DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Mwaka 1995 Dk. John Pombe Magufuli aliamua kuingia katika duru za siasa na kugombea ubunge Jimbo la Biharamulo Mashariki mkoani Kagera.

Agosti 23, 1995, Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilitangaza majina ya wagombea ubunge na uwakilishi wa majimbo mbalimbali nchini, jina la Magufuli likiwa miongoni mwa majina hayo.

Dk. Magufuli aliyeonekana mchanga katika siasa alishinda ubunge katika jimbo hilo linaloelezwa kuwa na wanasiasa wakongwe kutokana na uchapa kazi wake na nidhamu ya hali ya juu katika utumishi.

Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 1995, Dk. Magufuli aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, nafasi aliyoihudumu kwa miaka mitano.

Akiwa na nafasi hiyo ndani ya Serikali ya Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa, Dk. Magufuli alifanya kazi kwa weledi mkubwa na kuleta matumaini kwa Watanzania.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, akagombea tena ubunge katika jimbo hilo na kuibuka na ushindi wa kishindo; baadaye akateuliwa kuwa waziri kamili wa ujenzi.

Ni ukweli kuwa Wizara ya Ujenzi ndiyo iliyomjengea jina na kumletea sifa kwa wananchi baada ya kufanya kazi kubwa iliyoacha alama za maendeleo makubwa ya miundombinu kuwahi kutokea tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961.

Kutokana na uchapa kazi uliotukuka kwa miaka 10 ya Awamu ya Tatu, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alimteua kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Ardhi na baadaye Waziri wa Ujenzi.

Baada ya kudumu kwa miaka 20 katika Baraza la Mawaziri, Dk. Magufuli alijizolea umaarufu mkubwa katika utumishi wake ambao wakati wote hakuwahi kukumbwa na kashfa yoyote ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyo kwa baadhi ya watumishi wengine.

Mwaka 2015, Dk. Magufuli alikuwa ni miongoni mwa wanachama wa CCM waliochukua fomu kuwania nafasi ya Rais wa Tanzania kwa tiketi ya chama hicho.

Ni mwaka ambao ulikuwa na ushindani mkali ndani ya CCM kumpata mpeperusha bendera katika urais. Ni mwaka ambao baadhi ya wagombea wa nafasi hiyo waliokuwa na nguvu na majina makubwa waliamua kuhamia upinzani na baadaye kurejea CCM.

CCM ilimpitisha Dk. Magufuli kuwania nafasi ya Urais kutokana na uadilifu wake, utumishi usio na shaka na zaidi sifa ya kuchukia na kupiga vita ufisadi na rushwa.

Katika kampeni akinadi sera na Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Dk. Magufuli aliahidi kuwashughulikia mafisadi na wala rushwa wakubwa.

Alijenga mahakama ya wahujumu uchumi, kusimamia nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, kuboresha huduma za kijamii na kutekeleza kwa vitendo sera ya Tanzania ya viwanda.

Novemba 5, 2015, Dk. Magufuli aliapishwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete.

Baada ya kula kiapo, Rais Magufuli aliwashukuru Watanzania kwa kumpa ridhaa ya kuongoza nchi na kuwahakikishia dhamira yake ya kuwatumikia na kuwaletea maendeleo huku akibainisha kwamba maendeleo hayana chama.

Tofauti na ilivyozoeleka baada ya kuingia Ikulu, Rais Magufuli akaanza ziara za kushtukiza zilizowafanya watumishi wa umma wa sekta na idara mbalimbali kukaa mguu sawa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Siku moja baada ya kuapishwa; yaani Novemba 6, 2015, Dk. Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza Wizara ya Fedha na Mipango, akienda kwa mguu kukutana na kuzungumza na watumishi wa Hazina.

Alifanya ziara ya kushtukiza pia Hospitali ya Taifa Muhimbili kujionea uendeshaji wake.

Mei 14, 2016 akitokea Uganda, akatembelea kwa kushtukiza Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Februari 8, 2017 alifanya ziara nyingine ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa jengo la tatu (Terminal III) la JNIA na kuagiza ujenzi huo uendelee kwa kasi zaidi.

Katika kuhakikisha watumishi hawafanyi kazi kwa mazoea, Mei 15, 2018 alifanya safari ya kushtukiza katika Bandari ya Dar es Salaam na kukagua matanki ya mafuta ya kula yaliyokuwa yameadimika.

Mbali na ziara za kushtukiza, Dk. Magufuli alitumia muda mwingi kufanya ziara za ndani kukagua, kuelekeza na kutoa maagizo mbalimbali ya maendeleo.

Katika kipindi cha kwanza cha miaka mitano, alifanikiwa kuanzisha miradi mikubwa ya kimkakati ya maendeleo, ufufuaji wa Shirika la Ndege (ATCL), utekelezaji wa sera ya viwanda, kuboresha mikataba ya madini na serikali kuhamia Dodoma.

Kwa mara ya kwanza, Aprili 12, 2017 Rais alizindua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ambao unaendelea kwa kasi. Reli hiyo yenye urefu wa kilometa 1,219 kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza, inaelezwa kukamilka katika baadhi ya maeneo.

Matarajio makubwa aliyokuwa nayo Dk. Magufuli aliyaonyesha Novemba 13, 2020, alipofungua Bunge la 12 na

kusema serikali itakamilisha ujenzi wa kilometa 2,500 za barabara za lami; ujenzi wa madaraja ya Kigongo – Busisi (Mwanza ) na la Tanzanite, Dar es Salaam.

Julai 26, 2019, Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa megawati 2,115 katika Bwawa la Mwalimu Nyerere (Stigler’s Gorge).

Katika kipindi cha miaka mitano, serikali ilinunua ndege kubwa za kisasa 11, hatua inayoongeza tija katika usafiri wa anga nchini na kimataifa.

Serikali ikafikisha umeme katika vijiji 9,112 hadi mwaka 2020 kwa kutumia Sh trilioni 2.27; ikajenga vituo vya afya 400, hospitali za wilaya 70 na za rufaa 10. Haya ni maendeleo makubwa yaliyofikiwa na Tanzania chini ya Magufuli.

Juni 11, 2020 wakati akivunja Bunge la 11 jijini Dodoma, pamoja na mambo mengine, Dk. Magufuli alieleza mafanikio ya serikali akisema imejenga viwanda vipya 8,477; vikubwa 201, vya kati 460 na vidogo 3,406, hivyo kuongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015 hadi 61,110 mwaka 2020.

Tofauti na matarajio, Julai 1, 2020, Benki ya Dunia ilitangaza Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zilizoingia katika uchumi wa kati.

Novemba 2020, Rais Magufuli aliapishwa kuongoza nchi kwa kipindi cha pili baada ya kupata ushindi wa asilimia 84.4 katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Katika hatua nyingine, Novemba 1, 2020, Magufuli aliwashukuru Watanzania kwa kumchagua tena yeye na

Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, akisema kipindi hicho kitakuwa cha mwisho cha utawala wao.

Tamaa ya madaraka imekuwa tatizo kubwa kwa baadhi ya viongozi Afrika. Tumeshuhudia machafuko na mageuzi ya uongozi kutokana na baadhi ya watawala kung’ang’ania madaraka.

Rais Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021, kwa nyakati tofauti alikuwa akitoa msimamo wake wa kutobaki madarakani mara muda wake utakapokwisha kwa mujibu wa Katiba.

Desemba 18, 2019, akiwa Chato, alisema kwa kuzingatia sheria na Katiba ya nchi hategemei kuongeza hata siku moja baada ya kumaliza muda aliopewa kikatiba akisisitiza kuwa angeondoka kumpisha mwingine.

“Sitegemei kuongeza hata siku moja baada ya kumaliza muda wangu, kwa sababu muda nitakaokuwa nimepewa kwa mujibu wa Katiba ndio nitakaokuwa nimepewa na Mungu kuwatumikia Watanzania,” alisisitiza Magufuli.

Mwaka mmoja bila Dk. Magufuli, Watanzania tunapaswa kumuenzi kwa kuchapa kazi, uadilifu, uzalendo na kutanguliza masilahi mapana ya nchi yetu.

Ametuachia somo la kujifunza kuchapa kazi kwa maendeleo ya taifa, na wenye dhamana za uongozi watumie nafasi zao kwa manufaa ya umma.

Stuwart Samandalo wa Ngaramtoni, Arusha, amesema Rais Magufuli alipigania maendeleo ya Watanzania na wakati wote alimtanguliza Mungu katika kutekeleza majukumu yake.

“Alidhamiria na kufanikiwa kuleta maendeleo makubwa kwa Watanzania. Pia alimtanguliza Mungu katika kutekeleza majukumu yake. Hatuna budi kuyaenzi hayo yote kwa mustakabali wa nchi yetu,” anasema Samandalo.

Machi 17, mwaka huu, Rais Samia amewahakikishia wana Chato kuwa atamuenzi Dk. Magufuli kwa kutekeleza miradi yote aliyoiasisi.

“… miradi yote hata ambayo sijaitaja ili kumuenzi mpendwa wetu, Dk. John Magufuli,” anasema Samia.

0755-985966