DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu 

Umewahi kumshuhudia Aishi Manula akiwa na siku mbaya ofisini kwake, yaani katika lango la Simba au Taifa Stars? Kwa hakika huwa anatia huruma. Ngoma za masikio yake hupokea kila neno chafu kutoka kwa mashabiki.

Lakini Manula mwenyewe hubaki kimya tu, ingawa kwa ukimya wake haina maana kuwa hasikii, wala haoni. Anasikia na kuona vema kila kinachosemwa juu yake. Busara humuongoza na kuchagua kunyamaza.

Umewahi kuona siku Manula akiwa kwenye kilele cha ubora katikati ya milingoti mitatu ya timu hizo mbili ambazo kwa miaka mingi sasa amekuwa akizitumikia kwa nyakati tofauti?

Kikundi cha watu wachache ndicho hujitokeza kumsifu, lakini kundi kubwa la watu ambalo ndilo humtolea maneno machafu, huwa ni zama yake kukaa kimya. 

Mfano wa karibu umetokea majuzi tu. Ni kama vile mashabiki hawa hawaoni alichokifanya Manula nje ya nchi alipokuwa kazini na Klabu yake ya Simba katika pambano dhidi ya ASEC Mimosas. 

Katika nyakati zote anazopitia; ziwe mbaya au nzuri, Manula amechagua kuwa kimya. Ukimya wake hauna maana hasemi. Huishia kusema na moyo wake. Hawezi kutoka hadharani na kusema.

Haya ndiyo maisha ya Watanzania wengi tuliyoyachagua kuishi na Manula. Akifanya makosa atafananishwa na makipa wa timu nyingine. Atabezwa na watu watasema hafai.

Lakini akifanya vizuri husikii ule ubishi wa nani kipa bora, wala husikii dhihaka dhidi yake. Haya ndiyo maisha ya Watanzania waliyoyachagua kuishi na Manula. 

Manula akiwa katika ubora wake, hakuna kipa anayemsogelea hapa nchini. Mimi huwa ninaamini hivi na namba huwa hazidanganyi. Muda mwingine makosa yanayomtokea kiwanjani ni makosa ya kimchezo ambayo hutokea kwa mwanasoka yeyote yule. 

Shida kubwa tumemgeuza Manula kuwa kama malaika asiyetakiwa kukosea kitu chochote awapo uwanjani. Kila kitu akifanye kwa usahihi. Jamani mpira wa wapi huu?

Mashabiki wa soka na Watanzania wenzangu lazima tujifunze kuwaelewa wachezaji wetu wakiwa na siku mbaya kazini. Lakini sijui kwa nini kwetu inakuwa tofauti! 

Kila siku shabiki anamtaka mchezaji atoe asilimia 100 ya kiwango chake uwanjani. Siku ambayo Manula ataacha kucheza na kutundika glovu zake, huenda ndipo hapo tutakapojua kwamba tulikuwa na kipa wa namna gani. Lakini kwa muda huu acha abezwe tu. 

Juma Kaseja kwa sasa anaondoka polepole katika soka la ushindani, akiliacha lango la Stars katika mikono salama kabisa. Sidhani kama kuna mtu anaweza kushituka siku Kaseja akisema anastaafu soka la kimataifa. Sidhani. 

Unadhani sababu ni nini? Ni kutokana na lango la Stars kuwa kwenye mikono salama ya Manula. Hakuna anayeweza kuhuzunika na taarifa za Kaseja, zaidi tutamuaga kwa heshima, nderemo na vifijo.