DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Mchakato wa utekelezaji wa sera ya Tanzania ya viwanda unapaswa kuanzia shuleni na vyuoni kwa kuwaandaa wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu.

Ni lazima kutekeleza sera hiyo kwa vitendo baada ya  mafunzo na kuiva katika masomo ya Sayansi na Hisabati.

Mataifa yaliyoendelea katika sekta ya viwanda na mambo mengine yamewekeza nguvu kubwa katika sayansi na teknolojia, somo  la Hisabati likipewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika  mapinduzi ya viwanda.

Pamoja na viwanda kuhitaji malighafi, masoko na vitega uchumi, wataalamu waliobobea katika sekta hiyo ni muhimu sana katika maendeleo ya viwanda; mhimili mkuu wa uchumi na ustawi wa jamii.

Baada ya kupata uhuru mwaka 1961, Mwalimu Julius Nyerere alitilia mkazo mkubwa elimu na baadaye  kuweka msukumo katika sekta ya viwanda kuinua uchumi wa nchi na kuzalisha ajira.

Mwalimu Nyerere alifanikiwa kuanzisha viwanda vingi nchini ili kuinua uzalishaji na kutoa ajira kwa Watanzania.

Baadaye viwanda hivyo vikaanza kudorora kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo uhaba wa wataalamu wa ndani na baadhi ya watumishi kutokuwa waadilifu katika kutimiza majukumu yao.

Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli ilikuja na sera ya Tanzania ya Viwanda iliyolenga kuifikisha nchi katika uchumi wa kati.

Katika utekelezaji wa sera hiyo, serikali ilianza kwa kasi ujenzi wa viwanda na kufufua vilivyoacha uzalishaji kwa muda mrefu.

Sera ya viwanda inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inatukumbusha kujua umuhimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika kutekeleza azima hiyo.

Misingi imara ya sayansi na teknolojia huzalisha wataalamu wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa nchi, miundombinu na huduma za kijamii.

Somo la Hisabati ambalo ni mbegu muhimu katika fani ya Sayansi linapaswa kujengewa msingi imara kuanzia shule ya awali na msingi.

Pamoja na serikali na wadau wengine kuwekeza katika sekta ya elimu, bado wanafunzi wengi hawafanyi vizuri sana katika masomo ya Sayansi.

Hisabati inaonekana kuwa mwiba kwa wanafunzi wa ngazi mbalimbali za elimu nchini.

Upimaji elimu hufanyika kwa njia mbalimbali, lakini njia kuu ni mitihani ya kitaifa kwa wanaohitimu ngazi fulani ya elimu baada ya muda maalumu kwa kufuata na kuzingatia mtaala.

Hapa nchini wanafunzi huanza kufanya mitihani ya kitaifa wakiwa darasa la nne kisha la saba; kidato cha pili, cha nne na hatimaye kidato cha sita.

Matokeo ya mitihani huonyesha idadi ya watahiniwa, ufaulu wa ujumla wa kila somo, pia hutaja shule kumi bora na wanafunzi kumi bora.

Januari 15, mwaka huu, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dk. Charles Msonde, alitangaza matokeo ya mitihani iliyofanyika mwishoni mwa mwaka jana.

Kwa kidato cha nne watahiniwa 438,820 walifanya mitihani 422,388; sawa na asilimia 96.3 walifaulu, wasichana wakifanya vizuri zaidi.

Somo la Kiswahili lilipata ufaulu wa juu ikilinganishwa na masomo mengine huku Hisabati likishika nafasi ya mwisho katika ufaulu kati ya masomo 11 kwa mujibu wa NECTA.

Somo la Kiswahili liliongoza kwa ufaulu wa asilimia 95.58, Kemia (92.02), Uwekaji Hesabu (Book-keeping) kwa asilimia 71.30 na Uraia (70.46).

Masomo mengine ni Biashara (67.40), Biolojia (67.23), Kiingereza (66.84), Jiografia (60.55) na Historia asilimia 59.21

Nafasi ya pili kutoka mwisho katika ufaulu ni Fizikia (55.33) na somo la mwisho ni Hisabati asilimia 19.45.

Matokeo hayo na ya kidato cha pili (2021) yameonyesha udhaifu mkubwa kwa watahiniwa wengi katika somo la Hisabati, ufaulu ukiwa chini ya wastani.

Dk. Msonde anasema hata mwaka 2020 ufaulu wa Hisabati ulikuwa chini ya wastani ambapo watahiniwa walipata asilimia 20.12.

Kuhusu ufaulu wa kidato cha pili, anasema: “Wanafunzi hawakufanya vizuri katika masomo ya Historia, Fizikia, Hisabati, Kemia na Biashara ambapo ufaulu wake upo chini ya wastani kati ya asilimia 19.52 kwa Hisabati na 49.77.”

Kwa miaka mingi jamii imejenga dhana kwamba Hisabati ni somo gumu, dhana ambayo inarithiwa kizazi hadi kizazi shuleni.

Wanafunzi ni moja ya makundi ya jamii yanayoathirika na kasumba hii, wengi wakiangukia katika kundi linaloamini kuwa Hisabati ni somo gumu kujifunza tofauti na uhalisia wenyewe.

Baadhi ya wazazi, walezi na walimu wamekuwa chanzo cha wanafunzi kulikimbia somo la Hisabati, kwa kuwakatisha tamaa wakisisitiza kuwa ni somo gumu lisilo na msaada baadaye.

Pia baadhi ya walimu wa Hisabati ni wakali sana na mara  nyingine hutoa adhabu kali kwa wanafunzi wanaoshindwa kufanya vizuri, hali inayosababisha wengi kujenga hofu.

Mara nyingine walimu hufundisha na kuwasaidia zaidi wanafunzi wenye uwezo darasani na kuwaacha wenye uwezo mdogo wa kuelewa. 

Tabia hiyo huwagawa wanafunzi katika madaraja wakati wa kujifunza.

Uhaba wa walimu wa Hisabati katika baadhi ya shule inaelezwa kuwa ni sababu ya wanafunzi wengi kushindwa kufanya vizuri katika somo hilo muhimu kwa wahitimu na taifa kwa ujumla.

Zana za kufundishia na kujifunzia somo la Hisabati ni changamoto kubwa katika shule nyingi. Walimu hufundisha Hisabati kwa nadharia zaidi kuliko kuwashirikisha wanafunzi kwa kutumia zana.

Wanafunzi kutopewa motisha  wa kutosha katika kujifunza Hisabati kuanzia ngazi ya msingi, walimu wengi  kutoa adhabu kwa wanaoshindwa kufanya vizuri badala ya kuwapa motisha wanafunzi kupenda kujifunza somo hilo.

Badala ya kufundishwa tu Hisabati, wanafunzi pia wanapaswa kuelezwa na kuelewa umuhimu wa somo hili katika maisha ya kila siku na faida yake katika kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Mapema Februari mwaka huu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alisema serikali imeandaa mpango wa kufanya utafiti kwa kuwashirikisha wadau wa elimu juu ya matokeo mabaya ya Hisabati kwa shule za sekondari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (MAT), Dk. Said Sima wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema ni muhimu kuchukua hatua madhubuti kuwajengea walimu na wanafunzi uwezo wa kufundisha na kujifunza Hisabati kuanzia ngazi ya msingi.

“Hili limekuwa ni tatizo la muda mrefu, wanafunzi hawapaswi tu kufundishwa Sayansi na Hisabati darasani pekee ni lazima wajifunze kwa vitendo zaidi ili kuelewa masomo hayo,” anasema Dk. Sima.

Mwalimu Shaaban Ramadhan wa Manispaa ya Morogoro anasema Hisabati lazima ijengewe msingi imara kuanzia shule ya awali na kwamba kwa shule za msingi  na sekondari kuwepo midahalo ya kuelezea umuhimu wa somo hilo na kufuta dhana ya kusema Hisabati ni somo gumu.

“Serikali kupitia Wizara ya Elimu iweke utaratibu wa midahalo shuleni itakayotoa nafasi kwa walimu na wanafunzi kujua njia mbalimbali za kufundisha na kujifunza somo la Hisabati na kufuta dhana kuwa somo hilo ni gumu,” anasema Mwalimu Ramadhan.

Kutoka Kigoma Ujiji, Mwalimu Damian Dismas, anasema wazazi na walezi wanapaswa kushirikiana na walimu katika kujenga nidhamu na taaluma kwa wanafunzi badala ya jukumu hilo kuachwa kwa walimu peke yao.

0755-985966