Na Bashir Yakub
Kesi iliyo mahakamani dhidi ya Makonda si mashtaka ya jinai. Kilicho mahakamani mpaka sasa ni maombi tu ya Saed Ahmed Kubenea.
Wala Makonda hatafutwi kukamatwa na mahakama yoyote, wala taasisi nyingine ikiwamo Polisi.
Nimeona hadi magazeti yanayoheshimika yakisema Makonda ana jinai za kujibu mahakamani, mara anatafutwa kukamatwa, si kweli.
Ni hivi, Saed Ahmed Kubenea anaomba ridhaa ya kumshitaki Makonda. Kawaida ya sheria ni kuwa DPP (Mwendesha Mashtaka wa Serikali) ndiye mwenye mamlaka ya kushitaki na kuendesha kesi ya mtu yeyote aliyeonewa katika jinai zote. Anaendesha kesi za jinai kwa niaba ya raia au mtu aliyeonewa ama aliyekosewa (aliyeibiwa, aliyeumizwa, aliyebakwa nk).
Hata hivyo mtu binafsi anaweza pia kushitaki na kuendesha kesi yake ya jinai mwenyewe bila kupitia kwa DPP.
Lakini ikiwa mtu binafsi atataka kuendesha kesi yake mwenyewe bila kupitia kwa DPP, basi anatakiwa kuomba ridhaa ya Mahakama kwanza, kupitia maombi (application) maalumu, chini ya vifungu vya 99(1)(3), 128(2), na 392A(1)(2) vya Sheria ya Mwenendo wa Kesi za Jinai.
Haya maombi ya ridhaa ndiyo yaliyo mahakamani mpaka sasa na si jinai dhidi ya Makonda. Maana yake Kubenea anaomba ridhaa yeye kama yeye ili aweze kumshitaki Makonda. Hiki ndicho kilicho mahakamani.
Kwa hiyo Kubenea anaweza akakubaliwa kumshitaki Makonda yeye kama yeye bila DPP ama akakataliwa. Na hiyo ni mpaka hapo hiyo Mahakama ya Kinondoni yalipo hayo maombi itakapotoa uamuzi kuhusu hilo.
Katika maombi hayo utamualika DCI, utamualika DPP na utamualika yule unayetaka kumshitaki, ambao nao kila mmoja kwa nafasi yake anaweza kujibu maombi kwa kupinga ama kukubali.
Na kwa haya maombi ya Kubenea, DCI na DPP tayari wamejitokeza na kupinga asishitaki yeye kama yeye.
Makonda hajajitokeza kujibu lakini kwa kuwa haya ni maombi tu (application), basi halazimishwi. Wanaruhusiwa kuendelea tu bila yeye kujibu ama kuwapo (exparte).
Ikiwa Kubenea atakubaliwa kumshitaki Makonda yeye kama yeye bila kupitia kwa DPP, basi hapo ndipo kesi ya jinai dhidi ya Makonda itaanza, na hapo sasa ni lazima Makonda kufika mahakamani atake asitake, na akikosa anakamatwa.
Kwa hiyo tuelewane kuwa mpaka sasa Makonda hana kesi yoyote ya jinai katika mahakama yoyote, wala hatafutwi kukamatwa.