*Yatikisa uchumi wa Marekani kwa ngano, mafuta
*Ujerumani yakalia kuti kavu, uchumi hatarini kuporomoka
*Bara la Ulaya linategemea gesi kwa asilimia 40
*Putin abadili gia, auza gesi kwa Ruble, hisa zake zapanda
DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Wakati Rais wa Urusi, Vladmir Putin, akitangaza kumalizika kwa awamu ya kwanza ya ‘operesheni ya kijeshi’ nchini Ukraine, kuna kila dalili kuwa vita hiyo huenda ikasababisha balaa kubwa duniani.
Hofu hiyo inatokana na hatua ya Urusi kuzuia usafirishaji nje ya nchi bidhaa zake muhimu, mbolea na ngano, ikijibu mapigo ya vikwazo vya uchumi ilivyowekewa na Ulaya na Marekani.
Tayari hatua ya Urusi imeleta madhara ya moja kwa moja katika mataifa yaliyokuwa yanategemea kupata bidhaa hizo.
Nchini Marekani, mfumuko wa bei ya chakula, ikiwamo ngano, umepanda kwa kasi kubwa huku hali ya uchumi ikiporomoka na kuleta kero kwa wawekezaji mitaji yao kukatika.
Hata kodi ya pango ya nyumba nchini Marekani nayo imepanda takriban mwezi mmoja sasa, huku wananchi wakilalamika kukosa nyumba bora za kuishi baada ya kupanda kwa gharama za usafirishaji wa vifaa vya ujenzi.
Inaripotiwa kuwa wiki iliyopita baada ya tukio la kulipuliwa kwa kisima cha mafuta nchini Saudi Arabia, bei ya mafuta nchini Marekani imepanda na kusababisha sekta ya usafiri kusuasua.
Wakati hali ikiwa hivyo Marekani, Bara la Ulaya limo katika kipindi kigumu cha kuendesha uchumi ambao kwa asilimia 40 unaendeshwa kwa gesi inayozalishwa Urusi.
Katika hatua ya Putin kuimarisha sarafu yake ya ‘Ruble’, ametangaza kuwa nchi zote ambazo zimeliwekea vikwazo taifa lake zitatakiwa kununua gesi kwa kutumia sarafu hiyo.
Hatua hiyo inapingwa na mataifa ya Ulaya, hasa Ujerumani ambayo kwa sasa inakabiliwa na mgawo wa gesi, ikilenga kupunguza matumizi ya nishati hiyo ambayo inaipata kwa wingi kutoka nchini Urusi.
Ujerumani inadai kuwa si kazi rahisi kununua gesi nchini Urusi kwa kutumia Ruble kwa sababu tayari ilikuwa kwenye makubaliano na taifa hilo kununua gesi kwa kutumia sarafu ya Euro.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Chritian Linder, amekaririwa akiwashauri wasambazaji wa gesi nchini humo kutonunua gesi ya Urusi kwa kutumia Ruble.
Anasema sharti la Urusi linalenga kukuza uchumi wake na kuimarisha sarafu ya ‘Ruble’ huku akidai kuwa kuna umuhimu wasambazaji wa nishati hiyo kuendelea kuzingatia makubaliano ya mkataba wa awali wa ununuzi wa gesi nchini Urusi.
Akihutubia Bunge la Ufaransa kwa njia ya video, Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amezilaumu kampuni za Ufaransa ambazo bado zinaendesha shughuli za uzalishaji nchini Urusi, akisema kitendo hicho ni kuipa nguvu Urusi ya kuendesha vita.
Na sasa, EU na Marekani wamesaini makubaliano ya kusambaziana gesi, ikiwa ni mkakati wa kujiondoa kwenye utegemezi wa Urusi na kupambana na mfumuko wa bei ya gesi.
Pamoja na kufikia hatua hiyo, barani Ulaya zipo nchi zinaonyesha kusita kujiondoa moja kwa moja kwenye soko la biashara inayohusisha taifa la Urusi.
Wakati mataifa ya Ulaya na Marekani yakipambana kudhibiti mfumuko wa bei za vitu, Urusi imefungua soko lake la hisa na mauzo ya hisa kuripotiwa kupanda kwa silimia 4.4 baada ya kuwa limefungwa kwa takriban mwezi mmoja.
Awali Urusi ilifunga soko hilo ikilenga kutathmini hali ya vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa na mataifa yanayoishinikiza kusitisha operesheni hiyo ya kijeshi nchini Ukraine.
Kupanda kwa mauzo ya hisa kwenye soko la hisa la taifa hilo kunatokana na mauzo ya mafuta na gesi inayopata kutokana na kuuza bidhaa hizo kwa kutumia sarafu yake ya Ruble.
Kauli tata ya Biden
Wiki iliyopita Rais wa Marekani, Joe Biden, amefanya ziara barani Ulaya na kukutana na viongozi wa mataifa saba duniani yaliyoendelea kiviwanda (G7), Umoja wa Kujihami wa NATO, na Umoja wa Ulaya na kujadiliana namna ya kujibu uvamizi wa majeshi ya Urusi nchini Ukraine.
Baada ya mkutano huo, G7 wameafikiana kuzuia matumizi ya dhahabu ya Benki Kuu ya Urusi katika shughuli za malipo.
Urusi inadaiwa kuhodhi takriban dola bilioni 130 katika akiba ya dhahabu, hazina hiyo ikitajwa kuhifadhiwa kwa miaka mingi.
Katika hali inayoonyesha kuwa taifa hilo lilikuwa limejipanga kwa hatua ambazo mataifa hasimu yangechukua dhidi yake, Februari 28 lilitangaza kuanza kununua tena dhahabu kwenye soko la ndani la madini.
Uingereza pamoja na Marekani zenyewe zimeendelea na mkakati wa kutumia vikwazo kudhibiti Urusi huku Marekani ikitangaza vikwazo vipya vikiwalenga watu binafsi na matajiri wa Urusi wapatao 400, wakiwamo wanachama 300 wa Bunge la Urusi (Duma).
Mkutano wa viongozi hao uliowakutanisha mjini Brussels nchini Ubelgiji, Rais Biden alisisitiza kuwa ni lazima Urusi italipa gharama kubwa.
Akiwa nchini Poland, nchi iliyo karibu na mpaka wa Ukraine, Rais Biden alipokwenda kuzuru majeshi ya taifa lake na kusalimiana na wakimbizi kutoka Ukraine amemlaumu Putin, na kudai kuwa hawezi kudumu madarakani, kauli iliyozua utata nchini Urusi na Marekani pia.
Serikali ya Urusi imekaririwa ikisema taifa hilo ni huru na haliwezi kupangiwa utawala na Marekani; huku Msemaji wa Ikulu ya Marekani akijibu kwa kusema kauli ya Biden haikumaanisha kuupindua utawala wa Putin.
Baada ya kauli hiyo, inaripotiwa kuwa majeshi ya Urusi yameongeza mashambulizi nchini Ukraine, ambapo kwa kutumia roketi yameushambuliwa mji wa Lviv, mji uliokuwa umebakia nchini Ukraine bila kushambuliwa.
Rais Zelensky kwa mara nyingine ameyaomba mataifa ya Magharibi kumuongeza silaha za kivita, zikiwamo za kudhibiti anga la Ukraine.
Hali ya vita kwa sasa
Saa chache baada ya Rais Biden kuizuru Poland, takriban wakimbizi 48,450 waliokuwa kwenye mji wa Lviv wamekimbilia nchini Poland, wakikimbia mashambulizi ambayo yameanza kuelekezwa katika mji huo.
Kabla ya shambulizi hilo, mji wa Lviv ulikuwa na watu 200,000 ambao miongoni mwao ni waliokimbilia eneo hilo kutoka maeneo mengine ya Ukraine yanayoshambuliwa na majeshi ya Urusi.
Mji wa Lviv awali ulikuwa haujashambuliwa na majeshi ya Urusi baada ya kuuacha kama sehemu maalumu ya wananchi wanaoikimbia Ukraine kupita hapo.
Hadi sasa kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Wakimbizi Duniani (UNHCR), jumla ya wananchi milioni 3.8 wamekwisha kuikimbia Ukraine na miongoni mwao jumla ya watu milioni 2.2 wamekimbilia nchini Poland.
Tangu ilipoanza operesheni hiyo, Februari 24, mwaka huu, jumla ya vifo vya raia 1,081vinaripotiwa kutokea nchini Ukraine na kusababisha majeruhi 1,707.
Kwa upande mwingine, Urusi imedai kuanza mkakati wa kuyalinda maeneo ambayo imeyateka kutoka Ukraine, ambapo Jimbo la Luhansk limedai kuwa hivi karibuni litapiga kura ili wananchi wake waamue iwapo wanakubali kujiunga upande wa Urusi, huku Ukraine ikipinga hatua hiyo ikidai kuwa haina uhalali.
Jimbo jingine ambalo limo mbioni kujiunga na Urusi ni Donetsk. Haya yatakuwa yameongeza idadi ya majimbo yanayojiunga na Urusi kufikia matatu, baada ya mwaka 2014 Jimbo la Crimea kumegwa kutoka Ukraine na kujiunga na Urusi.