Mafundisho ya Mt. Yohane Paulo II (Papa)
19. Mt. Yohane Paulo II (Papa) aliona umuhimu wa upatanisho kwa Kanisa na kwa ulimwengu mzima.
Papa aliona upatanisho kama njia ya kuuponya ulimwengu uliovunjika kutokana na mgawanyiko katika uhusiano kati ya watu binafsi na kikundi; mataifa dhidi ya mataifa na kambi za nchi zinazopingana katika kutawaliwa.
Mgawanyiko huu hutokea kwa sababu ya kukanyaga haki za kimsingi za binadamu, mfano haki za kuzaliwa kama ile ya kuishi na maisha bora; ubaguzi wa rangi, tamaduni na dini; vurugu, vita na mafarakano.
Aidha, ndani ya Kanisa pia kumeshuhudiwa migawanyiko kwa sababu ya maoni tofauti katika nyanja za mafundisho na kichungaji. Haya yote yanahitaji upatanisho.
20. Mt. Yohane Paulo II (Papa) aliona hamu ya upatanisho wa dhati kuwa ni nguvu ya msingi katika jamii yetu. Hamu hii ya upatanisho, na upatanisho wenyewe ni fursa ya kuponya jeraha la asili ambalo ni shina la vidonda vingine vyote: yaani dhambi.
21. Papa Yohane Paulo II alionyesha uhitaji huu wa upatanisho wakati wa Maadhimisho ya Yubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo pale alipoomba msamaha kwa makosa ya Kanisa kama Vita ya Msalaba (Crusades), Baraza la Kuhukumu Wazushi na makosa dhidi ya Wayahudi.
Papa Yohane Paulo II alisema: “Tunaomba msamaha kwa unyenyekevu kwa sehemu ambayo kila mmoja wetu na tabia zake alishiriki katika maovu kama hayo na kuchangia kuvuruga sura ya Kanisa. Wakati huo huo tunapokiri dhambi zetu, tunasamehe yaliyofanywa na wengine kwetu.”
Aidha, Papa Yohane Paulo II aliongeza kusema kwamba: “Upatanisho wa kweli haupatikani kwa kuwatesa waliotuumiza bali hupatikana kwa kuwapenda kwa vitendo.”
Kauli hii ya Papa Yohane Paulo II ilithibitishwa na yeye mwenyewe pale alipomsamehe mtu aliyetaka kumuua kwa kumpiga risasi, akamtembelea gerezani, kumsalimia na kumwonyesha upendo kwa vitendo.
22. Haya ni maneno yenye mwangwi wa upatanisho, upatanisho kati ya Kanisa na Mungu na Kanisa na wanajamii. Ni sauti ya unyeynyekevu ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa; na kwamba sisi sote tunahitaji kusamehewa na wengine, kwa hiyo tunapaswa kuwa tayari kusamehe. Kwa lugha nyingine tunahitaji kupatanishwa.
Mafundisho ya Papa Fransisko kuhusu Upatanisho
23. Papa Fransisko anaongelea Upatanisho kama dhana muhimu katika kuishi kindugu; na kwamba kunahitajika njia za kuelekea amani na kuponya majeraha.
Hivyo kadiri ya Papa Fransisko kunahitajika watengeneza amani, wake kwa waume waliojiandaa kufanya kazi kwa ujasiri na ubunifu ili kuanzisha michakato ya uponyaji na makutano mapya.
Upatanisho na undugu kwetu hauna budi uwe ni chemchemi ya utu na undugu uliomo katika Injili ya Yesu Kristo. Kama ndugu tunatakiwa kuvuka mipaka na kujenga madaraja ya kuleta amani na upatanisho.
Baba Mtakatifu Fransisko akitumia aya za Mwinjili Matayo (taz. Mt 5:20-26), anasema kwamba Yesu anatualika kwenye ‘upatanisho kamili’, anatamani upatanisho wenye nguvu.
Ili kufikia upatanisho huo, Papa anasema kwamba Yesu anatumia hekima ya kibinadamu katika kujadiliana na wanafunzi wake. Ili kuendesha mafundisho yake kuhusu uhusiano wa upendo na upatanisho, Bwana anatumia mifano ya kila siku ya maisha ya watu.
24. Mama Kanisa anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika Sakramenti ya Upatanisho kama mahali muafaka pa kuonja huruma na upendo wa Mungu, tayari kusimama tena na kuendelea na safari ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani!
Baba Mtakatifu Fransisko anawakumbusha mapadri waungamishaji katika sakramenti ya upatanisho kwamba, wao ni vyombo vya upatanisho, huruma na upendo wa Mungu na kamwe si wamiliki wa dhamiri za waamini.
Wajenge utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, ili wawasaidie waamini wao kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu maisha na wito wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.
25. Baba Mtakatifu Fransisko, Machi 9, 2018 alipofanya Ibada ya Upatanisho wa jumla katika Kanisa la Mtakatifu Petro, aliwakumbusha waamini kwamba, ni upendo wa Mungu unaowafanya kuwa watoto wapendwa wa Mungu, kiasi hata cha kuvuka udhaifu na upungufu wa kibinadamu yanayoisuta dhamiri nyofu.
Huu ni upendo usiokuwa na mipaka wala vizingiti kama vinavyoweza kuwekwa na binadamu kwa hofu kwamba pengine uhuru wao utamezwa.
26. Kadiri ya Baba Mtakatifu Fransisko, dhambi inamtenganisha mwamini na Mwenyezi Mungu, lakini Mungu mwenyewe anaendelea kuwa mwaminifu na karibu zaidi kwa watoto wake.
Uhakika huu, uwe ni dira na mwongozo wa maisha ya waamini kukimbilia na kuambatana daima na upendo wa Mungu katika maisha yao.
Neema ya Mungu inaendelea kutenda kazi ili kuwaimarisha waja wake katika fadhila ya matumaini, ili kamwe wasitindikiwe na upendo licha ya dhambi wanazotenda kwa kukataa kutambua uwepo wake katika maisha yao.
Ni matumaini haya yanayowasukuma waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ni mahali gani ambapo wameteleza na kuanguka kama alivyofanya Mtakatifu Petro baada ya kumkana Yesu mara tatu, akasutwa na dhamiri yake kwa kuyakumbuka maneno ya Kristo Yesu kwamba, angemkana mara tatu! (taz. Mt 26:33-35, 74-75).
27. Papa Fransisko katika nafasi mbalimbali amehimiza na kuonyesha umuhimu mkubwa wa upatanisho na jinsi unavyoweza kuwa kiungo cha fadhila nyingine.
Ujumbe wa Papa Fransisko Machi 1, 2020 kwa Siku ya 53 ya Amani Duniani unaoitwa Amani kama Safari ya Matumaini: Mazungumzo, Upatanisho na Wongofu wa Kiikolojia; unathibitisha amani kama tumaini na matarajio ya familia nzima ya binadamu, na unachunguza umuhimu wa mazungumzo, upatanisho na wongofu wa kiikolojia katika safari ya kuelekea amani.
Kristo Yesu, Bwana na Mwalimu aliyasadaka maisha yake kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za binadamu.
Waamini wanaalikwa kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kutambua ukuu wa upendo wake unaosamehe na kufuta dhambi zote!
Daima wakimbilie huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao ili aweze kuwatakasa na kwa njia hii, wataweza kuonja upendo wa Mungu katika maisha yao.
Itaendelea…