Dar es Salaam
Na Mwl. Paulo S. Mapunda
Wiki iliyopita tuliona namna ambavyo shetani alifanikiwa kumrubuni binadamu na kuharibu mtazamo (mindset) wake. Tuendelee…
Shetani akafanikiwa kumshawishi binadamu amuasi Mungu, alilitenda hilo kwa kuziharibu programu zote ambazo Mungu alizisuka na kuziweka ndani ya mtu.
Akapandikiza fikra hasi kuhusu Mungu na ufalme wake. Katika kuasisi ufalme wake ulio kinyume cha ule wa Mungu wa mbinguni, shetani alifanikiwa kuwarubuni theluthi moja ya malaika, nao wakaasi kama yeye.
Katikati ya kundi la malaika waasi, kulikuwa na malaika wawili walioungana na shetani ambao awali walikuwa na vyeo vya juu sana katika ‘serikali ya mbinguni’ wakiwakilisha upande wa jimbo la duniani.
Malaika hao ni Lewiathani au Leviathani, Isaya 27:1; Ayubu 41:1-ESV, na Behemoth ambaye anatajwa sana katika kitabu cha Ayubu, hususan kwenye Biblia za Kiingereza (Job 40:15-ESV).
Katika Ayubu 40:19 imeandikwa: “Yeye ni mkuu wa njia ya Mungu; Yeye aliyemfanya alimpa upanga wake.” ESV mstari tajwa unasomeka: “He is the first of the works of God; let him who made him bring near his sword.”
Malaika hao walikuwa watawala wenza wakimsaidia mtu kuitawala dunia, Behemoth alipewa kusimamia eneo lote la nchi kavu ilhali Lewiathani alikuwa akitawala eneo la maji kama muwakilishi wa mtu. Anajulikana kwa majina ya ‘malkia wa bahari’ kwa Kiingereza ‘queen of the sea’ au ‘sea monster’.
Lewiathani ndiye aliyeasisi roho ya kikahaba ya Jezebeli inayojihusisha na umalaya duniani kote, ndiye anayeshughulika na ndoa na kuzivunja, ufuska wa aina zote, ngono za vikundi na ngono za kimfumo, ushoga na usagaji, ulawiti na mapenzi ya kinyume cha maumbile, hilo ni moja ya jukumu lake.
Halikadhalika anahusika na mambo ya urembo, kuharibu kazi ya Mungu, kuvuruga wanaohusika na uamuzi na hatima ya taifa au taasisi, viongozi (marais, wafalme na washauri wao).
Ahabu, Samson, Daudi, Selemani ni baadhi ya waathirika wanaofahamika wa utendaji wa roho ya ukahaba ya Jezebel (Lewiathani).
Pweza ndiyo taswira halisi ya muonekano wa Lewiathani awapo kazini, lakini anapotaka kuonekana na watu huchukua umbile la samaki aina ya nguva (serena).
Behemoth ni jicho la shetani ling’amualo hatima ya mtu tangu akiwa tumboni mwa mama yake, kumbuka Mungu anaweka kusudi la mtu akiwa tumboni mwa mama yake, kumbuka kisa cha Yohana Mbatizaji kujazwa Roho Mtakatifu akiwa tumboni mwa mama yake (Elizabeth), Yakobo alichaguliwa na Mungu tangu akiwa tumboni mwa Rebeka (Mama yake).
Mtu anakuwa mtu tangu akiwa tumboni mwa mama yake, na anasikia kila aambiwalo, maandiko yanasema walijifunza uongo tangu tumboni mwa mama zao, hii maana yake ni kuwa wanaweza kujifunza kitu wangali tumboni.
Hivyo Behemoth huweza kuijua hatima ya mtu akiwa tumboni, hivyo kuiua mapema (destiny killer demon).
Behemoth alijua Musa atawakomboa Waebrania kutoka utumwani Misri, hivyo akaingia katika moyo wa Farao na kupitisha sheria kwamba watoto wote wa kiume wa Kiebrania watakaozaliwa wauawe, aliyekuwa akitafutwa alikuwa ni Musa ili kuzuia ukombozi kwa Waebrania kutoka mkono wa chuma wa Farao.
Behemoth aliiona hatima ya Yesu siku ile alipozaliwa, hivyo akaingia katika moyo wa Herode na kupitisha sheria watoto wote wa kiume chini ya miaka miwili katika Mji wa Yerusalemu wauawe, aliyekuwa akitafutwa alikuwa ni Yesu ili kuzuia ukombozi wa binadamu kutoka katika utumwa wa dhambi.
Mimba nyingi zinaharibika, wanawake wengi wanafungwa matumbo yao (tasa), watoto wengi wanakufa wangali wadogo (pre-mature death), watu wanakuwa vichaa, wendawazimu, mateja na wasio na thamani katika jamii, hii yote ni kazi ya Behemoth.
Kuna wakati anafanya kazi kama ‘monitoring spirit and/or spirit of confusion.’ Kwa hiyo ujio wa shetani duniani uliharibu mfumo wa kiungu ‘divine connection/system’ na kuasisi mfumo mpya wa kishetani ‘demonic system’ kile ambacho binadamu alikatazwa na Mungu kwamba asikifanye, yeye akaanza kukipenda na kukifanya.
Mungu aliweka kanuni zilizotengeneza muunganiko baina yake na mtu, katika mfumo wa Amri Kumi (Kutoka 20:2-17) na baadaye Amri ya Upendo, kwa msingi wa usiibe, usizini, usiue, usiseme uongo wala usitamani mke au mali ya mtu mwingine.
Lakini binadamu akaanza kutenda kinyume; akawa mwizi, mzinzi, muuaji, mpora wake za watu, msema uongo na msengenyaji, mwenye tamaa na hila.
Haya yakiwa ni matokeo ya nje ya kuharibika kwa mfumo wa kiroho ndani ya mtu.
Uovu wote tunaoushuhudia duniani leo hii ni matokeo ya kuharibika mfumo wa kiroho ndani ya mtu. Mungu ndiye muasisi wa kafara ya damu, kwa kuwa damu ndilo chimbuko la uzima na chanzo cha uhai.
Uhai wa kila kiumbe uko katika damu, na tangu kale Mungu amekuwa akipokea kafara ya damu za wanyama. Hata pale alipomuagiza Ibrahimu kumtoa kafara Isaka mwanaye ikiwa ni kuijaribu imani yake, alipoonyesha utayari Mungu aliingilia kati na kuizuia sadaka hiyo, kwa kuwa alijua shetani atawafundisha wafuasi kutoa kafara za watu kwa kumwaga damu zao (kuua).
Mungu alisitisha kafara zote za damu kwa kuimwaga damu yake mwenyewe (Mdo 20:28) isiyo na hatia kwa ukombozi wa binadamu wote.
Kwa hiyo, Mungu aliikataa damu ya Isaka, mtoto wa Ibrahimu lakini akaidai ile damu kutoka kwake yeye mwenyewe kupitia viuno vya Isaka (yule aliyepaswa kuwa kafara).
Vizazi vingi baadaye kupitia mnyororo wa damu (blood genealogy) alizaliwa Yesu aliyeitwa Kristo, damu yake isiyo na hatia ilibeba nguvu ya utakaso ndani yake, hivyo kwa kifo chake aliwatakasa watu wote kutoka katika laana na hatia waliyobebeshwa na wazazi wetu wa kwanza (Adamu na Hawa).
Hii ilikuwa kafara kuu, zile nyingine zote ikiwa ni pamoja na zile za wanyama ulikuwa ni uwakilisho (mifano) wa kafara kuu iliyotokea pale Kalvari.
Na hiyo ilikuwa ndiyo kafara ya mwisho ya damu Mungu kuitaka kutoka kwa mtu. Damu ya Yesu iliyomwagika pale juu msalabani, inatupa ujasiri wa kusimama mbele za Mungu na kuzidai zile baraka ambazo Mungu alituandalia tangu kuumbwa kwa misingi ya ulimwengu.
Kwa hiyo hatupokei baraka kwa nguvu, akili na utashi wetu, hapana, bali tunapokea baraka kutokana na kile alichokifanya Yesu pale juu msalabani.
Yeye alifanyika laana ili sisi tupokee baraka, kwa kuwa imeandikwa amelaaniwa angikwaye mtini. Jukumu letu ni kusimama katika zamu yetu na kutenda kile alichoagiza Mungu, kisha kudai baraka zetu.
Tuwasiliane: [email protected]