Na Deodatus Balile, Zanzibar

Leo naandika makala hii nikiwa hapa eneo la Mlandege, Zanzibar. Nimemaliza mjadala wa kuelekea mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Mjadala huu ulihusu “Maendeleo katika Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.” Waendesha mjadala waliuliza, sisi wanatasnia ya habari tunauonaje mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia?

Sitanii, mjadala ulikuwa mzuri mno. Wachangiaji walieleza tulikotoka, tulipo na matumaini ya siku za usoni. Mkurugenzi wa Radio One/ITV, Joyce Mhaville, ameeleza sura halisi anayoiona kuwa chini ya Rais Samia kuna mwelekeo mzuri kwa vyombo vya habari katika eneo la uhuru na uchumi.

Wala alichosema Dada Joyce siyo siri. Tumeshuhudia Februari 10, 2022 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, amefungulia magazeti ya Mwanahalisi, Tanzania Daima, Mawio na Mseto. Ni bahati mbaya kutokana na sekta kupigika kiuchumi kwa muda mrefu, pamoja na kufunguliwa magazeti haya hayajaanza kuchapishwa kwa sababu za kiuchumi. 

Hiki nacho ni kitisho kingine cha uhuru wa habari. Magazeti yana leseni, hayazuiwi, ila yana ukata. Tuombe Mungu alichosema Dada Joyce kuwa uchumi umeanza kurudi kwenye vyombo vya habari kizae matunda haraka. Natamani kuona magazeti haya yakirejea sokoni, yakiwa na habari zilizosheheni ukweli kuwahudumia wananchi.

Nikiri katika mjadala nilioutaja hapo juu, Waziri Nape amenikosha. Kuna wachangiaji wawili walitaka magazeti na mitandao ya kijamii ifungiwe. Nilisema kwa uchungu kidogo. Niliwashangaa wachangiaji hawa, kwani huko katika ‘fungafunga’ ya vyombo vya habari ndiko tunakotoka, wao bado wana hamu ya kufungia. Niliomba mawazo yao yasubiri miaka 200 ijayo.

Sitanii, mimi nikimwangalia Rais Samia ana nia ya dhati ya kuunganisha Watanzania. Tulishuhudia mara tu baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, kupigwa risasi, alisafiri hadi Nairobi, Kenya kumjulia hali. Pamoja na hali ngumu ya uhuru wa kujieleza iliyokuwapo, alivaa ujasiri akamjulia hali.

Msomaji usidhani lilikuwa jambo rahisi. Balozi Joseph Sokoine aliyekwenda hospitalini Brussels, Ubelgiji kumwona Lissu, alitenguliwa ubalozi. 

Ni wazi kama Rais Samia wakati huo asingekuwa Makamu wa Rais na kwamba Katiba au hakuna sheria inayomruhusu Rais kutengua ushindi wa Mgombea Mwenza, basi naye sheria ingeruhusu, huenda angetenguliwa.

Nilisoma makala ya Mwandishi Mkongwe, Absalom Kibanda, aliyekuwa anaandika safu ya TUENNDAKO, ambayo nayo chini ya Awamu ya Tano safu hii ilikufa kifo cha asili, kwamba kabla ya kifo cha safu hii alisema: “Nchi imetoka katika nyakati za hatari, imeingia katika nyakati za giza.” Kilichotokea nyakati zilizopita ni cha kuandikia kitabu, na naomba Mungu anijalie nipate nguvu niandike kitabu hiki, pengine miaka 500 ijayo Watanzania wasirejee makosa yaliyofanywa na kizazi chetu katika uchaguzi wa mwaka 2015. Najua kuna baadhi ya wanufaika kwa kusema hivi mnafuka moshi kwa ndani.

Sitanii, nafahamu bado kuna masalia. Hata huko kwenye mitandao ya kijamii kwenye hiyo inayoitwa Club House, nako masalia hayakosekani. Nimesikiliza mjadala unaoendeshwa baadhi wakimmwagia matusi Rais Samia kwa kukutana na Lissu huko Ubelgiji. Wanamwita kila jina baya, ila unahitajika umakini kufahamu iwapo wanaorusha matusi si sehemu ya masalia.

Nafahamu hata baadhi ya watendaji kuna kambi. Kuna wale wenye mfumo dume, kuna wale waliokuwa wanufaika wa ukandamizaji wa Watanzania. Kwa sasa tumepumzika kusikia watu wakifikishwa Kisutu, maana ilifanywa mara nyingi, hadi watu wakaacha kuona anayefikishwa mahakamani ni mdhambi. 

Nimewahi kuliandika hili, Lissu amemwomba Rais Samia na mimi naomba kulirejea. Tanzania ni nchi ya amani. Tanzania udugu wetu ni zaidi ya majirani zetu wafanyavyo. Sisi si taifa la visasi.

Desemba 15, 2021 pale jijini Dodoma, Rais Samia ulitwambia enzi za kusema “amani inapatikana kwa ncha ya upanga zimepitwa na wakati”. Ulitusihi tuitafute amani ya Tanzania kwa “ncha ya ulimi”. Nafahamu Mahakama imetoa uamuzi wa awali kuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake wana kesi ya kujibu.

Sitanii, Mheshimiwa Rais Samia wewe ni jasiri. Hakuna lililokuwa jambo gumu kama ulipounda Kamati ya Wataalamu, wakakushauri ukabadili msimamo kuhusu ugonjwa wa Corona na kusema tuanze kuchukua tahadhari kama nchi. Hili lilikuwa gumu, kwani Watanzania walikwisha kuaminishwa kuwa Corona ni vita ya kiuchumi. Nilihoji hii vita inailenga Tanzania pekee? Sikujibiwa.

Nikahoji mbona Marekani, Uingereza, Brazil, Italia, Afrika Kusini na kwingine wanakufa kwa Corona? Mbona ilifika wakati vitanda vikajaa wagonjwa katika hospitali zetu hadi mtu akakosa nafasi ya kumlaza ndugu yake hospitalini? 

Achilia mbali kupewa matibabu. Mbona kipindi hicho nyumba za kuhifadhia maita (mortuary) zilijaa hata Wakristo wakalazimika kuzika siku hiyo hiyo kama Waislamu? Mambo ni mengi siwezi kuyataja yote. Kubwa, nafahamu umeunda Kikosi Kazi kupitia hali ya siasa nchini. Hapana shaka kitashauri. Niishie hapo kwa hili.

Narudia, uamuzi ulioufanya wakati wa Corona ulikuwa mkubwa na mzito kuliko hii kesi inayochafua taifa letu. Neno UGAIDI si la kutajataja katika nchi. Tukiwatangazia mataifa ya wenzetu kuwa hapa kwetu kuna magaidi, tujue tunafukuza watalii, wawekezaji na tunahatarisha usalama wa nchi yetu. Kumtangaza mtu kuwa ni gaidi kunapaswa kuwa mchakato mrefu na shirikishi, unaoihusisha Mahakama. Hili neno tukiendelea kulitumia tunaharibu wenyewe heshima ya nchi yetu. 

Sitanii, bila kupepesa macho, naomba kitumike Kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka, kinampa DPP madaraka ya kuondoa mahakamani shauri lolote ambalo halijatolewa hukumu. 

Nafahamu Mama umetenda mengi mazuri. Nakuomba kupitia kwa DPP ulimalize hili, nchi iondokane na joto lisilo la lazima.

Nafahamu kama nilivyosema hapo juu, bado tunayo masalia. Pia hata baadhi ya wasaidizi wako ni mateka wa mfumo dume. Wapo wanaosema: “Kama Rais angekuwa mwanamume Mbowe angetoa kauli kama hizi?” Haya wanayatumia kuhalalisha hulka zao za kutaka watu wateseke, nchi ichemke isiwe na amani. 

Jamii sasa inaacha kujadili madarasa 18,000 uliyojenga, vituo 420 vya Afya unavyojenga tena ukaweka madirisha ya aluminium, visima vya maji… inajadili mashahidi wanaougua kizimbani. Inajadili mashahidi wanaosema hawajui nini kilitokea. Wanajadili kesi ya ugaidi wa Sh 600,000. Mama nakuomba liponye taifa letu vidonda vya ukatili. Tulikotoka siko, umekwishasema tushikane mikono. Kama nilivyosema, iwapo ulilimaliza la Corona, hushindwi hili la Mbowe.

Kama ni adabu, ameishaishika. Ametimiza miaka 60 akiwa jela. Ni historia asiyoweza kuifuta. Jamii yetu naamini haijafikia mahala pa kuulizwa kati ya Yesu na Baraba aachiwe nani tukasema Barabaaaaaaa…. Mheshimiwa Rais mimi nakuamini, naamini mengi uliyoyafanya, wala usisikilize hizo kelele za mtandaoni, kuna waliopandikizwa wakutoe kwenye ajenda ya maendeleo, uanze kuhangaika na watu. Njia hiyo si salama sasa na baadaye huko tuendako. Mungu ibariki Tanzania.