*Wavutiwa na idadi kubwa ya wajane kando ya Hifadhi ya Serengeti 

*Wawatumia wajane hao, ‘nyumbantobhu’ kuhifadhi nyara, zana

*Mjane ahoji; ‘kiherehere cha nini ilhali bwana wangu haibi mali ya mtu ila nyara za Serikali?’

Mara

Na Antony Mayunga 

Wakati serikali ikipambana kuimarisha sekta ya maliasili na utalii inayochangia takriban asilimia 17 ya pato ghafi la taifa, majangili nao wamebuni mbinu mpya za kuzorotesha juhudi hizo.

Sekta hiyo iliyoathirika kwa kiwango kikubwa na janga la ugonjwa wa corona (Uviko-19), imepewa na serikali mabilioni ya fedha kuinusuru na mikakati chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea.

Hata hivyo, imebainika kuwapo kwa mbinu mpya zinazofanywa na Watanzania wachache wanaojihusisha na ujangili katika kutekeleza hujuma dhidi ya serikali.

Uchunguzi wa Gazeti la JAMHURI umebaini kuwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na mapori yanayoizunguka yamekuwa yakilengwa zaidi na majangili, hivyo kutishia sekta ya utalii wa picha na uwindaji.

Mmoja wa maofisa wastaafu wa serikali, Julius Nyigesa, amesema wajane wanaoishi pembezoni mwa maeneo yanayozunguka hifadhi wanatumika kufadhili mtandao wa ujangili.

“Ujangili ni mtandao unaowashirikisha watu wengi na wa aina tofauti; wakubwa na wadogo, vigogo na watu wa kawaida,” anasema Nyigesa. 

Anasema mtandao wa majangili huwatafutia wapenzi kwenye vijiji jirani na hifadhi wanunuzi wakubwa na wadogo wa nyamapori na nyara za serikali.

Wapenzi hao, wengi wao wakiwa ni wajane, huwapa hifadhi salama majangili na washirika wao. 

“Huwatumia (wajane/wapenzi wao) fedha za maandalizi ya mahitaji ya kambini na wao ndio huwaunganisha na majangili wenyeji. Wapenzi wao hao huwaandalia sehemu ya kutunza nyara na zana za ujangili wanapotoka kuwinda, kwa kuwa wanapolala sipo wanapotunzia nyara. Wakati wa msako unaweza ukamkamata jangili lakini usipate nyara au zana zake. Hiyo ni mbinu ya wanawake hao,” amesema Nyigesa.

Nyigesa mwenye umri wa miaka 70 ni askari mstaafu wa Idara ya Wanyamapori.

JAMHURI limeelezwa kuwa vijiji vya Bisarara, Nyamburi, Mbiriki na Bonchugu vilivyopo Kata ya Sedeko, Serengeti, vinaongoza kwa kuwa na wajane.

“Sababu kubwa ni kufungwa jela kwa vijana wengi au wale wanaokwenda kuwinda (kufanya ujangili) hawarudi tena. Pia kuna vijana wanaokimbia wake zao kutokana na ugumu wa maisha,” amesema.

Wanawake ambao waume zao walikuwa majangili na sasa wamefariki dunia au wapo jela, wana uzoefu wa mambo ya ujangili, wanajua masoko na wao wenyewe wanafahamika kwa wanunuzi kutoka sehemu mbalimbali.

Mzee Nyigesa aliyefanya kazi serikalini kwa zaidi ya miaka 40, amesema kwa kawaida mchana majangili hushinda ndani wakinywa pombe na kupanga mipango, kisha kwenda porini usiku wakiwa na chakula, silaha za jadi, nyaya na wakati mwingine majiko madogo ya gesi kwa ajili ya kupikia, kwa kuwa hayatoi moshi.

“Ujangili wa wanyama wadogo kwa ajili ya nyama ya kukausha ambayo husafirishwa hadi nchi jirani hushika kasi ‘msimu wa nyumbu’; kuanzia Juni mwishoni na kuendelea. Wakati huo huwa kunakuwa na ongezeko la wageni, miongoni mwao wakiwa ni majangili na wanunuzi,” amesema.

JAMHURI limeelezwa kuwa mbali na wajane, ‘nyumbantobu’ pia hutumiwa kama hifadhi salama za majangili.

‘Nyumbantobhu’ ni miongoni mwa mila potofu ambapo wanawake wasio na watoto ‘huoa’ mabinti na kuwatunza, kisha kuwatafutia wanaume ili wawazalie watoto.

Uchunguzi umebaini kuwa majangili huwatumia wajane na ‘nyumbantobhu’ pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mapori ya akiba ya Ikorongo, Grumeti na Ikona wilayani kama makazi ya kufikia kabla na baada ya kwenda kuwinda.

Majangili hutumia nyumba za wajane na walioolewa ndoa za ‘nyumbantobhu’ kupanga mikakati kwa kuhusisha wenyeji wa maeneo hayo.

Sasa mbinu hii imeshamiri kwani inawawezesha watuhumiwa wa ujangili kuhifadhi vifaa kama baiskeli, unga, sufuria na mboga ya ‘kuanzia kazi’ ndani ya hifadhi. Inadaiwa kuwa kuna nyakati hukaa hifadhini kwa zaidi ya mwezi mmoja wakiwinda na kukausha nyama.

Wajane pia wanadaiwa kuficha nyara kabla ya kuuzwa au kusafirishwa kwa baiskeli, punda na bodaboda kwenda nje ya Serengeti hasa katika vijiji vya Maburi, Kebanchabancha, Rung’abure, Tarime na Rorya; baadhi hupelekwa Kenya, Somalia na Sudan Kusini.

Kipindi hatari zaidi

Jangili ‘mstaafu’ na mkazi wa Kijiji cha Bisarara, Samwel Nchagwa, anakitaja kipindi hatari zaidi kwa ujangili kuwa ni kati ya Julai na Oktoba.

“Ujangili hushika kasi kipindi hicho na hata wanafunzi hushiriki kutafuta fedha za mahitaji. Uwezekano wa kupata wanyama ni mkubwa, na biashara nyingi vijijini hushamiri maana watu wanakuwa na fedha,” amesema.

Amesema msimu wa nyumbu na mvua nyingi, licha ya nyama kutokauka haraka, ni salama kwao kwa kuwa doria hupungua kutokana na mito kujaa maji.

Kuhusu ujangili wa tembo, Nchagwa anasema kuwa umepungua ingawa majangili hutumia udhaifu wa serikali kushindwa kuwafukuza kwa wakati tembo wanaokula mazao.

“Sasa hapo jangili akijitokeza, wananchi hutoa ushirikiano wa kuwaua ili kuokoa mazao yao,” amesema.

Hata hivyo, anakiri kuwa kupungua kwa ujangili dhidi ya tembo kumetokana na serikali kudhibiti silaha za kuua mnyama huyo mkubwa.

“Ujangili uliopo sasa ni wa nyama za biashara kwa kutumia waya ambazo ni silaha hatari hata kuliko bunduki,” amesema.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wajane kutoka Kijiji cha Mbirikiri (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama), amekiri kuwa na uhusiano na watu kadhaa wanaojihusisha na ujangili.

“Sawa, sisi tunawahifadhi. Lakini wanapokuja wanashirikiana na wakazi wa hapa kwenda kufanya ujangili. Wenzao wakirudi wanahudumia familia zao, sasa kwa nini sisi tusihudumiwe na wapenzi wetu?” amehoji.

Amesema mtandao huo hauishii kwao tu, bali ni mpana na uwepo wake unafahamika hadi kwa viongozi (wa serikali).

“Jamii inatambua kuwa mimi ni mjane, lakini kwenye shughuli za maendeleo ninapangwa sawa na walio na waume zao wanaowasaidia kutafuta. Mbona hao wanaume wanaokwenda na mabwana zetu porini hawasemwi ila  wanaonekana mashujaa? Inakuwaje sisi tuonekane wabaya wakati uhalifu ni uleule?” ameendelea kuhoji.

Mjane mwingine kutoka Kijiji cha Bisarara (jina linahifadhiwa) amesema biashara ya nyama za porini haichagui mjane au mwenye mume; wote huifanya kwa kuwa inalipa na wateja ni wengi.

“Sisi wajane hatuna mpenzi mmoja. Tunaangalia masilahi tuweze kuhudumia familia. Unaponiona hapa mimi ndiye baba na ndiye mama. Mila za huku mume hata hatoi huduma, lakini mpenzi jangili fedha yake ni kama wachimba dhababu!” amesema. 

Anakiri kuwapo kwa idadi kubwa ya wajane kutokana na wanaume kufia porini (kwenye ujangili) na kuwaachia watoto bila msaada.

“Sasa ukimpata ‘mtwari’ (mpenzi jangili) unaweza ukaolewa na kupata nafuu katika huduma mbalimbali,” amesema na kucheka.

Hofu kwa watendaji

Kumeibuka hofu kwa baadhi ya viongozi wa vijiji, wakisema wingi wa wajane unasababisha majangili wengi kuingia kwenye maeneo yao, wana nguvu na mtandao mkubwa.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, viongozi wa vijiji vya Mbirikiri, Bisarara na Bonchugu, wamekiri kuwa vijana wengi hupotelea porini wanakokwenda kuwinda, hivyo kuacha nyuma wanawake wajane, na kwamba watuhumiwa wa ujangili kutoka nje ya kata na tarafa wanaongezeka.

“Tukiwakamata na kuwapeleka polisi, wanawake wao wanawadhamini mara moja na wanarudi vijijini wakitutishia kutushughulikia iwapo tutaendelea kuwafuatilia,” amesema mmoja wa viongozi hao.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mbirikiri, William Mwita, amesema kundi hilo ni hatari kwa maisha ya viongozi kwa kuwa Agosti mwaka 2015 aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mwita Mirumbe, aliuawa kwa kupigwa mshale na jangili aliyekuwa anafanya fujo kwa mpenzi wake. 

“Ni kundi hatari, si kwa wanyama tu, hata kwa viongozi na lina mtandao mkubwa hadi kwa watendaji wa vyombo vya serikali. Ndiyo maana wanakuwa na kiburi, wengi wao wana tuhuma mbalimbali huko walikotoka, kwa hiyo huku wanakuja kujificha na kufanya uhalifu tu.

“Majangili wengi wana mawakala wa kununua nyara maeneo mbalimbali ya mkoa na wengine wanatumiwa na watu wa nje. Hawa ni tishio kubwa maana wengine wameanzisha hadi VICOBA! Ikitokea mmoja wao amepata tatizo, wanachangiana na kutoa fedha,” amesema.

Anakiri kuwa katika kijiji hicho kuna idadi kubwa ya wajane na kwamba Februari 6, mwaka huu, vijana wanne wa kijijini hapo waliokwenda kuwinda na wenzao wakiwa na punda sita wa kubeba mzigo hawakurudi na wameacha wajane saba, kwa kuwa mmoja ameacha wake watatu. 

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Bisarara, Thomas Marwa, amesema wanaojihusisha na ujangili huingia kijijini wakitoka vijiji vya Maburi, Nyamatoke na Mosongo katika tarafa za Ikorongo na Ngoreme, wenyeji wao ni wajane.

Amesema kupitia uwekaji wa anwani za makazi unaoendelea, imebainika kuwa kijiji kina kaya zaidi ya 1,000; za wajane zikiwa nyingi zaidi.

“Hawa wanawake wana siri kubwa, kukitokea tatizo ndipo mnapata taarifa, vinginevyo wanaojua ni wale wanaoshirikiana kwenye pombe na uwindaji, kwa kuwa wakifika hukaa ndani na mawasiliano na wenzao wenyeji huwa ya siri. 

“Kundi hilo lina nguvu kubwa ndani na nje ya vijiji, kwa kuwa wanapojaribu kuwadhibiti wanawake wanaungana kuwashambulia viongozi. Kuna siku katika mazingira ambayo hayakutarajiwa mwanamke mmoja alikuja hadi kwangu na kunishambulia kwa maneno makali akihoji kwa nini ninafukuza wapenzi wao, nani atawahudumia?” amesema.

Wajane hao huwashangaa viongozi wa vijiji wakiwauliza kwa nini kuwa na kiherehere ilhali mabwana zao hawaibi mali ya mwanakijiji yeyote ila wanaiba nyara na mali za serikali?

Marwa analilalamikia Jeshi la Polisi kwa kutowapa ushirikiano kwa madai kuwa Mtanzania ana haki ya kwenda kokote atakako kama havunji sheria.

“Lakini sisi tunaathirika kwa kuwa vijiji vyenye rekodi kubwa ya ujangili havipati miradi kutoka TANAPA,” amesema kiongozi huyo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Bonchugu, Makena Mhono, amesema tukio la Mwenyekiti wa Mbirikiri kuuawa na jangili limewajengea hofu viongozi.

“Hili ni kundi ambalo lina vurugu hasa wanapokuwa wameuza mzigo kwenye klabu za pombe za kienyeji. Hutamba sana. Tumesema hili lakini hatusikilizwi. Kwanza hawachangii maendeleo na vijiji vinakosa ufadhili wa miradi ya TANAPA kutokana na kuwa na sifa ya ujangili,” amesema.

Wanavyoendesha ujangili

Jangili mwingine mstaafu (jina linahifadhiwa) amesema nyaya hutumika kwa wanyama kama twiga na nyumbu wanapokuwa wengi; huku kwa nyati, pofu na pundamilia usiku huwamulika kwa tochi, kuwakata mapanga na kuwachoma mikuki.

“Waya zinaua wanyama wengi, hiyo ni silaha hatari ya kimyakimya tofauti na bunduki ambayo askari husikia mlipuko. Kwa muda mfupi unaweza kuua wanyama wengi ukachagua unaowataka na wengine ukawaacha,” amesema.

Soko la nyamapori

Kwa mujibu wa Nyigesa, nyama huuzwa Tarime, Rorya, Bunda, Musoma Vijijini na Butiama. Wanunuzi wa Tarime huzipeleka Kenya, Sudan na maeneo mengine.

Mmoja wa majangili jina limehifadhiwa amesema baadhi ya majangili sugu walikuwa wakiagiza silaha nchi jirani kwa kubadilishana na mzigo wa nyama kavu zinazotumika kwa uwindaji wa wanyama mbalimbali.

Usafirishaji

Mirumbe amesema wanunuzi wengi wanadai wakisafirisha mchana ni nafuu kuliko usiku na wanabeba kwa kutumia pikipiki na baiskeli na wenye mitandao mikubwa wanatumia magari na wanafanikiwa kupita katika Daraja la Mto Mara kwenye kizuizi cha polisi.

“Pale daraja la Mto Mara kulitakiwa kuwa na kikosi maalumu (task force) mambo mengi yangedhibitiwa maana inaonekana kuwa mizigo ya nyama inapitishwa kwa urahisi,” amesema.

TANAPA 

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Kanda ya Magharibi, Martin Loibooki, kwa nyakati tofauti amekiri kufahamu hayo yote.

“Zamani ilikuwa kidogo lakini kwa sasa inaongezeka. Tunatumia vyombo mbalimbali kubaini uharifu huo na wengi wanakamatwa na kufungwa. 

“Kupitia Jeshi Usu mambo mengi yamedhibitiwa tofauti na zamani. Tunawaomba viongozi wa vijiji wenye taarifa sahihi watujulishe kwa kuwa wana mawasiliano na wahifadhi, tuwakamate watuhumiwa.

“Kwa sasa tumeunganisha nguvu na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa suala la ulinzi wa maliasili za nchi ambavyo vinajitahidi kudhibiti mianya mingi ikiwamo maeneo ya vivuko kama Mto Mara.

“Tunaomba wananchi watoe ushirikiano kuhusu uhalifu huo ikizingatiwa kuwa faida za uhifadhi zinanufaisha nchi nzima,” amesema.

Kamanda wa Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Longinus Tibishubwamu, amesema hakuwa na taarifa ya mbinu mpya na kuahidi kuifanyia kazi.

“Wewe ndiye umenipa taarifa ngoja niifanyie kazi maana ‘information is power’,” amesema.

Pia amesema ushirikiano mkubwa wa taasisi za uhifadhi na vyombo vingine vya dola umesaidia kudhibiti kwa sehemu kubwa ujangili wa wanyamapori na kasi ya kuwakamata majangili ni kubwa.