Rais Samia Suluhu Hassan ametimiza mwaka mmoja tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kifo cha Dk. John Magufuli.
Taifa, kama familia, linapoondokewa na kiongozi mkubwa kwa kawaida huibuka shaka na sintofahamu miongoni mwa wananchi. Kwa Watanzania hali ilikuwa tete – wengi wakijiuliza hali itakuwaje?
Lakini kadiri siku zinavyokwenda ndivyo Watanzania wanavyoendelea kuona umahiri wa Rais Samia. Pamoja na kipaji chake cha uongozi, Rais Samia ameendelea kupita kwenye nyayo za misingi ya uongozi wa kitaifa kadiri ilivyojengwa na viongozi wa awamu zote zilizopita. Haikushangaza kuona uhamishaji madaraka kwa mujibu wa Katiba yetu ukifanyika kwa amani na utulivu.
Siku 365 si nyingi, lakini zinatosha kumpima aina ya kiongozi tuliye naye. Ndani ya muda huu mfupi Rais Samia ameonyesha kwa dhati kabisa nia yake ya kuleta matumaini mapya kwa Watanzania. Tutakuwa hatutendi haki tusiposema ukweli kwamba kwa wakati fulani Watanzania walionekana si watu wenye furaha hata kidogo.
Kulijitokeza genge la watu waliotumia maguvu kudai kodi, kupora utajiri wa nchi, kufanya mauaji, kujeruhi watu, kubambikiana kesi zisizo na ushahidi wa kutosha, na kadhalika. Haya na mengine yaliwafanya watu wakawa waoga na wengine wakadiriki kuikimbia nchi.
Ndani ya mwaka mmoja tunaona hayo mambo yakitoweka moja baada ya jingine. Matumaini na furaha miongoni mwa Watanzania vimeanza kujitokeza.
Pamoja na mafanikio makubwa ya kiuchumi, kidemokrasia na haki za binadamu tunayoendelea kuyashuhudia, tunao wajibu wa kuwapa hadhari wale wote waliojipanga kutumia kivuli cha kumsifu Rais wetu kama ngao ya kutenda maovu.
Tumeona awamu iliyopita kuna magenge yalijipachika kazi ya kusifu huku nyuma ya pazia wahusika wakitumia mwanya huo kufanya uovu. Tunatumia fursa hii kuuhadharisha uongozi wa juu kuwa makini na magenge ya aina hiyo ambayo kwa kawaida huwa hayakosekani katika utawala wowote.
Tuendelee kumsaidia Rais Samia kwa kumwonyesha wapi kunahitajika nguvu au msukumo wake. Tuendelee kuonyesha udhaifu katika maeneo ya elimu, afya na huduma za jamii kwa jumla ili kwa mamlaka yake aweze kuyapatia ufumbuzi. Tusijaribu kumficha mambo ambayo tunaamini akiyajua atayarekebisha. Kwa ufupi tunasisitiza tuwe wakweli na tulio tayari kumsaidia kwa kutekeleza wajibu wetu.
Mara zote amesisitiza uchapaji kazi. Tunaamini ni kwa njia hiyo pekee tunaweza kubadili maisha yetu ya mtu mmoja mmoja, kaya na hatimaye taifa zima.
Hongera sana Rais Samia. Bado mapema, lakini tukiri kuwa kazi uliyokwisha kuionyesha inakufanya ustahili pongezi kutoka kwa wapenda maendeleo wote nchini. Tunakuahidi ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha tunakuwa na Tanzania yenye haki, amani, upendo, usawa na mshikamano. Mungu akubariki sana.