DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa 

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema hataki kusikia kuna uhaba wa damu salama na anataka kuona inapatikana muda wote.

Akizungumza Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Ummy, amesema damu salama haipatikani sehemu nyingine zaidi ya serikalini.

“Kwa hiyo nimeshamwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya kwamba kati ya mambo sitaki kusikia ni kuna upungufu au uhaba wa damu au chanjo za watoto, chanjo za watoto huwezi kuzipata popote, huwezi kwenda kwenye duka la dawa binafsi ukanunua chanjo. Kwa hiyo nimemtaka ahakikishe chanjo za watoto zinapatikana muda wote,” amesema na kuongeza:

“Kwa sababu mgonjwa hawezi kwenda dukani kununua damu salama. Benki ya damu iko moja, na iko serikalini, kwa hili tunataka kuhakikisha hakutatokea tena uhaba.

“Ndiyo maana nimeelekeza tena sitaki kusikia hakuna mifuko ya kukusanyia damu, mifuko iwepo lakini kusiwe na wakusanyaji damu au watu wa kutoa damu.”

Ummy amesema hapo ndipo watasema wizara haina, lakini watahakikisha vifaa vya kukusanyia damu na mifuko ipo, kisha watarudisha lawama kwa jamii kwamba hawachangii damu salama.

“Niwatake waganga wakuu wa mikoa kulisimamia kikamilifu, wajibu wa halmashauri sasa utakuwa ni kuhakikisha watu wanakwenda kuchangia damu.

“Niwaombe viongozi wa serikali ngazi zote – mikoa na wilaya kuweka ajenda hii kuhamasisha wananchi kuchangia damu, kuona kwamba ni ajenda muhimu na ya kudumu, kama nilivyosema damu haipatikani sehemu nyingine, inapatikana serikalini,” amesema.

Ummy amesema wataendelea kuhamasisha watu wachangie damu kwa hiari. Pia wataendelea na utaratibu wa kuwataka ndugu wa mgonjwa nao kuchangia kwa hiari.

“Tutawaomba tu ndugu, hawatauziwa, ila iwe ni sehemu ya wajibu wao wa kuokoa maisha ya ndugu yao na ninachojua Watanzania wanaona fahari kumchangia mgonjwa damu,” amesema. 

Vilevile amesema watakwenda kuhakikisha hawapati tena tatizo la vifaa vya ukusanyaji wa damu na kuanzia sasa ikiwamo mifuko itatolewa bure.

Amesema jukumu la halmashauri zote litakuwa ni kuhamasisha watu kuchangia damu na kuandaa matukio ya watu kuchangia damu, na sasa hivi mifuko yote itanunuliwa na serikali na kugawiwa katika halmashauri, waganga wakuu wa mikoa wahakikishe wanaipata.

MSD wasema hakuna uhaba wa mifuko ya damu

Wakati Ummy akitoa agizo hilo huku Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) Kanda ya Mashariki wakifurahia ongezeko la ukusanyaji damu, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nao wamezungumzia upatikanaji wa mifuko ya kuhifadhia damu.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa wiki kadhaa umegundua kuwapo kwa uhaba wa mifuko hiyo, kitendo kinachowapa shida maofisa wa timu za ukusanyaji damu za hospitali hiyo.

Akizungumzia suala hilo, Ofisa Habari wa MSD, Etty Kusiluka, amesema wiki iliyopita mifuko 8,000 ya kuhifadhia damu ilipelekwa NBTS.

“Kupungua na kuwapo kwa mifuko hii ni suala la kawaida, lakini kwa sasa hakuna shida hiyo kwa kuwa tumepeleka mifuko ya kutosha kwa wahusika.

“Ni kweli kwamba mifuko ya kuhifadhia damu huwa inakwisha kwa kuwa tunaiagiza kutoka nje ya nchi na hutumika sana. Sisi tunachokifanya ni kuhakikisha hakuna uhaba,” amesema Etty.

Akizungumzia upatikanaji wa damu salama Kanda ya Mashariki kwa sasa, Meneja wa NBTS Kanda ya Mashariki, Pendaeli Sifueli, amesema kumekuwapo ongezeko la wachangiaji wa damu kwa hiara tangu gazeti hili lilipochapisha taarifa ya uhaba wa damu Januari mwaka huu.

“Katika benki ya kanda ya damu salama kwa sasa tuna damu ya kutosha. Wadau wetu ambao ni wananchi wanajitokeza kwa kuchangia damu, hivyo kusaidia kuokoa wagonjwa,” amesema Sifueli.

NBTS Kanda ya Mashariki inaundwa na mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam. Sifueli amesema vyanzo vikuu vya ukusanyaji damu ni shule, vyuo, nyumba za ibada na masoko.

Ameitaka jamii kubadilika na kuanza kuchangia damu mara kwa mara hata wanapopeleka mahitaji kwa wagonjwa wao waliolazwa hospitalini.

“Watu wasiogope kujitolea damu. Wajitokeze kwenye kambi za kuchangia damu ambapo watapata fursa ya kupima bure afya yao na kujua magonjwa yanayowasumbua,” amesema.

Sifueli amesema miongoni mwa faida za kujitolea damu ni kupunguza madini ya chuma mwilini ambayo yakizidi husababisha magonjwa kama shinikizo la damu.

“Ikumbukwe kwamba hakuna kiwanda cha damu. Kwa hiyo damu lazima ichangiwe na watu na ndiyo maana tumeanza kufungua klabu za wachangia damu vyuoni ili kuweka msukumo zaidi kwa jamii,” amesema.

Miongoni mwa watu wenye mahitaji ya damu ni wagonjwa wa saratani, wajawazito na watoto wanaozaliwa na matatizo mbalimbali.

Takwimu zinaonyesha kuwa Mkoa wa Pwani unaongoza kwa kuwa na wachangiaji 8,550 sawa na asilimia 150 ukifuatiwa na Morogoro; 14, 924 sawa na asilimia 133 na Dar es Salaam wachangiaji 23,924 sawa na asilimia 92.

“Tunawashukuru wakuu wa mikoa hii kwani wametupa msaada wa kutosha kufanikisha shughuli yetu,” amesema.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa wachangiaji damu, Shukuru Fadhili, amesema amefikia uamuzi huo baada ya

kusoma taarifa ya upungufu wa damu salama katika Hospitali ya Muhimbili.

“Dini zinatutaka kutoa sadaka na moja ya sadaka ni kutoa msaada kwa binadamu mwenzio. Kusaidia wengine ni moja ya sadaka zinazompendeza zaidi Mwenyezi Mungu,” amesema Fadhili.

Ameshauri jamii irithishe utamaduni wa kuchangia damu kizazi hadi kizazi ili kuokoa maisha ya watu wenye mahitaji.

MWISHO

Mifumo ya kidijitali yaipaisha TRA

DAR ES SALAAM

Na Alex Kazenga

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inajivunia ongezeko la makusanyo ya kodi kutokana na matumizi ya mfumo wa Stempu za Kodi za Kielektroniki (ETS).

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa wiki iliyopita na Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata, wakati akieleza umuhimu wa ‘App’ ya hakiki stempu’ inayoshirikiana na mfumo huo kuwa inalenga kulinda afya za watumiaji bidhaa na kuwalinda wazalishaji.

“Napenda kuwahakikishia wananchi kuendelea kupakua App ya hakiki stempu ambayo ni maalumu katika kuhakiki bidhaa kabla ya kuzitumia ili kulinda afya zao,” amesema.

Mbali na kulinda afya za watumiaji wa bidhaa, amesema App hiyo inaisaidia serikali kupata kodi halali kutoka katika ushuru wa bidhaa husika.

Tangu ulipozinduliwa mfumo huo Januari 15, 2019, amesema katika bidhaa za mvinyo na pombe kali zinazozalishwa nchini mamlaka hiyo imepata ongezeko la asilimia 86.2 katika makusanyo ya kodi ya ushuru wa bidhaa na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Pia amesema hadi Novemba Mosi, mwaka juzi, mfumo huo umewezesha ongezeko la asilimia 93 la makusanyo ya kodi ya ushuru na VAT kwa bidhaa ya maji yanayofungashwa katika chupa.

Kwa upande wa vinywaji laini vinavyozalishwa nchini, amesema tangu Agosti Mosi, 2019 limekuwapo ongezeko la asilimia 30 la makusanyo ya kodi ya ushuru na VAT.

Amesema ongezeko hilo limeshuhudiwa pia katika bidhaa za sigara na bia zinazozalishwa nchini tangu Januari 15, 2019 na katika sigara ongezeko limefikia asilimia 6.2 huku bia ongezeko likifikia asilimia tatu ya makusanyo ya ushuru na VAT.

“Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa ETS, tumeongeza idadi ya wazalishaji wa ndani wa bidhaa za sigara, vinywaji baridi na pombe wanaolipa kodi moja kwa moja. Wameongezeka kutoka wazalishaji 57 kabla ya kuanza kutumika kwa mfumo hadi kufikia wazalishaji 307 wanaotumia mfumo huo,” amesema.

Kidata amesema kwa kutumia mfumo huo, TRA imeweza kupata ongezeko la waingizaji wa bidhaa kutoka nje hasa bidhaa za sigara na vinywaji ambapo kwa sasa idadi yao inafikia waingizaji 122.

Kutokana na mafanikio hayo, anawahimiza wananchi wote kuendelea kupakua App hiyo  kwa sababu itawawezesha kujua uhalali wa bidhaa kwa kupata taarifa wapi ilipozalishwa, mzalishaji ni nani na lini imezalishwa?

“App ya hakiki stempu inalenga kumlinda mzalishaji kwa kuzitambua bidhaa zisiingie sokoni kudhoofisha bidhaa bora zinazozalishwa na wazalishaji waaminifu.

“Pia inawalinda wafanyabiashara waadilifu wanaotimiza wajibu wao wa kuzalisha bidhaa bora kwa kufuata sheria na kulipa kodi stahiki,” amesema.