu ameingia ndani ya mawazo yangu.

Sitanii, nilikuwa nasoma kitabu cha Dk. David Schwarze, kiitwacho ‘Positive Attitude’. Mwandishi wa kitabu hiki anasema jiepushe na tabia ya kuiambia nafsi yako mambo mabaya. Mara zote jenga utamaduni wa kujiambia kuwa ‘leo ni siku nzuri na jambo unalolenga kulifanya litafanikiwa’. Kuna usemi kuwa usipojiamini wewe nani atakuamini?

Mfano mzuri iwe mmekaa kwenye klabu ya kinywaji, kisha umwambie rafiki yako maneno haya na wenzake wakisikia: “Ndugu yangu naomba unishikie fedha zangu nisije nikazinywa.” Baada ya kauli hii unadhani yupo kati ya marafiki zako walioisikia kauli yako wanaoweza kukukabidhi fedha zao uwatunzie japo kwa muda – iwe ni siku hiyo au miaka miwili baadaye?

Hapa ninachozungumzia ni siasa chafu. Nchi yetu imejiingiza katika siasa za chee, na hatimaye kuifikisha mahala pa wanasiasa kugeuka viongozi wabovu. Viongozi wanadhani kuwa njia rahisi ya kukubalika na kuchagulika kwa wananchi ni kutetea ubovu badala ya kusimamia sheria. Ndicho wanachofanya kwa wamachinga Dar es Salaam.

Sitanii, mimi nasema tunajidanganya kama tunadhani wananchi watatupenda kwa kuwatetea wavunje sheria. Kwa njia hiyo suala la nchi yetu kuendelea tulisahau.

Tunaye mtu kama Waziri wa Ujenzi, John Pombe Magufuli. Waziri huyu nadhani Watanzania wangekuwa wanamchukia kama ukoma iwapo dhana ni kumchukia mtu anayesimamia sheria. Anasimamia nyumba ya mtu aliyeijenga kwa kuchoma maandanzi na vitumbua inabomolewa kwa sababu tu imejengwa ndani ya hifadhi ya barabara.

Wapo watu wanaozimia pale nyumba zao zinapovunjwa, isipokuwa Magufuli anasimamia sheria. Tumeshuhudia zilipovunjwa nyumba za vibopa katika fukwe za bahari huko Dar es Salaam. Nyumba zenye thamani ya hadi bilioni moja zimebomolewa, na hapa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, amethibitisha umuhimu wa kusimamia sheria pia.

Pengine niwarejeshe kwenye historia. Mwaka 1994 Edward Lowassa alifanya uamuzi wa kubomoa uzio wa Mnazi Mmoja uliokuwa umezungushwa kwenye viwanja vya Uhuru Mnazi Mmoja na mfanyabiashara aliyejulikana kama Baghdad. Hii ilimfanya Lowassa apendwe na kundi kubwa la Watanzania. Ilitokana na kusimamia sheria.

Nikiachana na mifano ya mawaziri, nirejee kwenye ngazi ya wakuu wa mikoa. Nenda Kilimanjaro leo, Mwanza na Kagera (Bukoba) ushuhudie maajabu. Miji ni misafi, biashara zinafanyika katika maeneo maalumu na imefika mahala mtu anaogopa kutupa chini uchafu. Lakini si kwa Dar es Salaam. Kanali Fabian Masawe alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kitu cha kwanza alichofanya ni kusimamia usafi wa mji.

Hivi karibuni nilikuwa Bukoba, niliponunua kadi ya simu ya mkononi nikakwangua na nilipomaliza nikata kurusha nchini kikonyo cha vocha. Muuza duka alinikimbilia akakichukua. Nilimuuliza kwa nini, akasema faini ya kurusha chini kikaratasi cha vocha ni Sh 50,000 na wapo watu wamesambazwa kufuatilia wanaotupa  hovyo aina yoyote ya uchafu kisha wawakamate.

Moshi hata ukitema mate, unakuwa umejiandaa kukamatwa. Mji wa Mwanza ulikuwa kama kijiji miaka ya 1990. Leo kwa miaka saba mfululizo unaongoza kwa usafi. Kwa wanaokumbuka yaliyokuwa machimbo ya mitumba eneo la Makoroboi, wote hawa walihamishiwa Mlango Mmoja na wameendelea kufanya biashara zao huko.

Nikirejea katika miji ya kimataifa niliyoitaja, nakumbuka mwaka 2004 nilipotembelea Canada kwa mara ya kwanza katika Jiji la Montreal, nilikuta hakuna mtu anayeruhusiwa kujenga zaidi ya ghorofa tisa kwenda juu. Niliuliza kwa nini, wakasema nembo ya mji ule ni mlima uitwao Mount Royal. Ni kwa hoja hiyo, hawataki mtu ajenge ghorofa liende juu kwa kiwango cha kuuziba mlima ule usionekane.

Watu wote na mamlaka zinazotoa vibali vya kujenga majengo katika jiji hilo kwa pamoja wanaheshimu mpango na sheria hii. Rejea hapa kwetu. Pale Masaki sheria inazuia kujenga ghorofa zaidi ya tano kwenda juu. Kibopa mmoja aliamua kujenga nje kidogo ya ufukwe wa bahari ghorofa 12. Serikali ilijitutumua kidogo ikabomoa yale maghorofa, ikadaiwa kuwa kuna watu wanamuonea wivu mwekezaji. Akaenda mahakamani ‘akashinda’ kesi.

Na inawezekana baadhi ya watu hawafahamu. Sababu ya kuzuia pale kujengwa majengo yenye urefu zaidi ya ghorofa tano ni za kiusalama zaidi. Kama nchi hatupaswi kuamini kuwa tunao marafiki wa kudumu. Imethibitika kuwa nchi nyingi zinapojiandaa kwa vita ukiwa kwenye ufukwe wa bahari kama nchi, unakuwa na hatari kubwa kuliko walioko mbali na bahari.

Kuna madege ya kivita yanayoruka sambamba na usawa wa bahari, hivyo majengo yakiwa marefu itakuwa shida wakati wa vita. Rada zitashindwa kuyaona madege hayo na hivyo nchi itatekwa kwa urahisi. Hii ndiyo sababu ya kuzuia maghorofa kwenye ufukwe wa bahari, lakini hapa kwetu tunasema ni wivu wa viongozi wetu na wakati mwingine tunatumia rushwa kutoa vibali.

Katika miji niliyoitaja, hata mng’arisha viatu anacho kibanda maalumu katika jengo linalotambulika. Biashara hazifanywi njiani au mkononi. Mbali na kwamba ni shida kukusanya kodi, madhara ya wamachinga kutawanyika mitaani ni makubwa. Unatoa fursa ya kujichanganya na wezi, uchafuzi wa mazingira na uharibifu wa miundombinu. Wamachinga nao wanajikosesha fursa ya kukopesheka kwa biashara zao kutotambulika.

Sitanii, tunaweza kupima ubovu wa viongozi wetu kwa matendo yao. Leo Dar es Salaam, kwa mfano, tumetumia fedha za walipa kodi kujenga jengo la Machinga Complex, lakini ajabu badala ya wamachinga kupanga bidhaa kwenye jengo hilo, sasa wamevamia barabara zinazolizunguka jengo na kupanga vitu chini nje ya jengo hilo. Hivi sisi wananchi wa kawaida tuamini katika hili?

Ninaloweza kuamini ni kwamba Mkoa wa Dar es Salaam una viongozi wabovu sijapata kuona. Maegesho ya muda mfupi (slot parking) leo yamekabidhiwa kwa wakusanya ushuru ndiyo maegeso ya siku nzima (day parking) kati ya saa 2:00 hadi saa 11:00 jioni.

Fedha zinazokusanywa hata hazionekani zinaelekea wapi. Barabara sasa zimepunguzwa ukubwa na kugeuzwa maegesho, magari yanapita kwa shida eneo kama Posta wakati Jengo la Benjamin Mkapa lina sehemu ya maegesho, bado wenye hoteli wamepewa barabara ya umma iwe maegesho yao.

Naamini viongozi wanaoongoza jiji hili wana matatizo makubwa kuliko maelezo. Haiwezekani hawana matatizo barabara zikaminywa na kuwa sawa na njia za kupitishia baiskeli wakati wao wanaona. Kwamba magari yataegeshwa wapi hili si tatizo. Watu watumie daladala kwa kuboresha usafiri kama huo mijini.

Mwisho, ningependa kueleza masikitiko yangu kuona wamachinga wanazagaa jijini Dar es Salaam wakati limejengwa jengo lao mahususi na halitumiki. Hivi kuna umakini kiasi gani? Hii inathibitisha kuwa tuna uongozi mbovu na siasa chafu Dar es Salaam kwa sasa. Tubadilike.