NGORONGORO
NA MWANDISHI WETU
Kutokana na hali mbaya ilivyo katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Pori Tengefu la Loliondo (LGCA), serikali haina namna nyingine isipokuwa kuchukua uamuzi mgumu wa kuyanusuru maeneo hayo.
Ndani ya wiki moja, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amezuru maeneo hayo mara mbili katika juhudi za kuhakikisha uhifadhi unaendelea, pia kuona namna bora ya kukabiliana na ongezeko la watu, mifugo na shughuli za kibinadamu.
Hata hivyo, mpango huu wa serikali unapata ukinzani wa wazi na wa kificho kutoka kwa baadhi ya viongozi, wakiwamo wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mmoja wa wana CCM aliyewahi kuwa kiongozi mwandamizi mkoani Arusha, amekuwa sehemu ya wanaoipinga serikali akiwa anafanya vikao vya siri ndani na nje ya mkoa huo. Hivi karibuni alidiriki kuandaa ‘maandamano’ mjini Dodoma, lakini yakazimwa baada ya kuwapo taarifa za kiintelijensia.
Katika eneo la Loliondo, waziri mkuu amesema suala la ushoroba wa kilometa za mraba 1,500 lililopo katika Pori Tengefu la Loliondo ambalo kumekuwapo ubishi wa muda mrefu juu ya mipaka yake, ni vema mipaka hiyo sasa ikajulikana.
“Ubishiubishi wa eneo kwenye namba upo kati ya wenyeji na wahifadhi, lakini hakuna anayejua kiuhalisia eneo linaanzia wapi na linaishia wapi. Haya ni maamuzi ya mwaka 2018 yaliyofikiwa kwenye kikao cha Ololosokwan. Ni vema tukaweka alama za kudumu ili iwe rahisi kubaini eneo hilo; kilometa za mraba 1,500 zijulikane zina ukubwa gani na zinagusa eneo lipi,” amesema waziri mkuu.
Amewahakikishia wananchi wa Loliondo kwa kusema: “Hakuna jambo linataka kufanywa kwa ‘trick’ kwa kutaka kumuathiri Mtanzania, hakuna serikali ya namna hiyo. Kila jambo linalozungumzwa kwenu ni jema tu, linafanywa kwa nia njema.”
Kwenye kikao cha ndani alichokifanya katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro zilizopo Loliondo, waziri mkuu alisema serikali haikusudii kuwaumiza wananchi, bali inataka kuona uamuzi unaofikiwa unakuwa wenye masilahi mapana kwa umma wote wa Watanzania.
“Tuweke masilahi ya taifa mbele, nasikia kuna watu wanataka kutuchonganisha, wilaya hii ndiyo tajiri kwa NGOs (mashirika yasiyo ya kiserikali), ilikuwa na NGOs 35 na nyingine zilikuwa hazijasajiliwa, baada ya mchujo tukabaini NGOs 17 ndizo halali.
“Vikao tumefanya vingi, kuna maeneo sisi serikali hatukufanya vizuri… hatukufikia kiwango cha kutekeleza yaliyoazimiwa mwaka 2017 na mwaka 2018. Naomba tujadiliane hapa kwa kuzingatia masilahi mapana ya taifa, tuzungumzie wafugaji na si kabila,” amesema.
Waziri Mkuu amesema si vijiji vyote vya Loliondo vimesajiliwa na kutangazwa kwenye Tangazo la Serikali (GN).
“Kuna vijiji vina barua za usajili tu, ni barua tu. Ili kijiji kiwe kimesajiliwa sharti kuwe na GN. Sasa jiulize, kijiji chako kina GN? Hakuna – hakuna GN hakuna kijiji,” amesema.
Amesisitiza ulinzi wa ushoroba wa ikolojia ya Serengeti, akisema eneo hilo halina budi lilindwe ili wanyamapori waendelee kuwapo kwa manufaa mapana ya umma.
Waziri Mkuu amewakemea watu wanaoeneza propaganda za chuki, akiwamo raia mmoja wa kigeni ambaye amefukuzwa nchini kwa taratibu za uhamiaji. Japo hakumtaja kwa jina, mtu huyo aliyesemwa huenda ni raia wa Sweden, Susanna Nordlund, ambaye anatumia mitandao ya kijamii kuichafua Tanzania na wote wanaomkosoa.
Amekuwa kiungo imara cha utafutaji fedha kwa NGOs zinazojihusisha kwenye masuala ya Loliondo. Amekwisha kufukuzwa nchini mara mbili.
Wanaotaka kuhama Ngorongoro kwa hiari
Februari 17, mwaka huu Waziri Mkuu Majaliwa alitoa fursa kwa wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro wanaotaka kuhama kwa hiari yao wajitokeze na waseme wanataka kwenda wapi kuishi.
“Suala la idadi ya watu ni kubwa. Kumbe huko nyuma kulishakuwa na mapendekezo. Yeyote anayeona anaweza kuishi mahali pengine yuko huru kusema. Kama yuko mtu wa aina hiyo, awe huru kwenda kwa DC (Mkuu wa Wilaya) kajiandikishe na serikali itakuhudumia vizuri. Hayo ni maamuzi ya mtu binafsi, kusiwe na mtu wa kumshinikiza fulani asifanye maamuzi yake. Kama yuko aachwe afanye maamuzi yake, aseme anataka kwenda wapi na sisi tutamhudumia,” amesema.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo alipozungumza na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro ilimo NCAA. Hatua hiyo inalenga kupunguza idadi ya watu, mifugo na shughuli za kibinadamu katika eneo hilo baada ya kuonekana limelemewa.
Majaliwa alikuwa akizungumza na viongozi na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro kwenye kikao cha ndani kilichofanyika makao makuu ya zamani ya NCAA, wilayani Ngorongoro.
Mkutano huo pia ulihudhuriwa na mawaziri wa Maliasili na Utalii; Mifugo na Uvuvi; Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Makatibu Wakuu wa wizara za Maji na TAMISEMI na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wadau wengine walioshiriki mkutano huo ni Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Shangai, viongozi wa kimila (Malaigwanan), wenyeviti wa vijiji na vitongoji, Baraza la Wafugaji la Ngorongoro na viongozi wa dini.
Muda mfupi baada ya kauli ya waziri mkuu ya kuwataka wanaotaka kuhama kwa hiari wajiorodhehe, kumeripotiwa matukio ya wenye nia hiyo kutishwa.
“Wamekuwa wakitoa taarifa kuwatisha watu wanaotaka kujiorodhesha, wanawatisha wasiondoke. Nadhani kungekuwa na mfumo mzuri na siri kwa kujiandikisha watu wote wanaotaka kuhama kwa hiari. Lakini pia kwenda Loliondo kujiorodhesha kwa DC ni mbali sana. Tunapendekeza pale yalipokuwa makao makuu ya NCAA ndipo kiwe kituo kimojawapo cha watu kujiorodhesha,” amesema mmoja wa wafugaji.
Kifo cha Ngorongoro
Januari, mwaka jana NCAA ilifanya kikao na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini. Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dk. Freddy Manongi, alisema kama hali iliyopo sasa ikiachwa iendelee kwa miaka 10, Ngorongoro itakuwa katika hali mbaya zaidi na huenda ikawa imetoweka.
Serikali ilikuwa imeshaanza kuchukua hatua kadhaa, zikiwamo za kuundwa kwa timu mwaka 2020 kulikofanywa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo. Tume ilimaliza kazi Mei, 2020 na kuwasilisha ripoti kwa waziri.
“Kitu ambacho walishauri kikubwa (nitasema kimoja) walipendekeza kitu kinaitwa ‘zoning scheme’ – kwamba tujaribu kugawa eneo hili na maeneo yanayozunguka eneo hili. Tugawe katika kanda, na kila kanda itathmini shughuli zinazofanyika na idadi ya shughuli za uhifadhi ndani ya eneo hilo,” amesema.
Hata hivyo, wataalamu wa uhifadhi wanapinga hatua hiyo wakisema haiondoi tatizo, badala yake maeneo ya wananchi yakilemewa na watu na mifugo watavamia yaliyotengwa kwa uhifadhi.
Sheria iliyoanzisha Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro imekipa chombo hicho dhima kuu tatu: Mosi, kusimamia uhifadhi wa wanyamapori na malikale, kuendeleza wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi, na kuendeleza utalii.
Kwa mujibu wa sensa maalumu iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mwaka 2017 idadi ya watu ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro imeongezeka kutoka watu 8,000 mwaka 1959 hadi takriban watu 100,000 mwaka 2020.
Dk. Manongi, anazungumzia hali hiyo: “Hatujui baada ya miaka 10 hali itakuwaje. Binadamu wanaendelea kuongezeka kwa sababu mbalimbali. Lile lengo la uwiano kati ya uhifadhi na maendeleo tumeona limefikia hatua mbaya kiasi kwamba mpango wowote wa uhifadhi unaathiri wenyeji, na hicho si kitu kizuri; na mipango yoyote ya maendeleo ya binadamu inaathiri uhifadhi – na huo ndio uwiano tuliotakiwa kuwa nao kati ya maendeleo ya binadamu na uhifadhi.
“Tumeanza kuona kwa kweli hii ‘model’ inafikia mahali pagumu. Tunajiuliza sasa tufanyeje? Hatujapata uamuzi, lakini itabidi tuendelee kufikiria jinsi ya kuelezea masuala ya maendeleo, lakini pia masuala ya uhifadhi ili tuhakikishe kwamba huo uwiano unakuwapo, kwa sababu kwa kweli bila hivyo baada ya miaka 10 naamini model hii ya multiple use (matumizi mseto) itakuwa imefikia sehemu ngumu sana – kwa kweli kuna haja sasa tulipo kuanza kuiangalia upya ili tuweze kufanya uamuzi mpya.
“Suala ni je, tunaweza vipi kuweka uwiano wa maendeleo endelevu ya binadamu, lakini pia maendeleo endelevu ya uhifadhi? Je, tunaweza ku-balance vipi? Nadhani mwisho wa kikao (wahariri) mtatusaidia mawazo ili kwa pamoja tuweze kuendelea na juhudi za kuangalia upya hii ‘model’.
“Kila kinachofanywa kwa manufaa ya uhifadhi kinaathiri binadamu ndani ya hifadhi, na kila ruhusa unayotoa kwa wenyeji ina athari kwa uhifadhi. Tume imeliona kabisa hilo wazi. Na kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa wahifadhi kuhusu idadi ya watu na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu, na kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa jamii kuhusu shughuli za uhifadhi kwa maana zinawaumiza.
“Wiki iliyopita kuna diwani mmoja alinitumia picha ya fisi ameua kondoo 38, nadhani alikuwa na ugonjwa wa rabies (kichaa), kwa hiyo wakanipigia simu wakasema fanya mpango tuzuie mambo kama haya ambayo huwezi ukayazuia kitaalamu…ni ngumu kweli kweli. Lakini si hiyo tu, kwa kweli kuna athari nyingi sana za uhifadhi zinazotukabili,” amesema Dk. Manongi.
Athari nyingine ni kuwapo kwa magugu vamizi ndani na nje ya kreta yanayosaidika kuenezwa na binadamu na mifugo.
Wakati mamlaka za nchi zikijitahidi kuinusuru Ngorongoro, baadhi ya wananchi wanaofaidika na shughuli za ufugaji katika eneo hilo wanapinga kwa nguvu zote mipango ya, ama kuwapunguza, au kuwaondoa binadamu na mifugo hifadhini.
Mashirika yasiyo ya serikali na yale yanayodai kuwa ni ya utetezi wa haki za binadamu hushikamana kupinga mipango yoyote ya kupunguza watu na mifugo hifadhini.
Dk. Manongi amesema: “Hatima ya Ngorongoro tuna changamoto ambayo inabidi tuitatue…baada ya kufanya sensa tumeona idadi ya watu inaongezeka sana, na eneo la hifadhi limebaki pale pale [kwa ukubwa] takriban kilometa za mraba 8,300. Hili ni tishio – kama idadi ya watu inaongezeka, lakini eneo liko pale pale ni tishio kwa sababu mwingiliano kati ya maisha ya binadamu na wanyamapori utakuwa ‘very complicated’.
“Kama hatutaweza kupunguza kwa namna yoyote ile idadi ya watu ndani ya hifadhi hili eneo litafika wakati ambao litakuwa halina ustahimilivu. Halitakuwa endelevu. Hiyo ni changamoto kubwa sana. Inabidi tuone namna ya kuhakikisha eneo hili ni endelevu – maisha ya watu yanakuwa bora, lakini bado uhifadhi unaboreka zaidi kwa njia mbalimbali. Tumeanza kuangalia upya huu muundo wa matumizi ya mseto,” anasema.