Morogoro

Na Everest Mnyele 

Wiki iliyopita tulizungumzia umuhimu wa kuwa na Katiba mpya ya umma. Ninajua kuwa kuna wataalamu wengi wameandika juu ya umuhimu wa kuwa na katiba thabiti ya umma. 

Nia yangu ni kuendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na katiba thabiti ya umma. 

Ninatumaini kuwa lugha rahisi ninayotumia itawafanya wengi kunielewa tofauti na wataalamu nguli wa masuala ya katiba kama akina Profesa Issa Shivji.

Inawezekana pia wakati wataalamu nguli walipokuwa wakiandika uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa katiba thabiti ya umma ulikuwa duni tofauti na sasa, hasa baada ya kutokea matukio kadhaa ambayo hatukuwa tumeyazoea. 

Sasa uelewa ni mpana hadi vijijini kwani shule za kata zimesaidia kuondoa ukungu na kuwafanya Watanzania kuanza kuona mwanga wa umuhimu wa kuwa na katiba thabiti ya umma. 

Kwa maana hiyo, wasomi wetu hao ngazi ya kata watakuwa chachu ya kuwaelimisha wengine na kuibua mjadala mpana kuhusu kuwa na katiba thabiti ya umma.

Tuanze kwa kukubaliana kwamba, ni ukweli usiopingika kuwa na katiba ambayo haikutokana na matakwa ya wananchi kunaweza kuwa chanzo cha kudumaza maendeleo.

Hii inatokana na ukweli kuwa sheria na taratibu za utawala, sera na mambo mengine muhimu hutegemea ‘sheria mama’ ili kuendeshwa. 

Tunaweza kujidanganya na kujivuna kwamba tuna katiba na mambo yanakwenda sawasawa, lakini kwa kweli mambo yangeweza kwenda vizuri zaidi kama tungekuwa na katiba inayotokana na wananchi watakayoamua kuifuata kama mwongozo wa maisha yao. 

Hivyo ni muhimu wananchi kuimiliki katiba yao. Kuwapo kelele nyingi za kudai katiba ni ishara kuwa katiba ya sasa haitoshi. Kelele hizi wala hazijaanza jana!

Ni busara kufika mwisho na kupata katiba inayotokana na umma. Kuwa na katiba kama iliyopo sasa husababisha kuwapo kwa serikali na taasisi zisizofanya kazi kwa misingi ya haki, usawa na uwazi; hivyo kuleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi. 

Sasa viongozi waliopo madarakani, wasomi na viongozi wa taasisi mbalimbali kwa pamoja waone umuhimu wa kuwa na katiba inayotokana na wananchi ambayo itachochea maendeleo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Tunaweza kusema; mbona tuna maendeleo? Lakini tukubaliane kuwa katiba mbovu inaweza kusimamisha shughuli nyingi za wananchi za kujiletea maendeleo.

Tuna sheria ya kuwaweka watu kizuizini, sheria za viongozi wa serikali kuwaweka watu ndani kwa sababu binafsi kwa kigezo cha kuhatarisha amani. 

Sheria kama hizi zinatoa mwanya kwa viongozi wenye nia ovu kuzitumia vibaya.

Kabla sijaendelea, nitoe mfano. Bunge limepewa mamlaka kikatiba kumuondoa Rais madarakani kwa wabunge theluthi mbili kupiga kura ya kutokuwa na imani naye, lakini kwa upande mwingine Rais ana mamlaka ya kulivunja Bunge wakati wowote! 

Katiba ya namna hii inaweza kumfanya Rais aonekane ‘mungu mtu’.

Katika hali kama hii hamuwezi kutiana adabu (checks and balance), maana Rais ana nguvu kubwa kuliko Bunge linalotokana na wananchi linalofanya kazi kama timu. 

Katiba thabiti ingeishia kulipa Bunge nguvu ya kumuondoa Rais kwa kura ya kutokuwa na imani naye na Rais akaondoka; kwisha. 

Hii ingeleta maana ya kuwapo kwa ‘mgawanyo wa madaraka’ kati ya mihimili mitatu ya Serikali (Rais), Bunge (Spika) na Mahakama (Jaji Mkuu). 

Pili, katika uchaguzi wetu matokeo ya urais yakishatangazwa hayapingwi katika mahakama yoyote hata kama mshindi amepatikana kwa njia isiyofaa. 

Wakati huo huo matokeo ya ubunge na udiwani yanapingwa mahakamani, hii ni ‘double standard’ na sheria ya namna hii inaweza kutumiwa vibaya na watu wenye nia ovu na nchi yetu.

Kwa mifano hii tunaweza kuona zaidi sababu ya kuwapo madai ya katiba mpya itakayotokana na wananchi.

Katiba iliyopo inampa Rais madaraka na nguvu kubwa sana inayoweza kumshawishi kuwa dikteta (haya si maneno yangu, bali ya muasisi wa taifa na wa katiba iliyopo, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere). 

Hivyo si afya kwa nchi katika karne hii kuwa na katiba inayotoa mamlaka makubwa kiasi hiki kwa kiumbe, binadamu ambaye si malaika.

Jambo jingine kwenye taasisi ya urais ni mamlaka makubwa ya uteuzi. Rais ateue Jaji Mkuu na majaji; ateue Mkurugenzi wa Uchaguzi, wakuu wa mikoa, wilaya, ma-DAS, wakurugenzi wa halmashauri na wengine wengi!

Tuwe wa kweli, hivi kwa mzigo huu wa uteuzi tutapata viongozi waadilifu waliopimwa kwa rekodi zao za utendaji na uadilifu? 

Ni ukweli usiopingika kwamba Rais atachomekewa marafiki, ndugu na maswahiba wa watu wanaomzunguka. 

Kwa mantiki hii ni vema kuwa na katiba inayotoa utaratibu wa wazi wa uteuzi unaofanywa na Rais, nje ya hapo itatuchukua miaka mingi nchi kutokufikia malengo yake kwa sababu ya kuwa na wateule wasiopimwa kwa sifa, uwajibikaji nk.

Nalisema hili kwa sababu tunapaswa kuwa na viongozi bora kabisa kutoka miongoni mwetu kwa ajili ya kutuletea matokeo bora. 

Ni vema tukajifunza kwa wenzetu wanatumia njia gani kuwapata watu wazuri kushika nafasi nyeti na si kuteuateua tu.

Uimara wa nchi na taasisi zake unategemea katiba madhubuti. Kuwapo kwa taasisi imara zinazoendeshwa kwa mujibu wa katiba na sheria za nchi kutasaidia kuondoa dhana ya viongozi au wateule kuongoza na kuendesha baadhi ya taasisi kama wanavyotaka, hii ni hatari sana katika ustawi wa taifa.

Tukumbushane kwamba tuna ya Serikali, Bunge na Mahakama yenye taasisi nyingi chini yake. 

Hivyo, mihimili hii inapaswa kuwa huru kabisa kwa kupewa nguvu kikatiba. 

Kusiwepo wakati mhimili mmoja unaingilia uamuzi wa mihimili mingine bila utaratibu na kuyumbisha mwelekeo wa nchi (tunakumbuka sakata la hivi karibuni na kilichotokea). 

Tiba ya kutoingiliana mihimili ni kuwa na katiba ya umma madhubuti na nchi itakuwa tamu kuongoza, kwani nchi ni yetu sote, kama Rais asemavyo na kurudia mara kwa mara.

Nipende kuwatoa hofu na kuwahakikishia kuwa nchi yoyote ambayo mihimili hufanya vema na kwa kadiri ya matarajio ya watu wake yaliyo kwenye katiba, imani ya wananchi kwa serikali yao, Bunge na Mahakama ni kubwa sana. Nje ya hapo ni kelele tupu.

Chini ya mihimili kuna taasisi kama jeshi, polisi, usalama wa taifa, Tume ya Uchaguzi na nyingine nyingi. 

Kuwapo kwa taasisi imara ni kichocheo kikubwa cha maendeleo. Katiba inapaswa kuweka wazi muundo na uendeshwaji wa taasisi hizo na kuzitungia sheria, kwani taasisi hizi ndizo hufanya kazi moja kwa moja na wananchi. 

Hivyo taasisi zinapaswa kufanya kazi zake kwa haki, usawa bila upendeleo wowote kiasi cha kuwafanya wananchi kuwa na imani kubwa na huduma wanazopata kwa taasisi husika. 

Nje ya hapo uhusiano kati ya serikali na taasisi zake huzorota na kuleta manung’uniko na kukata tamaa.