DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Washiriki wa Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania wanawatuhumu baadhi ya viongozi wao kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo ubadhirifu wa fedha na matumizi mabaya ya madaraka.

Tuhuma hizo zimesababisha mgogoro wa muda mrefu na kusababisha washiriki hao watano; Nathanael Bhubuli, Maila Makambi, Nehemiah Matiku, John Augustine na Machibya Mayala kuziwasilisha kwa Msajili wa Jumuiya wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kuomba uchunguzi maalumu ufanyike.

Kupitia barua waliyoandika Agosti 30, 2021 kwenda kwa Msajili wa Jumuiya, washiriki hao wanasema kuanzia mwaka 2014 hadi sasa kanisa la Jimbo Kuu la Kusini, Konferensi ya Mashariki Kati (ECT) na Konferensi ya Kusini Mashariki (SEC) limeshindwa kutoa taarifa ya mapato na matumizi na kuonyesha mali zao na kusababisha kutoaminiana kati ya waumini na viongozi kwa kuwa ni wagumu kusikiliza sauti na vilio vyao vya kutaka kupewa taarifa ya mapato na matumizi.

“Tafadhali rejea maelekezo yako, pia kikao cha pamoja kilichofanyika Agosti 17, 2021 kilichoitishwa na Msajili wa Jumuiya ili kusikiliza malalamiko ya tuhuma za ubadhirifu unaoendelea ndani ya kanisa letu, hususan Jimbo Kuu la Kusini, ECT na SEC.

“Kwa kuzingatia kuwa hatusikilizwi pamoja na kuandika barua mbalimbali, baadhi ya washiriki tulionana na Msajili wa Jumuiya kwa pamoja na viongozi wakuu wa unioni zote mbili za Kaskazini na Kusini za kanisa.

“Katika kikao hicho ilikubalika kuwa mambo haya mawili ni makubwa na yanahitaji ‘commitment’ kubwa ya viongozi ili yafanyiwe kazi na kuondoa tofauti za viongozi na waumini.

“Malalamiko hayo yaliwasilishwa kwako na washiriki wa kanisa baada ya kulalamika na viongozi wa jimbo kuu na konferensi zake kutokuwa tayari kusikiliza malalamiko yetu na katika kikao hicho kulitolewa maelekezo na kuagiza kufanyia kazi maeneo mawili makubwa na walalamikaji walipewa jukumu la kuyawasilisha.

“Maeneo hayo ni uchunguzi maalumu ufanyike kuthibitisha tuhuma za kukosekana utawala bora kwa kipindi cha Januari, 2014 hadi Juni, 2021 na katiba iliyopo sasa ifanyiwe marekebisho ili kuingiza kasoro zote zilizowasilishwa kwenye kikao hicho.”

Washiriki hao wanasema walielekezwa kufanya hivyo kwa kuorodhesha maeneo yote yanayolalamikiwa na yenye kasoro ya utawala bora wayawasilishe na nakala kwa unioni zote mbili ili kumwezesha msajili kuteua mchunguzi maalumu atakayefanya uchunguzi huo.

Licha ya kufanya hivyo na kuomba uchunguzi huo uanze mara moja lakini wanasema kwa bahati mbaya vinara wa tuhuma hizo ambao ni viongozi wao katika Unioni ya Kusini (STUM) na katika konferensi za ECT na SEC bado wapo ofisini na wana taarifa zinazodai kwamba wameanza kuharibu ushahidi na wanashauri wakae pembeni.

“Tunashauri wakae pembeni na kupisha uchunguzi utakaokuwa huru na haki. Malalamiko yaliyowasilishwa tuna hakika ni ya kweli na bado ubadhirifu unaendelea kufanyika kwenye kanisa letu, hivyo si vema watuhumiwa kuendelea kukaa ofisini wakati uchunguzi unaendelea,” wamesema.

Viongozi wanaoshauri wakae pembeni ili kupisha uchunguzi huo ni kutoka Union ya Kusini mwa Tanzania ambao ni Mchungaji Mark Malekana (Mwenyekiti), Mchungaji Rabson Nkoko (Katibu Mkuu), Athanas Sigoma (Mhazini Mkuu), Mchungaji Christopher Ungani (Mkurugenzi wa Mawasiliano) na Reuben Mbonea (Mhasibu wa Vyombo vya Habari).

Kutoka ECT ni Mchungaji Joseph Mngwabi (Mwenyekiti), Mchungaji Amos Lutebekela (Katibu Mkuu) na Enock Rabieth (Mhazini Mkuu) na kutoka SEC ni Mchungaji Steven Ngussa (Mwenyekiti), Mchungaji Wilfred Mafwimbo (Katibu Mkuu) na Yusufu Zege (aliyekuwa Mhazini Mkuu).

Tuhuma

Kuhusu ubadhirifu wa fedha, wanadai unafanywa na viongozi hao wakuu waliopo sasa kwa kudaiwa kujitajirisha na kusahau wito wa kuchunga kondoo wa Mungu.

Pia wanasema katika ugawaji wa konferensi (majimbo) za SEC na ECT kutoka Konferensi ya Mashariki mwa Tanzania (ETC) kuna ubadhirifu ulifanyika ndiyo maana hakuna taarifa inayoonyesha kuna mali na madeni.

“Kwa kawaida kama taasisi inavunjwa au kufikia mwisho wa uhai wake inalazimika kuandaa financial statements itakayoonyesha mali na madeni (assets and liabilities) na kama ni endelevu au imegawanyika kama ilivyofanyika kwa ETC, ni lazima kuwepo jedwali linaloonyesha mgawanyo wa mali na madeni ya taasisi iliyokoma kuishi,” wamesema na kuongeza:

 “Lakini hadi leo hakuna taarifa yoyote ya maandishi ya mali na madeni ya iliyokuwa ETC na hayajulikani lakini viongozi hawataki kusema wala kutoa taarifa ya mgawanyo wa mali na madeni kama ilivyokuwa.

“Tunaelewa kuwa wakati wa kuivunja ETC kulikuwa na kiasi kikubwa cha fedha katika akaunti za benki lakini pia hatujawahi kuonyeshwa kama zilipelekwa ECT na SEC ingawa miongozo ya kanisa inawataka kufanya hivyo.

“Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi uliofanywa na Shirika la Kidini la Kisabato, ECT na SEC zimeanza na fedha sifuri bila fedha yoyote kutoka konferensi iliyogawanywa wakati tunaamini kulikuwa na zaidi ya Sh bilioni tano.”

Pia wanazitaja mali za ETC zisizopokewa ECT na SEC kuwa ni maeneo yaliyonunuliwa Chalinze kwa ajili ya kujenga makao makuu eneo la Vigwaza mkoani Pwani na magari na mashamba ya korosho yaliyonunuliwa Mtwara na Lindi.

Kuhusu fedha za zaka wanasema huwasilishwa katika konferensi na makanisa mahalia ili zipelekwe ngazi za juu za kanisa lakini wanamtuhumu Malekana kuwa alipokea Sh milioni 400 kutoka makanisa mbalimbali lakini hakuziwasilisha kwa wakati sehemu husika kwa zaidi ya mwaka mmoja.

“Kulingana na mgawanyo ulioanishwa na kusomwa katika makanisa mahalia mbalimbali, hivyo kusababisha ongezeko la deni kwa asilimia 56 ikilinganishwa na deni la mwaka 2015, jambo ambalo ni kinyume cha taratibu za kanisa.

“Kutumia fedha zilizotolewa na makanisa mahalia kwa ajili ya kuwasilisha ngazi za juu za kanisa lakini viongozi kushindwa kuziwasilisha ni kosa kubwa linaloweza kumtoa katika nafasi yake.

“Wakati wa kuipanga ETC pia kulikuwa na zaka ilipotea, hivyo tungependa uchunguzi uonyeshe zaka ya mwaka 2014 ilikuwa kiasi gani na ilipelekwa wapi? Tunaelewa kwenye Akaunti ya Zaka kulikuwa na zaidi ya Sh milioni 800 katika fixed deposit account na Malekana anajua fedha hizo zote zilikwenda wapi na kwa nini hazikupelekwa kunakostahili kwa wakati?”

Pia wanataja ubadhirifu mwingine kuwa umefanyika katika shamba lao la Kibidula lililopo Mafinga mkoani Iringa baada ya kukodishwa kwa siri kwa bei ndogo ya Sh milioni nne kwa mwezi kwa muda wa miaka 28.

Aidha, wanasema kulitokea wizi wa fedha katika Shule ya Msingi ya Kongowe Adventist na licha ya kamati mbili kuundwa chini ya Mchungaji Heri Kuyenga mwaka 2019 na Dk. Daniel Sabai mwaka 2020 na kuonyesha kuna matumizi mabaya ya madaraka lakini hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na fedha za ujenzi wa Kituo cha Afya Mtwara hazijulikani zimekwenda wapi licha ya kuchangwa na waumini na hadi sasa hakuna kilichofanyika.

Vilevile wanataja ubadhirifu mwingine kutokea katika ujenzi wa makao makuu ya SEC na ununuzi wa mashine ya kufyatulia matofali, miradi ya ujenzi ya ECT na katika mkutano wa ‘Extra Vaganza’ uliofanyika Morogoro mwaka 2020.

Katika hatua nyingine, wanasema katika kikao tendaji cha ECT kilichofanyika Agosti 2, 2016 ilikubaliwa na kupitishwa kwa ‘Evangelism Appropriation’ ya mwaka 2015 na jumla ya Sh 117,234,536.02 zilitolewa huku wakijua ulishapita na haiwezekani ikatolewa ruzuku kwa mwaka uliopita.

“Tunaelewa kuwa moja ya sababu ya kuondolewa Mchungaji Samwel Katengu aliyekuwa Katibu Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa ECT na Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi zinazodaiwa kupelekewa fedha hizo (shule za Kitungwa na Agape) ni pale alipohoji uhalali wa malipo hayo na kukataa kusaini muhtasari wa kikao kilichoidhinisha fedha hizo,” wanasema.

Pia wanasema ubadhirifu mwingine umetokea katika ununuzi wa Kituo cha Rock FM kutoka dola 15,000 za Marekani alizotaka muuzaji hadi Sh 150,000,000 na kuna tuhuma ya matumizi mabaya ya zaidi ya Sh milioni mia nne kutoka katika sadaka inayotolewa na washiriki wa kanisa letu kwa ajili ya vyombo vya habari vya kanisa.

Vilevile wanaomba ufanywe uchunguzi wa ujenzi wa jengo dogo la studio za STUM uliogharimu zaidi ya Sh milioni 200 usioendana na thamani ya fedha.

Pia wanaomba ufanyike uchunguzi kutokana na ubadhirifu uliotokea katika Kiwanda cha Uchapaji (Ufunuo Publishing House) kilichopo Morogoro pamoja na maduka ya vitabu ya kanda (ABC).

Uchunguzi mwingine wanaoomba ufanyike ni mapato na matumizi ya Chuo Kikuu cha Arusha na fedha inayotumwa kutoka kwenye zaka na  hatua hiyo imesababisha kushindwa kufanya udahili kwa mwaka wa masomo wa 2020/2021 pia uchunguzwe upotevu wa zaidi ya Sh bilioni mbili na fedha zilizotumwa kutoka divisheni kwa ajili ya ujenzi wa chuo.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani

Kwa upande wake Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Christina Mwangosi, anasema: “Ianabidi nimtafute msajili nimuulize kuhusu hilo suala maana liko mezani kwake kisha nitakujulisha limefikia hatua gani, maana migogogo makanisani yana mambo mengi mno.”

 Wanaotuhumiwa wafunguka

Mwishoni mwa wiki iliyopita Gazeti la JAMHURI liliwatafuta viongozi wote wanaotuhumiwa na washiriki wao, baadhi simu zao za mkononi hazikupatikana, wengine ziliita bila kupokewa na baadhi wakafunguka kwa kusema tuhuma hizo si za kweli kwa sababu haziwezi kutokea katika kanisa hilo na kwa kuwa sasa hivi ziko ngazi nyingine hawawezi kutoa ufafanuzi zaidi.

Mchungaji Malekana anasema na kuongeza: “Hizo tuhuma zimeshafika katika chombo kingine sasa tunaanzaje kuzisemea? Ngoja zishughulikiwe katika chombo kilichopelekewa. Zikishughulikiwa katika chombo husika utaandika.

“Nilivyosikia tuhuma hizo, kwanza nilishangaa, kwa sababu vitu vya hovyo haviwezi kutokea katika kanisa hili kwa namna yoyote ile, nadhani tusubiri, kwa sababu limekwenda katika chombo husika kinashughulikia na itafahamika kwa jamii na wanaotoa tuhuma hizo wana nia mbaya tu ya kuchafua taswira ya mtu kwa masilahi yao.”

Naye Sigoma amesema na kuongeza: “Hizo tuhuma nimeziona na kwa sababu ziko ofisini kwa Msajili wa Jumuiya isingekuwa vizuri kuanza kulizungumzia, kwa sababu sasa hivi tuko katika mchakato wa kukutana naye na tukishaonana tutakuwa na nafasi ya kuzungumza.

“Tarehe ya kukutana na msajili itapangwa na tutajulishwa kwa sababu liko mezani kwake. Sasa hivi tunamsubiri yeye tu na siwezi kujua yeye atatupangiaje? Ila ni vigumu kuzungumzia tuhuma hizo kama ni za kweli au si za kweli kwa sababu mtu akishakutuhumu anatakiwa alete ushahidi wa kutosha kuhusiana na tuhuma hizo na bila shaka kutakuwa na ushahidi wa kutosha kwa waliozipeleka na kututhibitishia.”

 Kwa upande wake, Mchungaji Mngwabi, anasema: “Tuhuma kama hizo siongei kupitia simu. Ninachofahamu ni kwamba hilo jambo liko kwa wadhamini wa kanisa kwa hiyo kwa sasa hivi siwezi kulizungumzia kwa sababu mimi si msemaji wake.”

Naye Mchungaji Nkoko anasema: “Siwezi kulizungumzia kwa namna yoyote kwa vyombo vya habari. Nakushauri hilo jambo achana nalo tu kwa jinsi lilivyo.”

Mchungaji Ngussa anasema na kuongeza: “Umefanya vizuri kunitafuta lakini kanisa lina taratibu zake za kujibu tuhuma kama hizo.

“Kwa namna yoyote ile nikusihi ukifuata utaratibu utapata majibu vizuri maana wapo wasemaji wa kanisa na kuna namna ya kuzipata hizo habari na hakuna habari yoyote inayofichika, sisi ni wasafiri wa mbinguni.”

Kwa upande wake Mchungaji Lutebekela anasema na kuongeza: “Hizo tuhuma nimeshazisikia lakini kuanza kuzisemea mimi si msemaji wa kanisa. Wako wenyeviti wa unioni na konferesi na hao ndio wanaoweza kuzisemea hizo tuhuma.

“Hizo tuhuma zinasema sisi tukae pembeni tupishe uchunguzi lakini hazijasema mimi nimechukua kiasi gani. Tuhuma zote hizo hazinitaji mimi kuchukua kitu chochote, sasa kama hizo tuhuma ni kweli au si kweli wanaotakiwa kusema ni hao viongozi wetu wa juu ambao ni wenyeviti wetu.”