*Wakiri hali ikiachwa hifadhi inakufa
*Waunga mkono uhamishaji wafugaji
*Ujangili, ulaji wanyamapori vyashamiri
*Angalizo shughuli za kibinadamu latolewa
NA MWANDISHI WETU
ARUSHA
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limeunga mkono uamuzi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuhamisha wafugaji wanaoishi ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCA).
Msimamo wa UNESCO umebainishwa kwenye ripoti zake tano kuanzia mwaka 2007 na ya karibuni kabisa ikiwa ni ya mwaka jana. JAMHURI lina ripoti zote.
Shirika hilo baada ya kuona hali mbaya ya Ngorongoro, limesema: “UNESCO kwa ujumla wake imeshauri yafanyike mapitio ya mfumo wa matumizi mseto ya ardhi ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ambao kwa sasa umebainika kushindwa kufanya kazi ipasavyo; na kuhamasisha uhamaji wa wenyeji kutoka eneo la hifadhi kwa kutoa motisha kwa wenyeji ili waweze kuhama. Aidha, inashauri kuhamisha wafanyakazi wa taasisi ya NCAA na wafanyakazi wa mahoteli ili waishi nje ya eneo la hifadhi.”
Mwaka 1979 Ngorongoro ilitangazwa kuwa Eneo la Urithi wa Dunia. Eneo la Urithi wa Dunia ni eneo lenye ulinzi wa kisheria na mkataba wa kimataifa unaosimamiwa na UNESCO. Maeneo ya Urithi wa Dunia yameteuliwa na UNESCO kwa kuwa na umuhimu wa kitamaduni, kihistoria au kisayansi.
Maeneo hayo yamethibitika kuwa na umuhimu mahususi kitamaduni au kiasili duniani kote na yanazo sifa za kipekee na thamani kubwa kwa binadamu.
Maeneo ya Urithi wa Dunia yanaweza kuwa magofu ya kale au miundombinu ya kihistoria, majengo, miji, jangwa, misitu, visiwa, maziwa, makaburi, milima au maeneo ya nyika; yenye sifa za kipekee na thamani kubwa kwa binadamu.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lilianzishwa mwaka 1959 kama eneo la majaribio ya matumizi mchanganyiko ya ardhi, huku wanyamapori wakiishi pamoja na wafugaji (Wahadzabe, Wadatoga na Waamasai).
Sehemu kubwa ya Waamasai ambao walihamishwa kutoka Serengeti wanachunga mifugo yao katika eneo la hifadhi. Mwaka 2010 UNESCO iliiorodhesha NCA kama eneo mseto kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia.
Ngorongoro kupoteza sifa
Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Profesa Hamisi Malebo, anasema Mkataba wa Urithi wa Dunia ni wa kulinda na kuhifadhi urithi wa dunia, unazuia mabadiliko kutokana na shughuli za binadamu.
Anasema Urithi Mchanganyiko wa Ngorongoro tayari umekiuka mkataba.
“Sheria ya NCA inatambua uwepo wa wafugaji na mifugo ndani ya hifadhi, inatambua uwepo wa makazi na mifugo na ulishaji mifugo katika eneo la hifadhi. Wananchi walioko katika eneo la hifadhi wanaathiriwa na wanyama: kuwinda wanyama, kuliwa na wanyama, kuumizwa na wanyama na magonjwa ya wanyama kuathiri binadamu na mifugo,” anasema Profesa Malebo.
Ukaguzi wa UNESCO
Profesa Malebo anasema Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO katika nyakati tofauti ilituma taasisi za ushauri za Kamati ya Urithi wa Dunia ambazo ni The International Council on Monuments and Sites – ICOMOS na The International Union for Conservation of Nature – IUCN zikiwa na wataalamu kutoka Ofisi ya Uratibu wa Mkataba huu kutoka Paris, Ufaransa.
“Pamoja na majukumu mengine, kamati ilipitia hali ya maisha ya wenyeji, uhifadhi na utalii ambapo ilibaini ugumu wa kupata uwiano kati ya maendelelo ya jamii, uhifadhi na utalii ndani ya eneo la hifadhi.
“Kamati hiyo ilibaini kuwa maisha ya wenyeji waishio ndani ya eneo la hifadhi yamezidi kudorora kutokana na ukosefu wa fursa za maisha mbadala (community alternative livelihoods) zaidi ya ufugaji,” amesema.
UNESCO imesema kwenye ripoti zake kuwa kuna mambo yaliyokiukwa na changamoto zinazoikabili NCA kwa sasa. Mambo hayo ni kuwapo kwa shughuli za kilimo na uzalishaji wa mazao; ugumu wa kiutawala wa kusimamia ongezeko la watu, mifugo na udhibiti wa maingiliano hasi kati ya binadamu na wanyamapori; kuongezeka kwa miundombinu ya usafiri wa ardhini katika eneo la hifadhi; shughuli zisizo halali kama bodaboda, daladala, maduka, mighahawa, ujenzi ya majengo ya kudumu na ya kisasa; athari za utalii/mgeni/burudani na wenyeji wanaachwa nyuma katika Malengo ya Maendeleo Endelevu katika afya, elimu, kiuchumi na kijamii.
Matatizo mengine ni kuwapo kwa mimea vamizi, kuongezeka kwa kasi ufugaji na kupanua eneo la malisho ya mifugo, malazi makubwa ya wageni na miundombinu inayohusiana, matukio ya wananchi kuuawa na wanyamapori, na kuibuka kwa wimbi la uwindaji na ulaji wa wanyamapori.
Nini kifanyike? UNESCO inajibu swali hilo kwa kushauri hivi Serikali ya Tanzania: “Kubadili Sheria na kuweka utaratibu wa kisheria wa kuwahamisha wanadamu na mifugo katika eneo la hifadhi.”
Kwa nini Ngorongoro?
Ngorongoro inathaminiwa kitaifa na kimataifa hata kutangazwa kuwa Eneo la Urithi wa Dunia kwa sababu kadhaa muhimu.
Sababu hizo ni uwepo wa mlolongo mrefu wa ushahidi muhimu unaohusiana na chimbuko na mabadiliko ya kibinadamu na mienendo ya mazingira ya binadamu, kwa pamoja inayoanzia miaka milioni nne iliyopita hadi mwanzo wa enzi hii (makusanyo yaliyopatikana katika Bonde la Oldupai na eneo la nyayo za zamadamu la Laetoli).
Pili, Ngorongoro ina mazingira ya kupendeza ya Kreta ya Ngorongoro pamoja na mkusanyiko wake wa wanyamapori ambavyo ni moja ya maajabu makubwa ya asili ya sayari ya dunia.
Tatu, uwepo wa idadi kubwa ya nyumbu wahamao (zaidi ya milioni 1) ambao hupita kwenye hifadhi hii kama sehemu ya uhamaji wa nyumbu kila mwaka kwenye Mfumo Ikolojia wa Serengeti – Mara.
Nne, Kreta ya Ngorongoro ndiyo kubwa zaidi ulimwenguni ambayo haijagawanyika. Kreta hiyo, pamoja na kreta za Olmoti na Empakaai ni sehemu ya Bonde la Ufa la Mashariki ambalo volkano yake ilianza takriban miaka milioni 252 iliyopita.
Tano, uwepo wa mifumo mingi ya kiikolojia, mfano nyanda fupi za nyasi, misitu ya nyanda za juu, misitu ya savana, nyanda za milima mirefu vimeifanya Ngorongoro iwe ya kipekee.
Sita, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lina aina mbalimbali za wanyamapori walio hatarini kutoweka duniani kama vile faru mweusi, mbwa mwitu, simba na duma; pamoja na aina zaidi ya 500 za ndege.
Mkataba wa urithi wa dunia
Mkataba huu unahusu Ulinzi wa Urithi wa Kitamaduni na wa Asili wa Dunia. Ulianzishwa Novemba 16, 1972 jijini Paris, Ufaransa. Urithi wa Dunia ni maeneo ya kitamaduni, asili au mseto wa kitamaduni na asili ambayo yana sifa za kipekee na ya thamani kwa binadamu wote, na kwa hivyo, yameorodheshwa katika Orodha ya Urithi wa Dunia ili kulindwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo, navyo viyakute na kufahamu na kufurahia.
“UNESCO inahimiza utambuzi, ulinzi na uhifadhi wa urithi wa kitamaduni na asili duniani kote ambao una sifa za kipekee na thamani kuu kwa binadamu.
“Sifa za kipekee (Outstanding Universal Value – OUV): kulingana na UNESCO, ina maana ya kitamaduni na/au umuhimu wa asili ambao ni wa kipekee kiasi cha kuvuka mipaka ya kitaifa na kuwa na umuhimu wa kidunia kwa vizazi vya sasa na vijavyo vya binadamu wote,” amesema Profesa Malebo.
Pamoja na Ngorongoro, maeneo mengine nchini ambayo ni Urithi wa Dunia na miaka yalipotangazwa ikiwa kwenye mabano ni: Maeneo ya Utamaduni Kondoa (2006), Magofu ya Kilwa Kisiwani, Magofu ya Songo Mnara (1981) na Mji Mkongwe Zanzibar (2000).
Maneo ya mvuto wa asili ni Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (1987), Pori la Akiba la Selous (1982), na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (1981).
Mwishoni mwa wiki, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alizungumza na wazee wa jamii ya wafugaji jijini Arusha na kutangaza kuwa serikali imetenga eneo la ekari 400,000 lililoko katikati ya maeneo ya wilaya za Handeni, Kilindi, Kiteto na Simanjiro kwa ajili ya kuwahamishia wafugaji walio tayari kuhama kutoka Ngorongoro.
Amesema ekari 220,000 tayari zimepimwa viwanja 2,406 ambako kati ya hivyo, viwanja 2,070 ni vya makazi – kila kimoja kikiwa na ukubwa wa ekari tatu.
“Tumeanza na nyumba 101 zenye vyumba vitatu vya kulala kwa wale wanaotaka. Tuna viwanja 336 kwa ajili ya huduma kama shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya. Ujenzi wa mifumo ya maji kazi inaendelea,” amesema waziri mkuu.
Kwenye kikao hicho waziri mkuu alipokea majina ya awali ya kaya 86 zenye watu 453 ambao wamekubali kuondoka kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari huku wengine wakiendelea kujiandikisha.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mazungumzo ambayo waziri mkuu aliyafanya na wadau wa uhifadhi kwenye vikao vilivyofanyika Februari 14 na 17, mwaka huu kwenye tarafa za Loliondo na Ngorongoro wilayani Ngorongoro, Arusha.
Akikabidhi orodha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, amesema majina hayo ni ya awali na tayari yalikwisha kuhakikiwa mara baada ya wakazi hao kujiandikisha. “Tutawasimamia vizuri hadi waende kule wapate hati za mashamba, nyumba na maeneo ya kulisha mifugo yao.”
Waziri Mkuu amesema Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara mkoani Arusha aliliambia taifa iko hatari ya kutoweka kwa Hifadhi ya Ngorongoro ndani ya muda mfupi, na akatoa maagizo viongozi waende kuwasikiliza wananchi juu ya hatua za kuchukua ili tunu hiyo isipotee.
“Ile hatari aliyosema Mheshimiwa Rais ni ipi? Zamani watu waliishi na wanyama bila tatizo kwa sababu kulikuwa na wakazi 8,000 tu wenye ng’ombe 20 hadi 30. Leo hii kuna wakazi 110,000 na mifugo zaidi ya 813,000 wakiwamo ng’ombe, mbuzi na kondoo.
“Zamani maboma yalikuwa yamesambaa lakini leo hii nyumba zimejaa, tena za bati na tofali. Idadi ya watu imeongezeka, idadi ya mifugo imeongezeka na makazi yameongezeka. Hakuna huduma za afya au shule wakati ni hitaji muhimu kwa wananchi.”
Tayari Waziri Mkuu Majaliwa ameshafanya mikutano ya aina hiyo Ngorongoro na katika Pori Tengefu la Loliondo ambako kunatakiwa kutengwe eneo la kilometa za mraba 1,500 kwa ajili ya kulihifadhi.
Eneo hilo linatajwa kuwa muhimu kwa ikolojia ya Serengeti-Maasai Mara ikiwa na vyanzo sita vya maji, mapito na mazalia ya nyumbu na pundamilia.
Baadhi ya vyanzo vya maji vilivyopo katika eneo hilo ni kama ifuatavyo: Mto Pololeti – vijiji vya Oloipiri, Soitsambu, Maaloni, Arash na Ololosokwan. Mto Irmolelian – vijiji vya Piyaya, Arash, Malambo na Maaloni. Mto Orgumi – vijiji vya Losoito, Arash, Oloipiri, Magaiduru na Piyaya.
Vingine ni vyanzo vya maji vya Lima One – vijiji vya Soitsambu, Oloipiri, Oloirien na Ololosokwan. Chanzo cha maji Mlima Loilale – vijiji vya Ololosokwan, Kirtalo na Soitsambu. Chanzo cha maji Mlima Loili – vijiji vya Ololosokwan na Soitsambu.
Endapo mpango huu utafanikiwa kwa kuziokoa Ngorongoro na Loliondo, Serikali ya Awamu ya Sita itakuwa imeweka rekodi, kwani serikali zote zilizopita zilikosa msimamo wa kupata suluhu ya kudumu katika kuzilinda Ngorongoro na Loliondo.