Zanzibar
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewasihi wafanyabiashara kutoutumia mgogoro wa Urusi na Ukraine kama kisingizio cha kupandisha bei za bidhaa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza katika risala ya kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Dk. Mwinyi amesema serikali haitasita kuwachukulia hatua za kisheria watakaokwenda kinyume cha maagizo inayoyatoa.
“Nimepata taarifa kwamba bidhaa nyingi za chakula zitakazouzwa Mwezi wa Ramadhani zimeingizwa nchini hata kabla ya kuibuka mgogoro wa Urusi na Ukraine,” amesema.
Amewahakikishia wananchi na wafanyabiashara kwamba serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uchumi wa dunia na gharama za kufanya biashara ili kuhakikisha bei za bidhaa zinazouzwa kwenye maduka ya jumla na rejareja zinaakisi uhalisia, uwezo na kipato cha mwananchi.
Amewahimiza wakuu wa taasisi zinazoshughulika na biashara, wakuu wa mikoa, wilaya na masheha kufuatilia mwenendo wa bei katika maeneo yao ya utawala na kuwachukulia hatua za kisheria wanaojaribu kukiuka sheria na maagizo ya serikali.
“Wakati Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ukikaribishwa, kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia bado haipo katika hali ya kawaida, kama ilivyokuwa kabla ya kuzuka kwa janga la UVIKO – 19 mwishoni mwa mwaka 2019.
“Pamoja na kuendelea kuwapo kwa changamoto zilizoambatana na maradhi hayo, hivi karibuni mgororo wa Urusi na Ukraine umeibua taharuki mpya kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii duniani.
“Serikali zetu zote mbili zinaendelea kufuatilia kwa karibu matukio hayo na kuchukua hatua za tahadhari ili kupunguza athari zinazojitokeza katika uchumi wetu,” amesema Dk. Mwinyi.