Na Joe Beda Rupia
Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) umefanyika jijini Dodoma wiki iliyopita. Ndiyo. Hili ni miongoni mwa matukio ambayo sisi wana habari hulazimika kuyafuatilia.
Ni tukio kubwa nchini kwa kuwa hukusanya watu kutoka kila pembe ya taifa. Hakuna wilaya iliyokosekana au iliyokosa mwakilishi Dodoma wiki iliyopita. Tena si mmoja au wawili!
Maana yake nini? Ni mkusanyiko mkubwa. Mkusanyiko huu unapaswa kutumika vizuri kwa kuonyesha, kuboresha na kuendeleza utamaduni wa Kiafrika; lakini zaidi utamaduni wa Mtanzania.
Kinachofanyika pale kinapaswa kuakisi utamaduni na ustaarabu wa Kitanzania na ikiwezekana, kichukuliwe na kusambazwa nchi nzima.
Sidhani kama neno ‘utamaduni’ na au ‘mila’ linaweza kuzua mjadala au linapaswa kuzua mjadala wa aina yoyote hapa.
Ni sahihi kwamba kila kabila lina mila, tamaduni na desturi zake. Tunafahamu au kuamini kwamba Tanzania kuna makabila zaidi ya 120.
Hapa ni pamoja na yale makabila mapya yaliyoongezwa au kuongezeka majuzi; yaani Wahutu wa Katumba, Mishamo na Bulyankulu katika mikoa ya Tabora na Katavi, pamoja na Wangazija wa Zanzibar.
Bara la Afrika linaundwa na mataifa 54 likiwa na zaidi ya watu bilioni 1.3 na makabila zaidi ya 3,000.
Pamoja na wingi wa makabila haya, yapo masuala kadhaa yanafanana na kukubalika miongoni mwa makabila mengi ya Kiafrika.
Sasa hayo yanayokubalika na kufanana ndiyo tunayoyajumuisha kwenye ‘utamaduni’ na ustaarabu wa Kiafrika. Vivyo hivyo kwa makabila zaidi ya 120 yaliyopo Tanzania.
Mathalani, heshima miongoni mwa wanajamii; lakini hasa kwa watoto kwenda kwa wakubwa, ni jambo ambalo linasisitizwa karibu na makabila yetu yote.
Pia yapo mambo yanayoweza kuzungumzwa au kufanywa hadharani na watu wa rika fulani, lakini kamwe hayawezi kufanywa au hata kutamkwa kwenye mchanganyiko wa rika labda tu iwapo ni kwenye mafunzo au mkusanyiko maalumu.
Hayo wala hayahitaji kwenda darasani na kufundishwa! Unakua tu na kuyaona huku ukijifunza ama kutoka kwa wazazi wako au marafiki zako.
Lakini pia kuna nyakati unaweza kukumbushwa kuwa, hili? Hapana. Hapa si mahala pake.
Hakuna siri kwamba Mkutano wa CCM jijini Dodoma ulifanikiwa sana katika kusudi la kukusanyika kwake. Lakini kulikuwapo dosari ya wazi kabisa. Burudani.
Ngoma, muziki, ngonjera, utani na vichekesho ni miongoni mwa tamaduni za Kiafrika na aghalabu hupewa nafasi kwenye mikusanyiko kama ule wa CCM huko Dodoma.
Nimewahi kuandika katika ukurasa huu Desemba mwaka jana nikimlaumu mchekeshaji ‘Mchungaji’ Masanja Mkandamizaji kwa alichokifanya wakati wa sherehe za miaka 60 ya Uhuru.
Sijui kama Masanja aliwaomba radhi waliomualika kwa kuleta utani wa kijinga kwenye shughuli ‘serious’ kama ile! Kama hakuomba radhi, ni bahati mbaya sana.
Juzi tena, msanii mwingine kijana, Zuchu, naye akaalikwa jukwaani. Sina shaka hata kidogo na kipaji na umaarufu wake! Na wala sikuwa na shaka nilipomuona akipanda jukwaani.
Nilijua fika kwamba atatoa burudani sahihi na stahiki kwenye hadhara ile. Ndiyo. Ni kwa kuwa mara ya kwanza kumuona ilikuwa kwenye mkusanyiko kama huo huo, kwenye ukumbi huo huo; Julai 11, 2020 wakati CCM walipokutana kumpitisha Dk. John Magufuli kuwa mgombea wa urais kwa muhula wa pili, kisha naye akamtangaza Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea mwenza.
Zuchu alitikisa mkutano ule kwa wimbo wenye maneno: ‘Tanzania ya sasa maamaa! Ni ya Magufuli maamaa!’ na kibwagizo cha: ‘Hai! Hai! Hai! Hai!’
Bahati mbaya sana safari hii akianza kwa kuimba nyimbo zisizo na maudhui ya mkusanyiko wa vijana, watu wazima na wazee; lakini kibaya zaidi viongozi wanaoheshimika ndani na nje ya nchi.
Bahati mbaya zaidi nyimbo za akina Zuchu kama ule ‘Sukari’, wala hazina mafumbo! Unaimbwa mchama kweupeeee! Unashangaa, ni nani alimuandaa Zuchu na kukagua atakachokiimba mbele ya Rais hata kama pale alikuwa mwenyekiti wa chama? Alitaka kuwafundisha Watanzania kitu gani?
Ni aibu kwa kibinti kidogo kama hiki kuimba wimbo ule kwa watu wenye umri na hadhi sawa na hata kuwazidi wazazi wake. Huu si utamaduni wa Kitanzania!
Hata kama aliimba sehemu ndogo tu ya wimbo huo, bado pale hapakuwa mahala sahihi kwa ujumbe wa wimbo huo. Hata ule wimbo mwingine wenye maneno ya ‘nyumba ndogo’ nao hakustahili hata kuudokeza ukumbini pale.
Mbona JUWATA, Sikinde na hata TOT Plus huwa wanabadili nyimbo zao na kuingiza maneno yenye maudhui stahiki?
Hata mwaka 2010 wakati wa kampeni za Rais Jakaya Kikwete, wasanii walibadili maneno ya nyimbo zao na kuingiza ya kampeni; sasa Zuchu anashindwa vipi?
Ushauri ni iwapo hakuna watu wa kuwaongoza wasanii hawa nini cha kuimba kwenye mikutano kama ile, ni bora wasialikwe kabisa, kwani ni aibu tupu.
0679 336 491