Nianze kwa kumpongeza kiongozi wetu Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza mwaka mmoja madarakani.
Mwaka mmoja ni muda mfupi, lakini kiongozi wetu amethibitisha nia yake njema ya kuwa na Tanzania yenye kukonga nyoyo za wengi. Hatuna budi kumuunga mkono na kumsaidia kila mmoja kwa nafasi yake. Mungu aendelee kumbariki.
Baada ya hiyo bashrafu niseme kuwa kuna video imesambaa ikimwonyesha mkuu wa wilaya mojawapo nchini akisema yeye hana mpango wa kuwakamata wanywa bia (pombe) kwa sababu wanachangia kwenye pato la uchumi wa nchi.
Anasema yuko tayari yeye na polisi waende kuwalinda hao wanywaji ili wawe salama, na kamwe asingependa kuona wakibughudhiwa. Bahati nzuri au mbaya yeye mwenyewe hanywi!
Inawezekana maneno ya DC huyu yakaonekana ya kuchekesha, na pengine ya kuudhi hasa kwa wale wanaodhani pombe si kinywaji kinachostahili kuenziwa.
Maneno ya kiongozi huyu yamenikumbusha visa viwili nilivyokutana navyo. Kisa cha kwanza kilikuwa mwanzoni mwa miaka ya 1990 ambako polisi wenye silaha za moto waliingia katika ukumbi wa disko saa 5 usiku na kutufukuza.
Sababu ilikuwa kwamba wanafanya hivyo kwa kuwa kuna wezi waliingia siku kadhaa zilizopita na kuiba nyumbani kwa mkuu wa mkoa. Fikiria, vibaka wanaingia kwa mkuu wa mkoa, lakini wanaoadhibiwa ni vijana wanaofurahia ujana wao.
Kisa cha pili kilitokea kijijini Butiama kwenye mkesha wa Krismasi ya mwaka jana. Rafiki yangu mlemavu ana ki-sehemu anauza vinywaji. Basi, siku hiyo akijua ni mkesha wa sikukuu kubwa, aliendelea kuweka muziki na vinywaji hadi saa 7 usiku kabla polisi wa doria hawajamkamata yeye na wateja wake. Alinipigia simu akipelekwa kituoni. Saa 10 alfajiri nilifika kituoni, lakini mlango ukawa umefungwa na sauti ya askari ikijibu kutokea ndani! Asubuhi nilifika kumdhamini. Nikawakuta watuhumiwa wa aina yake wapo wengi. Wamekamatwa na miziki yao. Polisi wakawa waungwana kwa kuwaruhusu wajidhamini.
Unaweza kuwalaumu polisi hasa wanapogeuza matukio ya aina hii kuwa biashara. Polisi hawana kosa, ingawa kimsingi tungetarajia watumie uungwana na busara zaidi. Polisi hawana kosa kwa sababu leseni za vileo zimeweka ukomo wa muda. Hapa ndipo kwenye tatizo.
Nayasema haya si kwa sababu ya kutetea tuwe na jamii ya walevi au watu wanaoshinda na kukesha baa, la hasha! Najaribu kuangalia sheria zetu kuu na ndogo ndogo zinaathiri vipi maendeleo yetu. Kwa mfano, huyu rafiki yangu mlemavu baa yake iko barabarani – njia kuu ya Tarime – Musoma – Mwanza.
Barabara hii inafanya kazi saa 24. Wasafiri wengi wanahitaji huduma za chakula na vinywaji. Unapomzuia huyu kufanya biashara usiku maana yake unataka hao wasafiri, ama wasafiri mchana tu (jambo ambalo haliwezekani), au wawe wanakula Kenya kabla au baada ya kuingia na kutoka Tanzania.
Kwa dunia ya leo ya ushindani mkubwa wa maendeleo tunafanya makosa makubwa mno kulazimisha watu walale mapema usiku. Hatuwezi kuendelea kama nchi kwa kudhani nusu siku pekee inatosha kutuletea maendeleo.
Kuna watu wengine ambao kwao usiku ndiyo mchana, na wengine mchana ndiyo usiku. Tutaendelea kuwa wa ajabu kama Jeshi la Polisi matumizi yake yatakuwa ya kuhakikisha watu wanalazimishwa kulala badala ya kuwapa ulinzi hasa kama wanayoyafanya yana tija kwa jamii na kwa nchi.
Hatuwezi kupata maendeleo kama tunaamini mwisho wa mabasi kusafiri ni usiku saa 4 badala ya kusafiri kwa saa 24. Waliofika Kampala wanajua namna jiji hilo lilivyo ‘bize’. Maduka makubwa yako wazi usiku kucha. Hao ni Waganda ambao wanakabiliana na vitisho vingi vya waasi na wahalifu wengine. Sisi tunashindwa nini kuwa na taratibu kama hizo Kariakoo na kwingineko nchini? Kwanini tuzidiwe na mataifa ambayo amani yao ni haba?
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amekuwa mfano mzuri wa matumizi sahihi ya muda. Tangu akiwa Simiyu alitumia madaraka yake kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ‘kuvunja’ baadhi ya taratibu ambazo hazina tija kwa maendeleo ya jamii na taifa. Akajitahidi kuweka hadi taa za barabarani na mitaani ili wachuuzi na wafanyabiashara waendelee na shughuli zao. Hakutaka kiza kiwe kikwazo. Akaamuru baa zifunguliwe na zifanye kazi kwa misingi ya kistaarabu, kwa maana ya kutopiga muziki mkubwa maeneo ya wazi, pia kujiepusha na vitendo ambavyo ni vya uvunjifu wa amani.
Fikra za aina hii ndizo zinazotakiwa katika ulimwengu wa leo ambao kasi ya watu kujitafutia maendeleo ni kubwa mno, lakini sisi badala ya kwenda na hiyo kasi, tunatumia dola kulazimisha watu waende kulala.
Tunapaswa kuzitazama upya sheria, kanuni na taratibu zetu kwa lengo jema la kuondokana na zile tunazoona ni kikwazo au zinafifisha kasi yetu ya maendeleo.
Tuangalie kama bado ni sahihi kuondoa watu sehemu za starehe saa 5 au 6 usiku. Tuangalie kama ni uungwana kwa mabasi kusafiri mchana tu. Kama ni suala la ajali, dawa si kuyazuia mabasi kusafiri usiku, bali kuangalia namna ya kuwa na barabara zisizoruhusu kupishana ana kwa ana. Sheria ziwabane madereva na watumia barabara wengine wazembe.
Twende tuifanye Kariakoo iwe soko lenye kufanya kazi kwa saa 24. Kuwekwe miundombinu ya kuimarisha ulinzi na usalama. Tuwe na maduka makubwa kama Mlimani City ambako mtu anaweza kuamka saa 8 au saa 10 alfajiri na kwenda kupata huduma anazohitaji.
Leo kwenye viwanja vyetu vya ndege ni aibu. Kuna huduma huwezi kuzipata usiku kwa sababu wahusika wamelala. Huu utamaduni ni mbaya na kwa kweli unaturudisha nyuma kimaendeleo.
Twende mbali zaidi tuhakikishe zahanati, vituo vya afya na hospitali zinafanya kazi usiku kucha. Juzi tu usiku saa 4 tumekwenda Kituo cha Afya Kwembe tukakutana na kufuri kubwa langoni. Tunaonekana wa ajabu kwa kuamini kuwa ugonjwa ni mchana na wagonjwa wanatibiwa mchana tu!
Twende mbele zaidi tuhakikishe vituo vya polisi vinabaki wazi saa 24 badala ya utaratibu wa sasa wa milango ya vituo kufungwa giza likishaingia. Tuna mengi ya kuachana nayo na kukumbatia yanayoweza kutusaidia kuendelea.
Tuache kutenda mambo kwa mazoea ilhali tukijua hayo mazoea hayana tena faida. Siri kubwa ya maendeleo inaanzia kwenye matumizi sahihi ya muda. Hutuwezi kupata maendeleo katika jamii ambayo muuza uji analazimishwa alale saa 5 usiku bila kujali wapo wanaohitaji huduma yake.
Tusiupalilie na kuutibia mbolea umaskini wetu kwa kupunguza muda wa kujitafutia maendeleo. Leo tunaona mechi zikichezwa usiku katika viwanja vyetu nchini. Huu ni mwanzo mzuri wa kuleta mabadiliko kwa kuachana na mazoea. Tukiamua kubadilika tunaweza. Tuanze sasa.