Wakati Jiji la Dar es Salaam lilipokumbwa na zahama ya ukosefu wa mafuta na vurugu kwenye vituo vya petroli na dizeli, sote tulibaki vinywa wazi.
Nilikuwa nimerudi Tanzania kwa ajili ya sherehe za ‘send off’ na harusi ya mdogo wangu wa kike hapo Nyanda za Juu Kusini. Amini usiamini nilikoma.
Hali ilikuwa mbaya, askari walikuwa wakiranda kujaribu kuzuia fujo zinazodhaniwa kuwa zingeweza kuleta madhara kama kuchoma vituo, na kwa wenye magari na madereva walipanga kupata mafuta.
Nilibahatika kupata mafuta kidogo kabla gari langu halijazimika. Lakini magari mengine mengi yalifia barabarani bila madereva au wamiliki kuyaburutia pembeni.
Wengine tuliishia kusema ni mambo ya nchi zilizoendelea. Lakini kilichotokea siku za karibuni nchini Uingereza kimeonyesha kwamba kweli dunia ni kijiji. Yale yale ya Tanzania yameingia kwa mkoloni wake wa zamani – Uingereza.
Vibopa kwa vidampa tulikuwa tukitimka kuhakikisha tunajaza magari pamoja na madumu mawili matatu ya petroli au dizeli, ili kuwa na uhakika wa usafiri binafsi tuliozoea, kama madereva wa malori makubwa ya mafuta (matenka) wangeligoma.
Vituo vingi vilivyofungamanishwa na maduka makubwa ya bidhaa (supermarkets) vilishabandika mabango yaonyeshayo kuwa hakuna mafuta tangu Jumatano wiki iliyopita, mengine yakiandika kwamba kuna vyakula tu, na mengine yakifunika kabisa pampu za mafuta.
Tofauti na nyumbani Tanzania uhaba wa mafuta unakosababishwa na kampuni za mafuta kugoma, kwa kiburi cha kutotaka kupunguza bei hata baada ya bei kushuka kwenye soko la dunia – hapa London na Uingereza kwa ujumla – kinachogomba ni madereva wa matenka kupitisha kura ya kugoma kufanya kazi ya kubeba mafuta.
Madereva hao wanaona kwamba hali zao za kazi ni duni sana, ratiba za kazi ni ngumu na mfumo wa pensheni yao ni mbovu, hivyo wakaamua kupeleka ujumbe kwa wakubwa.
Kwa kusema kila mmoja alitikisika kuanzia Waziri Mkuu David Cameron hadi kijakazi mnunuzi mafuta kwa walalahoi.
Kwa kutaka kuleta nafuu katika tatizo hilo, Serikali ikachukua uamuzi wa kuwapa mafunzo wanajeshi wa hapa kwa ajili ya kuweza ‘kukabarof’ na kuziba pengo kwa kuendesha matenka kupeleka mafuta kwenye vituo vya kuuzia.
Presha ilipanda na kushuka miongoni mwetu. Kwenye baadhi ya vituo ilibidi polisi waingilie kati na kufunga vituo, maana madereva na wenye magari walianza kupigana wenyewe kwa wenyewe.
Ilikuwa kimbembe. Kila mmoja akitaka kujaza mafuta kwa kiasi anachotaka kwenye madumu baada ya kujaza tangi la gari lake, ili kwenda kuyahifadhi majumbani.
Unajua tena hapa ni ‘self-service’, hakuna cha kusubiri muuzaji aje kukuuliza unataka dizeli au petrol kiasi gani. Unakwenda na gari lako au jerikeni lako, unachukua pampu unabonyeza tani yako kisha unakwenda kulipa. Ni kama vile unavyoingia supamaketi. Unachukua bidhaa tani yako kwenye kikapu na kisha unakwenda kulipa.
Mimi pia nilikuwa kwenye foleni nikaona ni sawa, kwa sababu viongozi wa kisiasa walisema hivyo.
Japokuwa msemaji wa makazi ya Waziri Mkuu (10 Downing Street) alionya watu kutochukua mafuta kwenye majerikeni Jumanne, lakini Jumatano Francis Maude ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, aliwaambia madereva wahifadhi mafuta kwenye madumu.
Wakati huo huo Alhamisi, Waziri wa Nishati Ed Evans akawataka madereva wahakikishe matangi ya mafuta ya magari yao yamejaa mafuta au kwa uchache yawe robotatu kuepuka, kuadhirika barabarani.
Pesa inavyotafutwa kwa shida, uhangaikaji hadi uliweke gari lako barabarani kwa ajili ya kukufikisha na kukurudisha kazini, halafu unapata mateso haya, kweli imekuwa nongwa!
Kiuchumi hapa kwa watu wanaounganisha kazi mbili au tatu, au wanaofanya kazi mbali, wanafaidika kwa kuendesha magari yao wenyewe badala ya kupanda treni au mabasi, angalau kwa umbali fulani.
Muda ni mali. Wazungu wenyewe walianza kusema, kwa hiyo hakuna mwajiri au wakala wa waajiri wanaoweza kuvumilia mtu kuchelewa na hivyo kumpotezea muda wake aghali.
Ndiyo maana watu hutumia magari yao kutoka nyumbani angalau hadi kituo fulani cha treni, wakapanda na hata kuunganisha basi kuendana na safari zao siku hiyo.
Wengine huchangishana watu wawili au watatu, kununua mafuta na kutumia gari moja kwa ajili ya kukwepa gharama kubwa ya treni na kukwepa ucheleweshaji ule wa mabasi.
Maana nauli ya mtu mmoja kwenye treni inaweza kutosha wote wanne kwenye gari binafsi kwenda na kurudi. Lakini kwenye basi ni nafuu ila tatizo ni kusimama vituo vingi, hivyo mwajiriwa anajikuta akichelewa kazini hata zaidi ya nusu saa au saa nzima, wakati malipo yake yanategemea amefanya kazi saa ngapi kwa siku, wiki hadi mwezi.
Hofu ya mgomo wa madereva wa matenka imepungua angalau kwa sasa, na wanasema watu wanaweza kula Pasaka bila shida, maana licha ya mawaziri kadhaa kuingilia kati, Cameron mwenyewe ameshalidaka hilo japokuwa shinikizo la kutaka baadhi wajiuzulu linarindima huku na kule.
Yetu macho bwana. Mafuta tunayo ya kutosha kwa sasa, lakini yatafika mahali yatakwisha.
La msingi ni kuomba mazungumzo ya madereva kupitia vyama vya wafanyakazi yafikie mwafaka endelevu, wakati nikiombea pia Mamlaka ya Maji na Nishati Bongo (EWURA) inapopandisha na kushusha bei ipokewe vyema na wanaouza mafuta bila kuathiri walaji.