Kitendo cha nchi za Afrika Mashariki na Kati kuandaa mafunzo ya kudhibiti ugaidi, kinaelezwa kuwatia hasira kundi la al-Shaabab hadi kuvamia na kuua watu zaidi ya 150 nchini Kenya.

  Jumla ya askari 300 kutoka nchi za Burundi, Rwanda, Tanzania, Uganda wamehudhuria mafunzo hayo yaliyoendeshwa na makomandoo kutoka nchi za Uholanzi na Marekani.

  Mafunzo hayo yalifanyika nchini Rwanda na yanadaiwa kuwatia hasira magaidi wanaounda kundi la al-Shaabab ambalo sasa limetangaza kuadhibu nchi za Afrika Mashariki. Tayari wamefanya unyama Kenya na Uganda wiki iliyopita.

  Askari hao — wanajeshi na polisi — walipatiwa mafunzo kwa muda wa wiki mbili nchini Rwanda. Mafunzo yalipewa jina la Command Post Exercise (CPX) au maarufu kwa jina la ‘Maliza Ugaidi 2015’.

  Yalifunguliwa na Mkuu wa Majeshi ya Uganda (UPDF), Jenerali Edward Katumba Wamala, yakilenga kuwaweka sawa askari walioshiriki juu ya namna ya kupambana na ugaidi.

  Mkuu wa mafunzo, Brigedia Mathew Gureme, aliwahakikishia askari kwamba baada ya kuhitimu watakuwa na utaalamu mzuri wa kukabiliana na ugaidi, lakini hawana budi kuwa makini.

  Brigedia Jenerali Kenneth H. Moore kutoka Marekani alitoa onyo kwa askari hao kushirikiana katika kujiamini na kuongeza kuwa, “Mafunzo haya ni kwa ajili ya wanajeshi wanaolinda mipaka.”

  Siku chache baada ya mafunzo hayo, magaidi wamenza kazi ya kuwamaliza watu wanaofuatilia nyendo zao katika maeneo ya Afrika Mashariki, ambako Alhamisi iliyopita walivamia na kuua zaidi ya watu 150 nchini Kenya, wengi wakiwa ni wanafunzi.

  Serikali ya Kenya imetangaza kuwashikilia watu watano kutokana na shambulizi lililoendeshwa na kundi la al- shabaab kwenye Chuo Kikuu cha Garissa.

  Waziri wa Usalama nchini Kenya amesema baadhi ya watuhumiwa walikamatwa wakijaribu kutorokea Somalia.

Mwanafunzi wa kike aliyenusurika shambulizi hilo aliyepatikana akiwa amejificha kabatini kwa zaidi ya saa 48 baada ya shambulizi, anasema kulikuwa na hali ya hatari katika maisha yake.

  Msichana huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 26, kwa sasa anahudumiwa na Shirika la Msalaba Mwekundu. Kundi la al-Shabaab hadi sasa limeapa kutekeleza mashambulizi mfululizo dhidi ya Kenya.

  Viongozi wa kundi hilo wametoa tamko wakisema wanafanya hivyo kulipiza kisasi vitendo vinavyofanywa na Jeshi la Kenya dhidi ya kundi la al-Shabaab nchini Somalia.

  Kundi hilo limejitangaza kwamba limehusika na mashambulizi ya Jengo la Biashara la West Gate mjini Nairobi nchini Kenya mwaka 2013 ambako watu 67 waliuawa.

   Tayari maofisa wa polisi katika taifa jirani la Uganda wanasema wamepokea habari zinazosema shambulizi kama hilo linapangwa nchini kwao.
  Wanafunzi walionusurika katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya wanatarajiwa kupelekwa chuoni chini ya ulinzi wa jeshi kundoa vitu vyao kabla ya kupelekwa nyumbani.

  Uchunguzi kuhusu tukio hilo unandelea na watu wawili zaidi wamekamatwa mwishoni mwa wiki na kufanya idadi ya watuhumiwa waliokamatwa kufikia watano. Kati ya waliokamatwa yumo Mtanzania, ambaye hajatajwa jina.

  Taarifa kutoka kwa walioshuhudia zinasema waliovamia chuo na kuua wanafunzi walikuwa wanazungumza lugha ya Kiswahili, lakini walionekana kupata maelekezo kwa njia ya simu za mkononi.

  Rais wa Marekani, Barack Obama, amekitaja kitendo hicho kuwa cha kinyama na kuahidi msaada wa hali na mali kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

  Kundi la magaidi liliingia chuoni majira ya saa 11 alfajiri ambako waliua walinzi wawili wa chuo katika lango kuu, kisha wakaingia moja kwa moja katika moja ya nyumba za ibada ambapo walikuta baadhi ya wanafunzi wakisali. Hawakufanya madhara msikitini.

  Baada ya kuingia chuoni humo walijigawa makundi, wengine wakijielekeza katika mabweni ya wanafunzi na kuanza kufyatua risasi hovyo wakiua wanafunzi. Baadhi ya wanafunzi waliuawa kwa kukatwa vichwa kwa visu kuvitenganisha na kiwiliwili.

  Kutokana na shambulio hilo, Serikali ya Kenya imeweka amri ya kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni mpaka saa 12 alfajiri  katika kaunti nne za mashariki mwa nchi ikiwa ni pamoja na Garissa, zikiwa ni juhudi za kukabiliana na vitisho vya kigaidi. Hii ina maana eneo hilo limewekwa chini ya hali ya hatari na yeyote atakayekaidi anaweza kupigwa risasi bila kuhoji.
 10628464_964012496950749_9148056650812356654_n

Rais Kenyatta pia amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi kutangaza nafasi 10,000 za kazi kwa nia ya kufundisha na kupata askari wa kutosha kulinda usalama ndani ya muda mfupi kama inavyowezekana.
  Hata hivyo,  viongozi katika kaunti hiyo ya Garissa wameitaka Serikali kuu na Umoja wa Mataifa (UN)  kuondoa kambi ya wakimbizi kutoka nchi jirani ya Somalia iliyopo Garissa na kuihamishia nchini Somalia ambako wataendelea kuhudumiwa na Umoja wa Mataifa wakiwa nchini mwao.
  Jeshi la Polisi katika nchi jirani ya Uganda linasema kuwa wamepata taarifa kuwa shambulizi la aina hiyo linapangwa kufanywa na kikundi hicho katika nchi hiyo, hivyo wameanza kuchukua tahadhari.


  Wakati hayo yakitokea katika nchi jirani za Afrika Mashariki, taarifa zinasema kwamba hali ya hatari inaweza kuikumba pia Tanzania katika mikoa mitatu ya Mwanza, Dar es Salaam na mji wa Bagamoyo mkoani Pwani.
  Taarifa zimethibitishwa na Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, aliyeiambia JAMHURI kwamba hali si nzuri kwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki, ikiwamo Tanzania.  
 Lema ambaye ni Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), amesema nchi inakabiliwa na viashiria vya matukio ya kigaidi katika kipindi hiki.

  Katika mahojiano yaliyofanyika mjini Dodoma hivi karibuni, Lema anasema vitendo vya askari wa jeshi la polisi nchini kunyang’anywa silaha na kuuawa wakiwa kazini vimekuwa vikifanywa na mtandao wa kikundi cha kigaidi, ambacho kinajipanga kufanya matukio ya kigaidi nchini.
  Anasema katika kipindi kifupi jeshi la polisi nchini limejikuta likipambana na mtandao wa kigaidi ambao haujaweza kugunduliwa na jeshi hilo, hivyo kuzidi kuhatarisha usalama wa raia na nchi kwa ujumla.

 “Askari wetu wanauliwa mfululizo, silaha zetu zinachukuliwa na wauaji hao ambao hawajulikani mpaka sasa, silaha zinazochukuliwa ni za kivita, tujiulize silaha hizi zinakwenda wapi?” Anahoji Lema na kuongeza:

“Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iko kimya, jeshi la polisi limekuwa kimya hawataki kusema ukweli kuhusu tishio hili la ugaidi na kuwanyang’anya silaha.”

  Lema anasema jeshi la polisi nchini limekuwa na tabia ya kufanya mzaha na maisha ya watu na usalama huku Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, akishindwa kutoa kauli bungeni kuhusiana na matukio hayo na kuishia kudanganya kuwa wamekamata silaha zilizoibwa, jambo ambalo si sahihi.

“Ni lazima Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na askari wakatambua kuwa usalama wa nchi haulindwi na Serikali  yenye uwezo wa kukamata wahalifu baada ya matukio ya uhalifu, isipokuwa Serikali yenye uwezo wa kuzuia uhalifu kabla ya tukio,” anasema.

  Akizungumzia kukamatwa kwa Watanzania wanaohusishwa na makundi ya kigaidi nje ya nchi, Lema anasema hana uhakika na suala hilo kutokana na Serikali kutotoa tamko lolote kuhusiana na kukamatwa kwao, lakini alishangaa Serikali kutokuwa na taarifa zozote kuhusiana na kukamatwa huko.

  Pia anasema kuna raia wa kigeni ambao wanamiliki hati za kusafiria za Tanzania kutokana na vitendo vya rushwa kushamiri katika Idara ya Uhamiaji na ofisi nyingi za Serikali, huku akieleza kuwapo kwa mtandao wa baadhi ya vikundi vya kihalifu kukutana na kufanya vikao nchini bila kufuatiliwa na vyombo vya dola.

  “Afrika Kusini, raia wa Nigeria wanamiliki hati za kusafiria za Tanzania. Wapo raia kutoka Congo nao wanamiliki hati za kusafiria [za Tanzania]. Kama twiga na tembo wanapita uwanja wa ndege, si ajabu wageni kumiliki pasipoti ya Tanzania. Huu ni udhaifu mkubwa wa Serikali,” anasema.
  Hata hivyo, Lema anaeleza kuwa pamoja na uadui mkubwa uliopo kwa askari na wananchi, ni vyema Watanzania wakawaombea askari waweze kupata mbinu za kujilinda.

  “Polisi anapofikia hatua ya kunyang’anywa silaha basi nchi ipo hatarini,” anasema Lema na kuongeza kuwa ifike hatua Jeshi la Polisi litambue kuwa dunia imeingia katika janga kubwa la ugaidi, hivyo wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi katika mapambano hayo si kuegemea kwa watawala wanaowatengenezea chuki kwa wananchi.

  Mbali ya Lema, Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, akizungumza na JAMHURI kuhusu mauaji ya askari wawili, amesema; “Hizi ni dalili ya ugaidi.”

  Baada ya mafunzo hayo, magaidi wamenza kazi ya kuwamaliza watu wanaofuatilia nyendo zao katika maeneo ya Afrika Mashariki. Walimvamia na kumshambulia Joan Kagezi, Jumatatu iliyopita.

 Kagezi aliyekuwa anaendesha mashtaka katika kesi dhidi ya watuhumiwa wa mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea mwaka 2010 nchini Uganda, aliuawa na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki.

  Watu 76 waliuawa kutokana na mashambulizi matatu ya mabomu yaliyotokea jijini Kampala, Uganda mwaka huo. Wahanga walikuwa wakiangalia fainali za Kombe la Dunia la soka katika migahawa miwili.
 

Kesi ya watuhumiwa 13 wa mashambulizi hayo ilifunguliwa Machi 17, 2015 na Jumatatu iliyopita Polisi Uganda wanasema Kagezi alikuwa akielekea nyumbani kwake saa moja usiku wakati pikipiki ya kukodiwa ilimposogelea karibu na gari lake na kuanza kumfyatulia risasi.

10404156_963930993625566_96457236336169867_n
  Kagezi alikuwa Mwendesha Mashtaka maarufu nchini Uganda na kwa sasa alikuwa akiongoza kitengo kinachokabiliana na ugaidi pamoja na uhalifu wa kivita kwenye ofisi ya mashtaka. Alikuwa mtu muhimu katika kesi ya watu 13 wanaotuhumiwa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea Kampala mwaka 2010.

Wakati hayo yakitokea Uganda, taarifa zinasema Rwanda nako hali si shwari hasa baada ya watu 16, akiwamo Joel Mutabazi, aliyekuwa mlinzi wa Rais Paul Kagame kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kupanga njama za ugaidi.

  Kutokana na hali hiyo, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamoud, mara moja amewaambia wakuu wa nchi za Afrika Mashariki kuwa inafaa sasa kuimarisha uhusiano wao dhidi ya ugaidi.

  Kauli ya Rais Mahamoud inakuja siku kadhaa baada ya wapiganaji wanaosadikika kuwa ni al-Shabaab kuvamia Chuo Kikuu cha Garrisa, Alhamisi iliyopita na kuua zaidi ya watu 150.

  “Huu ni unyama, Uislamu hauwezi kuwa hivi,” anasema Rais Mahamoud baada ya wanamgambo hao wa al- Shabaab kutumia kigezo cha dini kufanya ugaidi.

  Tukio hilo kumekuja siku chache baada ya vyombo vya usalama vya Kenya, kutangaza kuwashikilia wasichana watatu akiwamo Mtanzania, kwa kile kinachodaiwa kutaka kujiunga na kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Somalia.

  Kamishna wa Polisi Jimbo la Mombasa, Nelson Marwa, amesema Mtanzania aliyekamatwa, alijieleza kuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, nchini Sudan.

  Msichana huyo kwa jina la Ummul-Khayr Sadir Abdul (19), mwenyeji wa Zanzibar, anatajwa kuwa kiongozi wa kundi lililopanga kujiunga na al-Shabaab. Wengine ni Maryam Said Aboud na Khadija Abubakar Abdulkadir wote raia wa Kenya.

  “Hawa wasichana watatu, inaaminika kuwa walikuwa wanakwenda Somalia kupata mafunzo ya kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga,” anasema Kamishna Marwa.

  Kamishna Marwa amesema raia hao wawili wa Kenya, mmoja ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mount Kenya kilichopo Thika, na mwingine ni mwanafunzi wa Sekondari ya Burhania, iliyopo Malindi, Kilifi.

  Jijini Dar es Salaam, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Advera Senso, ametoa tahadhari kwa wananchi,  kuwa makini katika suala zima la ulinzi na usalama wa maisha na mali zao.

  “Uzoefu unaonesha kwamba, katika kipindi kama hiki cha sikukuu kuna baadhi ya watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vya uhalifu. Hata hivyo, Jeshi la Polisi katika mikoa yote limejipanga vizuri kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha kwamba hakuna vitendo vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza na pale vitakapoonyesha dalili ya kujitokeza viweze kudhibitiwa kwa haraka,” anasema Senso.

 Anasisitiza kwamba ulinzi umeimarishwa kwenye maeneo yote, yakiwamo maeneo ya kuabudia na fukwe za bahari baada ya taarifa kuzagaa kwamba kuna hatari ya miji mikubwa nchini kuvamiwa na magaidi.

  Kwa upande wake, Kamanda Kova anasema jeshi lake bado linawasaka watu wenye silaha waliovamia na kuua askari wawili na kujeruhi mmoja wakiwa kazini katika Kijiji cha Kipara, wilaya kipolisi ya Mbagala, Dar es Salaam.

  Aliwataja askari waliouawa kuwa ni D 2865 Sajenti Francis na E 177 Koplo Michael, na askari D 5573 Sajenti Ally alijeruhiwa kwa kupigwa risasi kwenye paja la mguu wa kushoto wakitumia bunduki aina ya SMG waliyopora kutoka kwa askari waliofariki.

  Kwa upande wake, Chikawe akizungumzia kukamatwa kwa Watanzania wanaohusishwa na matukio ya ugaidi nje ya nchi, anasema hana taarifa zozote za kiofisi na amesikia kupitia vyombo vya habari kama wengine walivyosikia.

  Chikawe anaeleza kuwa tayari ametoa maagizo Idara ya Uhamiaji nchini kufuatilia suala hilo kwa karibu na kumpatia taarifa za uhakika aangalie hatua stahiki za kuchukua.

  Aliwataka wazazi kuwa makini na watoto wao kutokana na kuwapo kwa taarifa za wanafunzi wengi kujiunga na vikundi vya ugaidi duniani wanapokwenda kwenye masomo nje ya nchi.

 “Nchi nyingi watoto wanaenda kujiunga na vikundi vya kigaidi, tunawaomba wazazi kuwa makini na watoto wao, Serikali inapambana na ugaidi usiku na mchana,” anasema Chikawe.

11108947_963860896965909_1596920409208835033_n
  Kuhusu kuuawa kwa askari polisi na kuporwa silaha anasema analaani mauaji hayo, lakini  ni jambo la kuangaliwa zaidi maana kutokana na hali ilivyo sasa kabla askari polisi hawajaanza kuwalinda raia wanalazimika kujilinda wao wenyewe.

  “Hali si nzuri kwa sasa, wizara inachukulia suala hili serious (kwa uzito), ila ninajua kuwa mwisho wa siku tutawakamata wote hata kama itatuchukua muda mrefu,” anasema Chikawe.

  Amesema kuwa silaha zote zilizoporwa  tayari zimekamatwa na kurejeshwa mikononi mwa polisi isipokuwa zilizoibwa Mkuranga na Kibiti ambazo zilichukuliwa katika matukio ya hivi karibuni.

  Kuhusu raia wa kigeni kumiliki hati za kusafiria za Tanzania, amesema wapo Watanzania ambao wamekuwa wakiuza hati hizo kwa raia wa kigeni huku nyingine zikiibwa kwa Watanzania na kuzirudufisha kisha kuzifanyia marekebisho mbalimbali na kuonekana kuwa zimetolewa Tanzania.

  “Pasipoti zetu ni nzuri zinaheshimika na zinapendwa duniani, zipo zinazoibwa na nyingine Watanzania wanaziuza wenyewe, ingawa inawezekana kupata pasipoti kutoka Idara ya Uhamiaji kwa kutumia njia za uongo, najua wapo vishoka wa kazi hii, lakini tunafanya kila linalowezekana kuhakikisha tunapambana nao,” anasema.

  Tukio la ugaidi la Kenya limewafanya Watanzania kukumbuka tukio la Agosti 7, 1998 ambapo Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulishambuliwa na kuua watu 11, huku nchini Kenya nako magaidi wakishambulia Ubalozi wa Marekani katika muda unaopishana dakika tano.

  Hii inadhihirisha kuwa Tanzania haipaswi kupuuza hata chembe hatari ya kushambuliwa na matukio ya uporaji silaha na kuua askari yanayoendelea nchini yanapaswa kuacha maswali mengi kuliko majibu.