Leo Jumanne Aprili 05, 2022, ni tarehe 3 Ramadhani (Mwezi wa 9 kwa Kalenda ya Kiislamu inayoanza Mwezi Muharram – Mfungo Nne) Mwaka 1443 Hijiriyya (toka kuhama kwa Mtume Muhammad –Allah Amrehemu na Ampe Amani – kutoka Makkah kwenda Madinah), kwa mujibu wa matangazo yaliyotolewa na Mheshimiwa Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Dk. Abubakar bin Zubeir bin Ally Mbwana na Mheshimiwa Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Salehe Omar Kaabi kwamba mwezi mwandamo wa Ramadhan haukuandama magharibi ya Ijumaa ya tarehe Mosi Aprili 2022 siku iliyokuwa tarehe 29 Shaaban Mwaka 1423 Hijiriyyah na kwamba kwa Waislamu wanaotii mamlaka hizo za Kiislamu walikamilisha siku 30 za Mwezi wa Shaaban na waliuanza mfungo wa Ramadhani siku ya Jumapili tarehe 3 Aprili mwaka huu.
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mbali ya kuwa unabeba ibada ya funga ikiwa ni moja ya Nguzo Tano za Uislamu, ibada iliyo kongwe sana kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah) Aya ya 183 kuwa: “Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Saumu (kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani), kama waliyoandikiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mwenyeezi Mungu.” Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni Mwezi wa Qur’aan Tukufu kwa kuwa ndio mwezi ambao imeteremshwa humo Qur’aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili) kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 2 (Surat Al-Baqarah, Aya ya 185 kuwa: “Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa humo Qur’aan kuwa ni uongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi. Basi atakaye kuwa mjini katika mwezi huu na afunge. Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mmtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru.”
Vilevile kama ilivyopokewa na Ibn Abbaas (Allaah Amridhiye) kuwa makusudio yake kwa hakika kuteremshiwa Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) Qur’aan mwanzo ni katika mwezi wa Ramadhwaan na vilevile Qur’aan mwanzo wa kuteremka ni usiku wa Laylatul-Qadir na Laylatul-Qadir iko katika mwezi wa Ramadhwaan.
Hivyo ni muhimu sana kukithirisha sana kusoma Qur-aan Tukufu katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. Wema Waliotangulia walikuwa wakikihifadhi Kitabu cha Allaah kwa kukisoma na kuyafanyia kazi yaliyokuwemo kwa mazingatio. Pia tunaambiwa kuwa Malaika Jibril (Juu yake Amani) alikuwa akimfundisha Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) Qur’aan Tukufu katika mwezi wa Ramadhan, na alikuwa Swahaba Uthmaan bin Afaan (Allaah Amridhiye) kila siku akisoma Qur’aan yote, yaani anausoma msahafu wote kwa siku moja.
Na walikuwa baadhi yao katika watu wema wakisoma Qur’aan yote kwa siku tatu, wengine kwa wiki moja na wengine kwa siku kumi. Walikuwa wakisoma Qur’aan ndani ya Swalah na nje ya Swalah.
Yaliyotangulia yamekusudia kuweka wazi upekee wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Sasa tuangazie baadhi ya fadhila zake.
Mwezi wa Laylatul Qadri (Usiku wa Cheo):
Katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani kuna usiku mashuhuri uitwao “Laylatul-Qadr” (Usiku wa Cheo), usiku ambao ni bora kuliko miezi elfu kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 97 (Surat Al-Qadri), Aya ya 1 – 5 kuwa: “Hakika sisi tumeiteremsha Qur’aan katika Laylatul Qadri, Usiku wa Cheo Kitukufu. Na nini kitachokujulisha nini Laylatul Qadri? Laylatul Qadri ni bora kuliko miezi elfu. Huteremka Malaika na Roho (Malaika Jibril) katika usiku huo kwa idhini ya Mola wao Mlezi kwa kila jambo. Amani usiku huo mpaka mapambazuko ya alfajiri.”
Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alipata habari ya mtu aliyepigana jihadi kwa muda wa miezi elfu moja na akaona umri wa ummah za mwanzo ni mrefu, na umri wa ummah wake ni mfupi, akamuomba Mola wake kwa kusema: “Ewe Mola wangu wa Haki, umeufanya ummah wangu ni wenye umri mfupi na amali chache.” Mwenyeezi Mungu Mtukufu Akampa usiku wa Laylatul Qadri ulio bora kuliko miezi elfu moja aliyopigana jihadi huyo mja mwema aliyetajwa.
Hakuna usiku mtukufu na mkubwa kama usiku huu, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuutafuta usiku huu katika kumi la mwisho kwa kufanya ibada ili tupate fadhila hizo.
Mwezi wa kuzidisha kufanya kheri na kutoa:
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mwezi anaopaswa kila mmoja wetu kujitahidi kukithirisha matendo ya kheri na kutoa kuwasaidia wasio nacho na wale wenye haki ya kupewa Zakkah na Swadaka, kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 9 (Surat At-Tawbah), Aya ya 60 kuwa: “Wa kupewa sadaka ni mafakiri na maskini, na wanao zitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao (waliosilimu), na katika kukomboa watumwa, na wenye madeni, na katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua Mwenye hikima.”
Tujitahidi kukithirisha kufanya ibada na kufanya kheri mbalimbali kwani Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) alikuwa akizidisha kheri nyingi katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Imepokewa na At-Tirmidhiy kutoka kwa Anas (Allaah Amridhiye), amesema Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani): “Bora ya (wakati wa) kutoa sadaqa ni kutoa katika mwezi wa Ramadhan.”
Ili kuona namna wema waliotangulia walivyoshindana katika kufanya kheri mbalimbali tujifunze katika haya yafuatayo:
Imepokewa na Zayd bin Aslamu kutoka kwa babake, amesema nimemsikia ‘Umar bin Al-Khatwaab (Allaah Amridhiye) anasema: “Ametuamrisha Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) tutoe sadaka nikatoa mali yangu nikasema leo nimemtangulia Abu Bakr nimekwenda na nusu ya mali, akasema Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) kuniambia: “Umewabakishia nini watu wako?” Nikasema, nusu kama hii, na akaja Abu Bakr na mali yake yote. Mtume (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) akamuuliza: “Umewabakishia nini watu wako? Akasema, nimewabakishia Allaah na Mtume wake. Nikasema huyu Abu Bakr hapitiki na kitu chochote Abadan.”
Milango ya Moto inafungwa, Milango ya Pepo inafunguliwa na mashetani wanafungwa:
Moja ya fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni mashetani kufungwa minyororo na milango ya Moto kufungwa na milango ya Pepo kufunguliwa.
Haya tunayasoma katika Hadithi inayopatikana katika vitabu cha Hadithi za Mtume Muhammad –Allaah Amrehemu na Ampe Amani – viitwavyo Sahih Al-Bukhari na Sahih Muslim), kuwa: Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Pindi unapokuja (Mwezi Mtukufu wa) Ramadhwaan inafunguliwa milango ya Jannah (Pepo), na hufungwa milango ya Moto, na mashetani wanafungwa kwa minyororo.”
Mwezi wa Subira:
Subira ni katika jambo gumu na halipati ila kwa mtu mcha Mungu na mnyenyekevu kwa Allaah. Na katika kufunga kunatakiwa subira pale mtu anapojizuilia kutokana na kutokula, kunywa, matamanio na mengineyo.
Imekuwa Swaumu (Funga) ni nusu ya subira na subira malipo yake ni pepo kama tunavyosoma katika Qur’aan Tukufu, Sura ya 39 (Surat Az-Zumar), aya ya 10 kuwa: “Sema: Enyi waja wangu mlioamini! Mcheni Mola wenu Mlezi. Wale wafanyao wema katika dunia hii watapata wema. Na ardhi ya Mwenyezi Mungu ni kunjufu. Hakika wenye subira watapewa ujira wao bila ya hisabu.”
Mwezi wa Kukubaliwa Dua:
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni fursa adhimu ya kuomba Dua na kukubaliwa kama tunavyosoma katika hadithi iliyopokewa na Imaam Ahmad: Kutoka kwa Jaabir (Allaah Amridhiye) kwa isnadi iliyo nzuri, kuwa: Mtume Muhammad (Allaah Amrehemu na Ampe Amani) amesema: “Kila Muislamu Dua zake ni zenye kukubaliwa atakapomuomba katika mwezi wa Ramadhan.”
Tuhitimishe makala hii kwa kukumbusha kuwa ibada ya Swaumu ya Ramadhani inatekelezwa kwa mfungaji kunuia usiku wa kuamkia alfajiri ya kuanza kufunga kuwa ananuia kufunga siku hiyo ikiwa ni miongoni mwa siku za Mwezi wa Ramadhani kwa ajili ya Allaah Mtukufu na baada ya hapo ajizuie na yanayobatilisha (yanayoharibu) Swaumu kuanzia mwisho wa wakati wa kula daku (mwanzo wa alfajiri) hadi wakati wa kuingia Swala ya Magharibi.
Yanayobatilisha (yanayoharibu) Swaumu ni: (1) Kula na kunywa kwa makusudi. Na si kwa kusahau au kwa kulazimishwa, katika mchana wa Swaumu. (2) Kujitapisha kwa makusudi. Kuwe kujitapisha huko kwa kutia kidole mdomoni au kunusa kitu kitachosababisha kutapika. (3) Mume kumuingilia mke wake. Na pia kumkumbatia au kumchezea hadi yakamtoka manii. (4) Kujichua (kuyatoa manii) kwa makusudi ima kwa mkono au kwa kuchezewa na mkeo au kwa njia yoyote ile. (Ama manii hayo yakitoka kwa kuota (ndoto) au kutazama (bila kukusudia), basi haiharibu Swaumu). (5) Kupatwa na hedhi au nifasi kwa mwanamke. Hata kukiwa kutokea huko kuwa ni wakati wa kukaribia kufuturu. (6) Mwenye kutia nia ya kula wakati amefunga, kwa sharti kuwa kaazimia tendo hilo hata kama hakulitekeleza. (7) Kudhania kuwa jua lishazama magharibi au bado hakujapambazuka (yaani haujaanza wakati wa kufunga), kisha akala, akanywa au akamuingilia mke wake.
Tunamuomba Allaah Mtukufu Atuwezeshe kuitekeleza ibada ya Swaumu ya Ramadhani kwa namna inavyopaswa ili tupate radhi zake. Allaahumma Aaamiiin!
Haya tukutane Jumanne ijayo In-Shaa-Allaah.
Sheikh Khamis Mataka ni Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata) na Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
Simu: 0713603050/0754603050