Sasa nimeamini kuwa ‘la kuteleza haliwezi kutembea’ na ‘la kuvunda halina ubani’. Wiki mbili zilizopita niliandika makala yaliyokuwa na kichwa chahabari, ‘Je, machozi ya walimu yatamimina fedha mitaani?’

Kuna wasomaji wanadhani kuwa kwa waraka huu ninaishabikia CCM, sina uchungu na nchi yangu na nimetumwa na Serikali. Msikilize huyu, “….acha ushabiki kwa CCM wewe, kuwa na uchungu na nchi yako. Mshahara anaolipwa mfanyakazi wa Tanzania hasa mwalimu hauwezi kumsaidia kwa lolote kujikwamua kiuchumi…!”

 

Kwa haraka haraka nimeyakumbuka moja ya mafundisho ya mama yangu mzazi alivyokuwa akinifundisha jinsi ya kuishi na watu. Siku moja aliniambia hivi (kwa lugha ya Kikinga);  “Hapa duniani hakikisha unaambatana na watu wenye mtazamo kama wako ili utimize malengo yako. Ukiona mtu ana mtazamo tofauti na wewe, lakini yupo tayari kujifunza, tumia muda wako kumsaidia.

 

“Ukiona mtu ameshikilia anachoamini na hataki kujifunza, huyo ni kama maiti, mkwepe. Maiti atabaki kuwa maiti hata kama ukimpamba na kumweka kwenye maonyesho. Maiti hafikiri, hajifunzi jipya, haoni uhalisia; watu wanaofanana na maiti ni hatari kuliko moto wa milele.”

 

Ngoja nitekeleze usia wa mama, nakwepana na ‘maiti’. Lakini kuna kitu kidogo nikiseme. Watu wanaopingana na maarifa ya kujikwamua kiuchumi na ambao ‘wanashadadia’ wapinzani kuchukua nchi hii; nina uhakika watakuwa mzigo mkubwa sana katika serikali itakayoongozwa na chama chochote cha upinzani.

 

Hakuna chama wala serikali itakayoweza (sasa na hata milele) kuwapa wafanyakazi mshahara unaotosha. Kama kuna chama cha upinzani kinachopigania kuingia Ikulu kwa ‘sapoti’ ya ‘maiti’, hakika kitajuta kuongoza nchi hii.

 

Hakuna mzigo mkubwa unaozidi ule wa kuongoza wananchi wenye “fikra tegemezi”, “hulka za malalamiko”  “tabia ya kutazamia yasiyowezekana” na “mioyo isiyo na shukrani”. Nina hakika chama kitakachoibadili CCM kupitia watu wa hivyo kitachokwa mapema kungali asubuhi.

 

Ninapoendelea na makala haya sisiti kuwakumbusha nia ya ninachotaka mkipate. Kimsingi ninaendelea kushirikisha maarifa ya kiuchumi ili muone, mjifunze na mhamasike kutumia mishahara kidogo mnayoipata kuwekeza na kufanya biashara ili kuongeza kipato.

 

La pili juu ya hilo ni mbinu za kuendesha vitegauchumi na biashara bila kuathiri ufanisi unaotazamiwa katika ajira zenu. Naanzia pale ambako wafanyakazi wengi wanadhani ‘haiwezekani’. Sasa ngoja niwaeleze uzoefu wangu binafsi.

 

Mwaka 2007 wakati huo nilikuwa ndiyo kwanza nimehitimu kidato cha sita na nikiwa ndiyo kwanza nimetimiza umri wa miaka 19 nikianza wa 20; niliajiriwa Shule ya Sekondari Karatu kama mwalimu wa muda kufundisha masomo ya Baiolojia na Kemia.

 

Ulikuwa ni wakati ambao nchi ilikuwa inapita katika kipindi cha upungufu mkubwa sana wa walimu, hivyo niliombwa kufundisha masomo hayo kwa kidato cha tano na sita. Mshahara niliokuwa nalipwa ni Sh 150,000 kwa mwezi.

 

Nikiwa natoka kwenye familia duni, mimi nikiwa mtoto wa kwanza, nilikuwa na jukumu la kutunza familia nzima. Kwanza nilitakiwa kuendesha maisha yangu mwenyewe. Pili, nilikuwa na kibarua cha kusomesha wadogo zangu wanne achilia mbali matumizi mengine ya familia. Yote hayo yalitakiwa kutekelezwa kwa kutumia Sh 150,000 tu.

 

Wale waliobahatika kufika Karatu nadhani wanaelewa namna eneo hilo lilivyo na gharama kubwa za maisha. Kwa wakati huo Sh 150,000 ilikuwa haitoshi hata kunitimizia mahitaji yangu binafsi kwa mwezi mmoja. Ninaamini changamoto kama hii ndiyo inayowakuta wafanyakazi wengi.

 

Niliwaza na kuwazua ndipo nikaibuka na mikakati ya kuhakikisha napambana kuongeza kipato ili kukidhi mahitaji yanayonikabili. Kutokana na kuwekeza katika fikra nikaibuka na wazo la kufanya biashara ya vitunguu. Nilikuwa nikihudhuria kazini Jumatatu hadi Ijumaa mchana na baada ya hapo naanza uchakarikaji wa kuongeza kipato.

 

Mchana wa Ijumaa nilikuwa nikiondoka pale Karatu kuelekea eneo moja liitwalo Mang’ula (wanalima sana vitunguu); hapo nilikuwa nanunua vitunguu halafu Jumamosi asubuhi naondoka kwenda Arusha mjini kuviuza. Jumapili ilikuwa ndiyo siku niliyokuwa ninatoka Arusha mjini kurudi Karatu tayari kujiandaa kwa majukumu ya kufundisha siku ya Jumatatu.

 

Kwenye masuala ya biashara watu wengi husingizia ukosefu wa mitaji kama kizuizi cha kufanya mambo. Lakini katika sayansi ya mafanikio tunasema mtaji si tatizo kwa sababu yapo mambo  unayoweza kuyatumia kama dhamana na ukabadilishana na fedha na ndivyo nilivyofanya.

 

Kiukweli mtaji nilioanza nao ulikuwa wa Sh 70,000 salio la mshahara na niliweza kununua magunia mawili tu ya vitunguu. Kutokana na kuishi vizuri na watu na uaminifu, kuna wakati ambao wakulima wa kule Mang’ula walikuwa wakinikopesha na ninawalipa nikishauza. Niliendelea kwa mtindo huo na ilifika wakati ambao mtaji wangu ulifika Sh milioni sita ndani ya miezi 11.

 

Haikuwa kazi rahisi kwa ‘mwalimu’ kuonekana ninahangaika na magunia ya vitunguu sawa sawa na wachuuzi wa sokoni! Wengi walikuwa wakinishangaa, lakini nilijua nilichokuwa nakitafuta. Wengi walinicheka, lakini sikufadhaishwa na dharau za muda mfupi kwa faida ya muda mrefu. Niliutenga muda wangu kiumadhubuti ili shughuli zangu za kuongeza kipato zisiathiri utendaji wangu darasani.

 

Ukienda pale Sekondari ya Karatu hata leo omba upewe takwimu za matokeo ya kidato cha sita kwa kipindi nilichokuwapo; hakika utaambiwa kuwa matokeo ya shule yalikuwa bora sana kwa masomo niliyofundisha ikilinganishwa na miaka iliyotangulia.

 

Hili nawaeleza ili mtambue kuwa kumbe inawezekana kufanya majukumu ya ajira yako kwa ufanisi mkubwa na wakati huo huo ukaweza kupigana kuinua kipato chako. Wafanyakazi wanaweza kujitetea kuwa majukumu yanabana, au muda hakuna, lakini mimi nilikuwa ninaanza kufundisha mfululizo saa 12:30 alfajiri hadi saa 4 usiku.

 

Kati yangu na mfanyakazi anayeingia kazini saa 2 na kutoka saa 10 jioni nani ana muda zaidi?  Hakuna kinachoshindikana kama mfanyakazi ukiamua kufanya mabadiliko ya kiuchumi katika maisha yako. Kulilia nyongeza ya mishahara si jambo baya, lakini tatizo lililopo ni kuwa “duniani hakuna mshahara unaotosha”

 

Wakati nikipambana kufanya biashara ya vitunguu pamoja na kufundisha tuisheni, nilikuwa nikitembea na wazo kubwa zaidi lililokuwa ni kufungua chuo cha mafunzo ya biashara na kompyuta. Julai 2008 nilifanikisha lengo langu hilo kwa kufungua chuo hicho ‘ Stepwise Universal College ’ wilayani Mufindi, Iringa.

 

Nikiwa naendelea na ‘ualimu’ wangu Karatu nikawa na biashara inayoendelea Mufindi ikiwa na wafanyakazi watatu, walimu wawili na mhasibu mmoja. Nawaeleza hili ili kuwatoa hofu wafanyakazi ambao huwa wanaogopa kuanzisha biashara au vitegauchumi kwa kuogopeshwa na mawazo ama hofu mbalimbali.

 

“Sina muda wa kusimamia biashara”, “Nikianzisha biashara nitakaowaajiri wataniibia”; ni baadhi ya hofu na mawazo yanayowazinga wafanyakazi wengi. Kwa kadiri ninavyoendelea na makala hizi za biashara na uchumi, nitakueleza mfanyakazi namna ya kuanzisha vitegauchumi na biashara kwa kutumia mshahara huo kiduchu unaoupata.

 

Juu ya hayo na lililo na thamani zaidi ni namna ya kutengenezea mifumo rasmi ya kimenejimenti itakayokuwezesha kuzalisha fedha pasipo wewe kuwapo eneo husika. Ndiyo maana wakati wote huwa naamini wafanyakazi mna nafasi ya kuliokoa taifa hili dhidi ya uhaba mkubwa wa ajira unaoendelea sasa.

 

Jambo la kufahamu ni kuwa mshahara unaoupata ni sawa na mbegu. Unatakiwa upande kabla hujaila. Punje moja ya hindi hutoa mamia ya punje ukiipanda. Kwa dhana hii unaona kuwa kiwango cha mshahara unacholipwa hakiamui hali yako ya kiuchumi. Kinachoweza kuamua hali yako ya kiuchumi na kimaisha ni kile unachofanyia mshahara unaoupata.

 

Wengine wanapata mbegu na kuzila zote, wengine wanapopata mbegu wanakumbuka kupanda. Mwingine anapata mshahara ananunua masofa makubwa, mwingine anapata mshahara na ananunua kuku wa kufuga. Mwingine anapata mshahara na kulewa au kuhonga; mwingine anapata mshahara na kukumbuka kulima shamba.

 

Bahati nzuri ninauandika uchambuzi huu nikiwa na uzoefu wa kivitendo kwa mazingira ya Tanzania na ninawaeleza mambo niliyopitia na nimeyathibitisha. Lolote ambalo haliwezekani nitawaeleza, lakini sitasita kuwaeleza yote yanayowezekana hata kama yatakuwa hayaendani na imani zenu za kisiasa.

 

Endelea kukaa nami wiki ijayo

[email protected] 0719 127 901