DAR ES SALAAM

Na Joe Beda

Wakati kupanda kwa bei ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kukielezwa kuwa hakuepukiki, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imekubaliana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwamba kuna haja sasa kwa taifa kuanza kutumia nishati mbadala.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje, amesema pamoja na kupanda huku kwa bei, taifa lina akiba ya kutosha ya nishati ya mafuta.

“Kwa mujibu wa mwenendo wa hifadhi ya mafuta, nchi ipo salama. Mafuta yapo na yanatosha,” amesema Chibulenje.

Taarifa ya Ewura inaonyesha kuwa hadi Jumamosi mchana akiba ya petroli ilikuwa inatosha kwa siku 27 huku dizeli ikiwapo ya siku 19, mafuta ya taa ya siku 108, pia kukiwa na mafuta ya ndege ya kutosha.

Mbali na hifadhi hiyo, Chibulunje amesema kuna meli zipo bandarini zinapakua mafuta na nyingine zipo njiani kuleta nishati hiyo nchini.

Bila kutaja bei mpya inayotarajiwa kutangazwa kesho, Chibulunje ametaja sababu ya kupanda kwa bei kuwa ni vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

“Vita hii imeathiri kwa namna fulani ‘logistics’ (mipango/operesheni) za usafirishaji wa mafuta ambapo kwa sasa tani moja ya petroli imepanda hadi kufikia dola za Marekani 1,106 kutoka dola 716,” amesema.

Hata hivyo, Chibulunje amesema kwa mujibu wa mwenendo wa bei ya mafuta duniani, tathmini inaonyesha kuwa pamoja na ukubwa wa bei unaoonekana nchini, bei hizo bado ni za chini kulinganishwa na baadhi ya nchi za Ulaya, Asia na Amerika huku kukiwapo matangazo ya kuanza kwa mgawo wa nishati hiyo katika nchi kadhaa.

Ametoa mfano wa petroli ambayo kwa Tanzania inauzwa kwa Sh 2,540 kwa lita; Kenya ni Sh 2,703; Zambia 2,827; Rwanda 2,839, Burundi Sh 3,095 na Malawi ni Sh 3,271.

Bei katika mataifa mengine ni Sh 3,347 (Afrika Kusini); Sh 5,436 (Zimbabwe); Sh 2,827 (Marekani); Sh 4,939 (Uingereza) huku Sweden wakinunua petroli kwa Sh 5,198 kwa lita.

Nini kifanyike?

Katika hali kama hiyo, Chibulunje amewataka Watanzania kutunza nishati iliyopo, kwa kuwa na matumizi makini.

“Ninaweza kusema ‘tufunge mikanda’. Lakini pia sasa wakati umefika wa kuongeza kasi ya matumizi ya gesi asilia kama nishati mbadala, kwa kuwa sisi hatuna udhibiti wa moja kwa moja wa nishati kutoka nje ya nchi,” amesema.

Kauli ya Chibulunje ikaibua mjadala mzito ukumbini, wahariri wakitaka kufahamu serikali imefikia wapi katika matumizi ya gesi asilia kama nishati stahiki badala ya mafuta ya petroli na dizeli viwandani, pamoja na matumizi ya nyumbani.

Miongoni mwa mapendekezo yaliyotolewa na wahariri ni kuondoa au kupunguza tozo kwa vifaa vinavyoingia nchini na kuwekeza kwenye miundombinu ya gesi asilia ili kuifanya ipatikane kwa urahisi na kuongeza idadi ya watumiaji wake.

“Uchumi wetu upo katika mafuta pekee; yaani ni ‘oil based economy’. Huu ni uchumi tegemezi. Kwa nini tusihamie kwenye ‘gas based economy’? Tunakwama wapi?” amehoji Allan Lawa, mwanahabari mwandamizi na mhariri mstaafu.

Wahariri kadhaa wameonyesha kushangazwa na idadi ndogo ya magari yanayotumia gesi, wakitaka kabla ya kuandaliwa kwa sera ya kitaifa itakayotoa mwongozo kwa kila mmiliki wa kituo cha mafuta kuwa na kituo cha gesi asilia, idadi ya watumiaji wa gesi iongezeke kwanza.

Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Ewura, Titus Kaguo, amesema tayari kuna leseni tatu za vituo vya kuuza CNG (compressed natural gas) kwa ajili ya magari zimetolewa.

“Leseni moja ni ya kituo cha CNG Ubungo Maziwa, kuna leseni nyingine ya kujenga kituo TAZARA na nyingine ni ya Dangote,” amesema Kaguo.

Ewura wamekiri kwamba kasi ya matumizi ya gesi majumbani, viwandani na kwenye magari ni ndogo kuliko ilivyotarajiwa; kauli iliyoifanya TEF kuomba juhudi ziongezwe.

“Tutafanya jitihada za kupanua wigo wa mjadala huu na kuwakutanisha wadau wengi zaidi kujadili namna ya kuondoka hapa tulipo. Ni lazima tuwe na nishati mbadala itakayoondoa adha ya kupanda mara kwa mara kwa bei ya mafuta na kuwa na uchumi tegemezi,” amesema Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile.

Kauli ya Balile imeungwa mkono na wahariri ambao ni wanachama wa TEF wakiahidi kulivalia njuga suala la matumizi ya gesi asilia.

Takwimu za mwaka 2020 zinaonyesha wastani wa uzalishaji wa gesi asilia kwa siku ulikuwa futi za ujazo milioni 160.92 (160.92mmsfd); katika hizo, wastani wa futi za ujazo milioni 136.068 kwa siku sawa na asilimia 85 hutumika kuzalishia umeme; futi za ujazo milioni 20.53 sawa na asilimia 14 zimekwenda viwandani na asilimia moja tu ndiyo imetumika kwenye magari na majumbani.