Kwa miaka mingi sasa sekta ya utalii nchini imekuwa ikitoa mchango mkubwa katika kuingiza pato la taifa, ambapo kabla ya dunia kukumbwa na janga la corona ilikuwa ikichangia asilimia 17.2.
Mchango wa sekta ya utalii hauishii katika pato la taifa pekee, kwani pia inachangia asilimia 25 ya mauzo pamoja na asilimia 60 ya mapato yote yatokanayo na biashara za huduma nchini.
Katika taarifa aliyoitoa wiki iliyopita, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro, amesema maliasili na utalii vina mchango mkubwa katika akiba ya fedha za kigeni.
Fedha za kigeni ni muhimu kwa taifa, kwa kuwa ni kama ‘bima ya afya’ ya taifa; kwa hiyo kuwa na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kunalipa taifa kujiamini na dhamana.
Tanzania ni miongoni mwa nchi chache duniani zilizojaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii kama mbuga za wanyama, milima, mabonde, fukwe na tamaduni za kuvutia.
Mbali na hayo, sekta hii imekuwa ikiitangaza Tanzania ndani na nje ya Bara la Afrika na kulifanya taifa letu kufahamika huku wageni mbalimbali wakija kutazama vivutio hivyo.
Ndiyo maana wala si ajabu kwamba taasisi mbalimbali za kimataifa zimekuwa zikitoa tuzo na kutambua mchango wa Tanzania katika uhifadhi wa mazingira na vivutio vyake.
Kwa kutambua mchango wa sekta hii ambayo imepambana sana wakati wa janga la corona, serikali imeipatia mabilioni ya fedha iweze kujipanga upya na kuendelea kulijenga taifa.
Tunaamini kuwa fedha hizo ambazo ni kati ya Sh trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kuchechemua uchumi nchini, zitatumiwa kwa lengo lililopangwa na kuinua utalii.
Kwa upande mwingine, kila Mtanzania anapaswa kujitathmini na kuona ni mchango gani anaoutoa katika kukuza sekta ya utalii pale alipo, akithamini mchango wake.
Tunaamini kwamba iwapo tutaunganisha nguvu kama taifa na kuwa na lengo moja tu; kulinda, kuhifadhi na kutunza mazingira, tutawezesha utalii kutoa mchango mkubwa zaidi kwa taifa.
Kila Mtanzania anapaswa kuyasema mazuri yanayopatikana nchini kwa sauti kubwa, huku yale mabaya yakisemwa kwa tahadhari na kutafutiwa ufumbuzi.
Sote tujiwekee lengo moja kama taifa; kwamba ni lazima Tanzania iwe nambari moja katika utalii barani Afrika.