Morogoro
Na Everest Mnyele
Katiba tuliyonayo sasa pamoja na marekebisho yake, ni ya mwaka 1977. Katiba hii ni matokeo ya kuundwa kwa chama kimoja cha siasa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) Februari 5, 1977.
Katika hali ya kawaida, Katiba iliyopo pamoja na marekebisho yake, ni ya CCM. Inawezekana watu wakapinga, lakini walio wengi wanalitambua hilo.
Kabla sijaeleza kwa nini Katiba mpya, naomba tukubaliane kwamba kuna tofauti kubwa ya maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kifikra, kiteknolojia, ufahamu na uelewa wa watu kati ya mwaka 1977 na 2022.
Idadi ya watu imeongezeka, watu wamesoma, wametembea na wamefanikiwa kuwa sehemu ya
‘dunia kama kijiji’.
Watu hawa wanasoma na kuchambua na kujiuliza; je, Katiba iliyopo ni ya wananchi? Baada ya hapo wanajiuliza, je, Katiba ya wananchi inapatikana kwa utaratibu upi?
Baada ya kujiuliza maswali haya wanaona kabisa Katiba iliyopo haikidhi matakwa ya ‘katiba ya wananchi/umma’.
Hivyo kwa kuangalia hilo, viongozi wetu wanauona umuhimu wa kuwa na Katiba mpya itakayokidhi matakwa ya wananchi, jinsi watakavyopenda kuendesha mambo yao kwa uhuru, amani, haki na ustawi.
Sijui tunakwama wapi kwani Serikali ya Awamu ya Nne ilianza mchakato wa kupata Katiba mpya.
Tusidanganyane, kwa tulipofikia tunahitaji katiba ya wananchi au katiba ya umma. Nani wa kulifanya hili?
Kwanza ni viongozi na wasomi wote wa nchi hii. Hawa ndio wanapaswa kuanzisha mjadala na kuwashawishi wananchi wa kawaida, na ndiyo maana hatua ya mwisho ya kupatikana Katiba mpya ni kupigiwa kura na wananchi wote ili kuhalalisha kuwa katiba ni ya umma.
Hivyo wanaopaswa kuanzisha mjadala ni viongozi wa serikali, vyama vya siasa, taasisi mbalimbali ambazo kwa ujumla wake zinaongozwa na wasomi na watu wenye ushawishi katika jamii.
Sasa tuelezane kwa nini Katiba mpya ni muhimu kwa nchi kama Tanzania.
Kwanza, ni ukweli kwamba katiba iliyopo haikutokana na wananchi, hivyo inakosa uhalali wa kuwa ‘katiba ya wananchi au umma’.
Pili, katiba ni sheria mama inayotoa uthibitisho na uhakikisho wa serikali inayoundwa kuwa inatokana na katiba iliyorithiwa na umma.
Tatu, katiba inatoa kiashirio kwa wananchi kuwa utawala wa sheria na heshima kwa binadamu na misingi yote ya haki italindwa na kuhifadhiwa kwa mujibu wa katiba.
Nne, katiba inatoa hakikisho kwa umma kwamba sheria zote, maelekezo yote yana nguvu ya kisheria na kiutawala, pia sera zote, kanuni zozote zile lazima zifungamane na kupata uhalali wake katika sheria na katiba iliyoridhiwa na wananchi.
Tano, katiba huwa ni msingi mkubwa wa utawala bora unaozingatia uwazi, uwajibikaji na utawala wa sheria, dhana ambayo kwa pamoja ni misingi mikubwa ya demokrasia na maendeleo ya nchi.
Hivyo basi, Katiba mpya ni muhimu ili kwenda na mahitaji ya sasa ya mfumo wa demokrasia ya vyama
vingi.
Katiba yetu ya sasa ina marekekebisho zaidi ya 14, lakini pamoja na marekebisho hayo, bado haikidhi mahitaji na maendeleo tuliyofikia.
Nchi yetu haihitaji vuguvugu (movements) kama za wenzetu ili kupata Katiba mpya. Tunaweza kupata Katiba mpya kwa njia nzuri kabisa, na uzuri safari hii ilishaanza na awamu ya nne na tunayo rasimu ya katiba! Tuangalie tulikwama wapi?
Kwa ufupi mimi binafsi naona mwanga wa kupatikana Katiba mpya japokuwa imewekwa kwenye mpango wa muda mrefu na Kamati ya Profesa Mukandala.
Maadamu Rais aliyopo ana nia na Tanzania ya miaka 100 ijayo na si mitano, basi Katiba mpya inayokidhi matarajio ya wananchi itapatikana kipindi chake kwani; nyota njema huonekana asubuhi.
Suala la mwisho kwa leo ni kukubaliana kuwa jambo lolote jema linaanza na viongozi, wasomi, wakereketwa, taasisi za dini na zisizo za dini na mwananchi wa kawaida ni wa kushawishiwa tu.
Kiukweli makundi niliyotaja mwanzo ndio ‘wengi’ (majority) na kundi la pili la wananchi ni ‘wachache’ (minority) kwa sababu hawa hushawishiwa tu. Inaweza ikawa ni vigumu kunielewa kwa sasa.
Mwisho, viongozi tuliopo madarakani tumsaidie Kiongozi Mkuu wa nchi kuijenga Tanzania kwa ajili ya vizazi vijavyo, tutumie elimu zetu, uzoefu wetu na utandawazi (exposure) kuisaidia Tanzania kuwa nchi
bora ya kuishi.
Tujiepushe na kuangalia masilahi ya kesho au kesho kutwa.
Ukweli tunahitaji Tanzania mpya. Tunaanzia wapi? Rais ameshaanzisha safari ya maridhiano. Tunaanza na mikutano ya kisiasa, tutaendelea kwenye Tume ya Uchaguzi labda na baadaye Katiba mpya.
Tusindanganyane, tunaweza kufanya haya kwa amani kabisa. Tuache woga, unafiki na mambo mengine kama hayo. Viongozi wa serikali na vyama vya siasa kazi kwenu mpira upo miguuni mwenu.